Epifania ya Bwana: Dhahabu, Uvumba na Manemane! Kazi kwako!
Sikukuu ya Epifania inayoitwa pia Tokeo la Bwana ni sherehe kubwa sana kwa wakristu.
Kwa bahati mbaya siku hii imegeuzwa kuwa kama ya maigizo ya watoto wanaopita kuimba
nyumba hadi nyumba na kupata zawadi. Kwa hiyo badala ya kuwa Epifania tungeweza kuiita
kwa kiingereza Happy-funny.
Sikukuu ya
leo inayo mafundisho ya maisha yanayoweza kumtosha kila mtu. Ukifaulu kutanguzana
kidhati na wasafriri wanaotajwa katika sikukuu ya leo watakufikisha kwenye uhondo
wa maisha. Wasafiri hao wanaitwa majusi. Wametokea mashariki ya mbali wakielekea Betlehemu.
Wasafiri hao hawatajwi idadi wala majina kama tunavyosadikishwa kuwa walikuwa watatu.
Tunaambiwa tu Kulikuwa majusi kutoka mashariki ya mbali.
Msafiri yeyote ni
mtu wa kuja siyo mwenyeji, ndiyo maana anaitwa “Msafiri kafiri.” Kama wewe ni msafiri
tu hapa duniani, basi hata wewe ni kafiri. Wasafiri wenzako, yaani majusi hawakutembea
mikono mitupu, walichukulia tunu au zawadi. Tunu hizo zilikuja kutambulika mwishoni
mwa safari yao tena baada ya kumwona mototo Yesu na mama yake, ndipo tunaambiwa, wakatoa
tunu zao yaani dhahabu, ubani na manemane. Kutokana na aina ya zawadi walizobeba tunaweza
kujua huyu mtoto waliyemtembelea alikuwa wa aina gani.
Kwa mantiki hiyo, katika
msafara wa maisha yetu hapa duniani, kila mmoja ni kama tunu au zawadi za kumkabidhi
Mungu sasa hivi na hata baada ya maisha ya hapa duniani. Hebu tujaribu kuzitafakari
tunu hizo walizozibeba wasafiri wenzetu na tujitafakari sisi wenyewe.
DHAHABU:
Ni kito au jiwe la thamani sana. Uthamani wake upo katika uzito wake, uimara, kudumu,
uzuri na kupendeza kwake katika kung’aa, dhahabu haipati kutu na wala haichujuki.
Watu wengi wameteseka, kuitafuta kwa udi na uvumba pengine hadi kufa. Wewe fuatilia
tu vituko vilivyo kwenye machimbo. Mwenye dhahabu ni mtu tajiri sana, hata mfumo wa
thamani ya fedha unapimwa kutokana na kiwango cha dhahabu.
Dhahabu ni jiwe
asilia lililogeuzwa hali yake kwa kuunguzwa kwa moto mkali sana ulioko ardhini uitwao
volcano. Hiyo ni kazi ya huluka (nature), yaani, Mungu ameficha raslimali ndani ya
tumbo la mama ardhi. Kwa hiyo utafutaji na uchimbaji wa dhahabu unaonesha thamani
ambayo Mungu ameihifadhi kwenye udongo kwa miaka elfu nyingi. Kadhalika hali ya kumtafuta
Mungu katika imani. Kwa vile imani inayo thamani zaidi ya dhahabu watu wamepigania
kuipata, watu wamefia imani yao kama wachimbaji wadogowadogo wanaofukiwa kwenye migodi.
Baada
ya kuichimbua ikiwa katika hali ya udongo yabidi kuihakikisha kama kweli ni dhahabu
kwani “si kila king’aacho ni dhahabu”. Masonara hufanya hivyo kwa kuiunguza kwenye
jiko (tanuru) la moto wenye joto la selsius elfu moja mia mbili. Kwa kawaida ukiunguza
tani moja ya udongo wa dhahabu unapata gram 2 tu za dhahabu.
Kishapo vyembevyembe
vya dhahabu iliyosafishwa hufinyangwa kulingana na ukubwa wa kikombola chenye umbo
kama la tofali dogo. Hapa ndipo dhahabu inapozidisha thamani yake. Hatua hii ya kusafishwa
inaitwa pia kujaribiwa dhahabu, nayo inalinganishwa na mateso anayopata mtu katika
maisha ya imani. [Jiko la kuunguza almasi linaitwa Kalibu, na jiko la dhahabu linaitwa
tanuru, lakini tanuru la kuunguza moyo wa mtu ni Mungu mwenyewe: “Kalibuni kwa fedha
na tanuru kwa dhahabu bali Bwana huijaribu mioyo”(Methali 17:3)].
