2014-01-06 09:01:38

Epifania, kielelezo cha mshikamano na watenda kazi katika shamba la Bwana Barani Afrika


Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana nchini Ufaransa na katika nchi nyingi za Ulaya ni kielelezo cha mshikamano wa upendo kwa ajili ya Familia ya Mungu Barani Afrika. Ni siku ambayo Majimbo mengi yanatoa mchango kwa ajili ya kusaidia jitihada za shughuli za kichungaji zinazofanywa na Majimbo mbali mbali Barani Afrika, katika mchakato wa kumkomboa mwanadamu: kiroho na kimwili. Kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho Sherehe ya Epifania kwa Mwaka 2014 “Tuwasaidie watenda kazi katika shamba la Bwana”.

Inasikitisha kuona kwamba, habari nyingi zinazopewa uzito wa kwanza na vyombo vya habari vya kimataifa kutoka Afrika ni: baa la njaa, vita na umaskini, lakini hata katika hali kama hii, Kanisa linaendelea kutekeleza dhamana na utume wake, kiasi kwamba, waamini wengi wamekuwa ni kielelezo cha furaha, huruma na upendo wa Mungu kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.

Hii ni changamoto kwa viongozi wa Kanisa Barani Afrika kuendelea kuwa ni vyombo vya haki, amani na upatanisho wa kweli kama ambavyo Mababa wa Sinodi ya Awamu ya Pili ya Maaskofu wa Afrika wanavyokazia. Waamini wajifunge kibwebwe kutangaza na kushuhudia upendo wa Kristo kwa jirani zao. Leo hii Kanisa linachangamotishwa kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko kuganga na kuponya madonda ya chuki, uhasa na vita kati ya watu, ili kila mtu aonje huruma na upendo wa Mungu.

Hizi ni juhudi za Mashirika ya Kipapa ambayo yanataka kuona kwamba, Bara la Afrika linapewa uzito linalostahili katika maisha na utume wa Kanisa na kamwe lisisahaulike kama ambavyo aliwahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alipokuwa anazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki kutoka Jamhuri ya Afrika ya kati walipokuwa wanafanya hija ya kitume mjini Vatican kunako Mwaka 2007.

Mshikamano na Familia ya Mungu Barani Afrika ni mchakato ulioanzishwa na kunako Mwaka 1888 na Kardinali Charles Martial Allemand Lavigerie, alipokuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Algeri, muasisi wa mapambano dhidi ya biashara haramu ya utumwa. Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2013, Kanisa limesherehekea Kumbu kumbu ya Miaka 125 tangu kuanzishwa kwa Kampeni hii.

Kwa kuguswa na mateso pamoja na dhuluma zilizokuwa zinafanywa dhidi ya Waafrika, Baba Mtakatifu Leo wa Kumi na tatu, Novemba 1890 akaanzisha Siku maalum ya mshikamano na Bara la Afrika.








All the contents on this site are copyrighted ©.