2014-01-04 12:14:57

Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipotembelea Yerusalem!


Ilikuwa ni tarehe 4 Januari 1964, takribani miaka 50 iliyopita, Baba Mtakatifu Paulo wa sita alikuwa anaanza hija ya kichungaji Nchi Takatifu na kuhitimisha safari hii ya kihistoria, jioni baada ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, maarufu kama Epifania ya Bwana.

Waamini wapatao millioni moja walikusanyika kutoka sehemu mbali mbali za Nchi Takatifu ili kumpokea na kumsalimia Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tangu wakati huo, utume wa Mapapa ukabadilika na kuanza kupata sura na mwelekeo mpya, wakitekeleza dhamana na utume ambao ulianzishwa na Kristo mwenyewe kwa kumkabidhi Mtakatifu Petro ufunguo wa Kanisa!

Hija ya kichungaji iliyofanywa na Papa Paulo wa Sita, ilikuwa ni nyepesi, iliyojikita katika: moyo wa Sala na Ibada; toba na upendo. Lengo lilikuwa ni kufanya hija ya maisha ya kiroho ili kutoa heshima ya pekee kwa maeneo ambayo Mtakatifu Petro aliishi na kutekeleza utume wake. Ilikuwa ni tarehe 4 Desemba 1963, mara baada ya Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Papa Paulo wa sita alipotangaza kwamba, alikuwa na wazo la kutembelea Nchi Takatifu.

Huu ulikuwa ni mwanzo mpya katika historia ya Kanisa katika mchakato wa kukabiliana na changamoto za Majadiliano ya Kidini na Kiekumene, ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu. Baba Mtakatifu Paulo wa sita, alibahatika kukutana na kuzungumza na Patriaki Atenagora wa Costantinopoli, baada ya miaka mingi ya kinzani, chuki na migawanyiko ya Kikanisa.

Viongozi wakuu wa Makanisa wakakutana kwa pamoja mjini Yerusalem, kwenye chemchemi ya Injili na kufungua ukurasa mpya wa Majadiliano ya Kiekumene, unaoendelea kufanyiwa kazi kwa zaidi ya miaka hamsini kwa sasa, ili wote waweze kuwa ni wamoja chini ya Kristo mchungaji mkuu.







All the contents on this site are copyrighted ©.