2014-01-06 08:43:39

Jiandaeni kikamilifu kabla ya kuanza wito na maisha ya ndoa!


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Kwa mara nyingine tena tuendelee kuhekimishana katika mambo ya muhimu yatakayosaidia kulijenga Kanisa la nyumbani linalofurahi, lililo ishara ya amani na matumaini ya Kanisa na Taifa. RealAudioMP3

Katika kipindi chetu kilichopita, tulihekimishana kwamba ni muhimu kabisa kwa wale wanaopokea wito wa ndoa na familia kujiandaa vema kisaikolojia kabla ya kuingia katika maisha hayo. Katika hili tunakaza kusema, maandalizi ni muhimu. Kwa moyo wa upendo tunazidi kuwageukia vijana wetu na wote wanaoupokea wito huu, JIANDAENI VIZURI.

Mtu usishitukie tu umekuwa mke wa mtu au usishitukie tu umekuwa baba bila kujiandaa. Pamoja na maandalizi hayo ya kisaikolojia; yaani kule kuwa tayari kupokea na kukabiliana na maisha; kuna maandalizi pia ya kijamii. Mnakwenda kujenga familia; bila shaka familia haitakaa juu ya miti au mitaroni, inahitaji makazi adili. Suala la kuwa na nyumba ya familia sio la kulipuuzia kamwe. Kama tunataka kujenga familia ya amani, ambayo ni shule ya maadili na fadhila mbalimbali kwa watoto wetu, ni vema tukawa na nyumba yetu.

Mang’amuzi ya kichungaji yanaonesha, kuna ugumu fulani wa kuratibisha maisha endapo wanandoa wanaishi katika nyumba ya kupanga au wanaendelea kuishi kwa wazazi wao. Katika nyumba za kupanga ambapo kuna wapangaji wa aina tofauti na desturi tofauti, kuna hatari ya watoto wetu kuanza kuiga mielekeo isiyofaa kwa kuona moja kwa moja kutoka kwa majirani. Hata kama familia ikijitahidi kupanda mbegu njema ndani ya mioyo ya watoto hao; bado mhalifu wa kupanda magugu yumo katika baadhi ya majirani. Hili nalo ni vema kulisemea; waanzaji wakumbuke kuandaa makazi!!

Twaweza kusema maisha ni magumu na hali ya uchumi ni ngumu kuanza ukiwa na nyumba, NI KWELI. Lakini kama tukirudi katika falsafa ya muda na vipaumbele; utakuja kugundua kwamba, sherehe zetu nyingi za harusi zinakuwa ni za gharama kubwa mno, kiasi ambacho tungeweza kujenga nyumba nzuri tu na fedha inayobaki ikatusherehekesha.

Kitchen Party ni ya gharama kubwa sana, Send-off ni ya gharama kubwa sana, harusi yenyewe ni ya gharama kubwa sana, baada ya hapo wanakwenda honey-moon kwa gharama kubwa sana, halafu mwisho, wanarudi kujibanza kwenye vyumba vya kupanga, ambamo nafasi haitoshi tena ya kuweka makochi na vitanda na magodoro na friji na TV walizopata zawadi kwenye send-off na harusi.

Je, hadi hapo, suala ni MPANGO-FIKRA au ugumu wa maisha? Si vema kujiandaa kwa kujenga nyumba? Mapindui ya fikra siku moja yatufanye tuwazawadie watoto wetu, nyumba ya kuanzia maisha. Hatusemi tusile na kunywa kusherehekea harusi ya watoto wetu; kusherehekea ni vema, lakini tusherehekee kwa vipaumbele. Sio kula tu, kunywa tu mpaka kupindisha kamati; hadi tunaacha madeni! Hapana.

Baada ya wewe mwenyewe kujiandaa kisaikolojia na kijamii, fuata taratibu-kanuni zilizowekwa na zilizokubalika na mama kanisa mtakatifu. Mafundisho ya ndoa ni hatua muhimu sana kwa wale wanaojindaa. TUSIYAPUUZIE. Wengi siku hizi wanajifanya wapo bize, au wanajua kila kitu. Hapana!! Usijidanganye, maisha hayajulikani, kila siku kuna jipya. Hata lile unalolifahamu, kubali uelezwe na mwingine; mwangwi wake ni tofauti kabisa. Daima Kanisa hujitahidi sana kuweka taratibu za hawa waoanaji kupata mafundisho ya kutosha, wao pamoja na wasimamizi wao. Lakini wengi huwa hawatilii umaanani.

Ni katika mafundisho hayo, waoanaji huhekimishwa juu ya uzazi mwajibifu, juu ya utakatifu na udumifu wa agano la ndoa na mambo mengine mengi. Kumbe ni vema sana kuzingatia.

Wapendwa, mwishoni mwa maandalizi kuelekea kufunga ndoa, tusisahau maandalizi ya kiroho. Kuweka maagano ya ndoa si jambo dogo, na siyo kiigizo. Ni vema pia kukawa na mfungo mfupi {retriti} yenye kuwazamisha hawa ndugu katika uzito na umaana wa sakramenti wanayokwenda kuipokea. Katika mafundisho pamoja na retriti hiyo, tunaamini wanandoa wetu watakuwa wamewezeshwa kuingia na kuanza vema kulijenga Kanisa la nyumbani. Hata makasisi kabla ya kupata madaraja, hufanya mfungo wa SIKU TANO.

Watawa hali kadhalika kabla ya kumwahidia Bwana kwa viapo, nao pia HUFUNGA SANA. Ni katika mfungo huo mtu anatafakari kwa kina zaidi jambo zito analokwenda kuapa mbele za Mungu na watakatifu wake, na papo hapo anachota nguvu ya kiroho ya kuweza kuanza vema maisha hayo. Iweje mtu wa ndoa asifanye mfungo, wakati anaingia katika mfumo wa maisha muhimu kabisa kwa Kanisa na jamii?

Tunaahirisha mada yetu ya leo kwa kukazia tena kwamba: ndoa ni wito, walioitwa tu wanapokea, lakini katika kuupokea wito huo, ni vema kujiandaa kisaikolojia, kujiandaa kijamii na kujiandaa kiroho. Katika kipindi kijacho, tutaendelea kuangazia juu ya ushiriki wa jamii katika maandalizi hayo. Kutoka katika Studio za Radio Vatican, tunakutakia heri na na baraka kwa mwaka mpya. Ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.