Wayahudi
waliyachukua mateso waliyokuwa wanayapata kuwa ni kujaribiwa. Daima wapatapo mateso,
yawe ya vita, au kuchukuliwa utumwa walikuwa wanasali “ Ee Mungu umetujaribu kama
dhahabu katika tanuru.” (Hekima 3:6-9); Mungu atupatia mateso ili kutusafisha.
Ndugu
yangu, ni kweli kwamba kuwa na imani ya dini yako ndiyo dhahabu yako hiyo. Lakini
huko ni sawa na kuwa na dhahabu iliyochanganyika na udongo, bado unahitaji kujaribiwa
katika tanuru la mateso ili kutakaswa na kuwa imara na thabiti. Kazi ngumu ya masonara
ni ya kuiunguza dhahabu katika tanuru la moto mkali hadi inang’aa. Sisi pia tunahitaji
sonara – au shule – ili dhahabu –imani – ijaribiwe.
Kwa mateso imani utaing’arisha
na itapendwa na kufuatwa.”Kibaya chajitembeza, chema chajiuza chenyewe”. Mkristo mwenye
imani iliyotakaswa ni yule anayejiaminisha, anayejisadikisha mwenye "conviction" –
katika kila hali ya maisha. Bahati mbaya siku hizi imani hiyo imegeuka kuwa imani
ya kwenye mikutano, imani ya mapambano, ya mikataba, ya kushawishiana, imani hiyo
ni dhahabu feki hata kama inang’aa “Kwani si kila king’aacho ni dhahabu.” Tunahitaji
mtu mwenye imani thabiti, mkakamavu mwenye kujizatiti. Katika kipengee hicho, ninamwombeni
radhi nikisema: “Ashakum si matusi” kwamba wakristu wengi hatujakomaa kiimani.
Tuko
bado watoto wadogo kwa vile hatujaisafisha imani yetu katika tanuru la moto mkali
wa dhahabu. Mathalani bado hatulielewi Neno la Mungu. Kama tunaelewa basi labda ni
kile kidogo tulichojifunza kabla ya kupata komunio ya kwanza, au pengine kwenye mahubiri
ya padre siku ya dominika kama naye ameamka vizuri. Kutokana na kutojaribiwa huko,
wakati mwingine unapata picha kwamba wakristu wana woga wa kuienjilisha imani yao
kwa matendo. Ili kuwa mkristo leo yabidi kuwa shujaa, imara, thabiti mwenye kuweza
kujikabili katika imani hiyo, hasa katika matatizo ya maisha.
Takataka nyingi
sana zimejinasa kabisa katika dhahabu ya imani yetu, tunabaki kuwa tu na nia njema
ya kujilaumu lakini bila kuwa na nguvu ya kujinasua kwa kujisafisha katika tanuru
la moto wa majitoleo. Mathalani uchafu mzito wa rushwa ulionasa vibaya katika maisha
yetu. Mkristu anajua kabisa kwamba “Mungu wetu si Mungu wa Rushwa”. Kwa nini basi
usianze wewe kujitia katika tanuru hilo la moto la kusafisha. Huko ndiko kuwa dhahabu,
iliyojaribiwa na ikawa dhahabu hai inayompendeza Mungu.
UBANI-UVUMBA: Zawadi
nyingine waliyobeba majusi ilikuwa ubani. Ubani kama manemane tutakayoyaona hapo mbele,
hutokana utomvu wa mti wa pekee unaoitwa mbani au manemane. Utomvu ni machozi ya mti
unapokatwa. Utomvu huo ukiganda hukusanywa na kuhifadhiwa. Ubani ukiwa umefungwa tu
kwenye mfuko au boksi, unafaa kwa kuuangalia tu, na pengine huwezi kuugundua. Ubani
unatambulikana pale tu unapounguzwa. Ukitaka kuufaidi ubani, tia penye makaa ya moto,
ndipo unaleta harufu nzuri. Ndiyo maana ubani unaitwa pia uvumba, na manemane huitwa
manukato.
Tungeweza pia kuita "perfume" – msamiati utokanao na maneno mawili
ya kilatini "per fumare" – kwa njia ya moshi. Kutokana na hali yake ya kunukia ubani
unatumika katika mazingira mengi sana. Ubani unasafisha hewa ya mahali ilipochafuka
kwa namna mbalimbali hata, kwa uhasama, wasiwasi, machungu, magomvi, masikitiko. Harufu
ya ubani inamliwaza mtu kiakili. Paolo anasema: “Nimepokea toka mkono wa Epafrodito
vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo
Mungu” (Fil.4,18)
Harufu ya ubani ni alama pia ya upendo. “Mkaenende katika
upendo, kama Kristu naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka
na dhabihu kwa Mungu kuwa harufu ya manukato” (Ef.5,2). Harufu ya ubani kwa ajili
ya tafakari na sala. Katika zaburi sala na masifu kwa Bwana yanalinganishwa na harufu
tamu ya ubani ipae juu “Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba” (Zaburi 140). Hadi
sasa ubani unatumika wakati wa ibada kama alama ya uabudu na ya sala, ya kuheshimu
mtu au kitu wakati wa madhehebu. Kwa hiyo moshi wa ubani ni alama ya sala zinazopaa
mbinguni na hulinganishwa pia na majitolea ya mashahidi mashemasi Stefano na Laurenti.
Majusi
walibeba tunu ya ubani – uvumba, uliokuwa umefungwa katika boksi wakaenda kumfungulia
mtoto Yesu. Nadhani uliunguzwa mbele yake, hasa ukizingatia palikuwa na hewa ya kizizini.
Sisi wenyewe na imani yetu ni ubani. Lakini endapo imani hiyo inabaki imefungwa tu
ndani ya mtu au ndani ya kanisa, imani hiyo inafaa kwa kuiangalia tu, hainukii. Kama
ulivyo ubani, imani yafaa iunguzwe ili kueneza harufu ya Kristo.
Kama vile
leo iitwavyo Tokeo la Bwana, maana yake Kristu anaonesha utukufu wake unaoshinda
giza lililobado limetanda ulimwenguni. Ni jukumu lako mkristu kama hawa majusi, kuonesha
au kudhihirisha mpango wa Mungu kwamba watu wameitwa kushiriki urithi huohuo kushiriki
mwili huohuo kushiriki katika ahadi hiyohiyo kwa njia ya injili. Yabidi kuifukiza
harufu nzuri ya imani uliyo nayo. Je, ni nani hao wanaotakiwa kufukiziwa perfume
hiyo ya ubani? Kwanza kabisa Mungu mwenyewe, anayetaka tumtolee maisha yetu na sala
zetu kama fukizo kuonesha uabudu wetu. Kadhalika watu wengine walioko kila mahali
wanaosubiri mchango wetu wa kushirikisha harufu hii tamu ya Neno la Mungu.
Wanaweza
kuwa vijana waliokosa mwelekeo wa maisha, wazee waliosahauliwa, wagonjwa, vilema,
watoto, maskini hata maadui wetu nk. Wanaosubiri mchango wetu katika imani, kama vile
harufu nzuri ya ubani uliounguzwa na kueneza harufu nzuri ya upendo wa Yesu Kristu.
Lakini, yabidi pia kuwa makini unapofukiza ubani wako, kwa wengine wanayo alleji ya
moshi. Moshi ambao hata kabla ya kuunusa unaanza kuukohoa na kutoroka. Kumbe ubani
wenye moshi mtamu unaonukia na usiokuwa na alleji kwa yeyote yule ni upendo. Ule uwezo
wa kujibu mahitaji, matatizo na mategemeo ya watu wa leo. Huo ndiyo ubani unaotegemewa,
huko ndiko kuunguzwa, ndiyo ushahidi katika Kristu. Hiyo ndiyo imani ya kweli.
MANEMANE
- MANUKATO: Zawadi ya tatu waliyobeba majusi ilikuwa Manemane. Manemane, maana yake
“chungu”. Asili na jinsi inavyopatikana manemane ni kama ile ya ubani. Manemane yalijulikana
na kutumika katika Misri ya kale katika kupaka maiti. Kadhalika huko mashariki ya
mbali manemane yalitumika kumhifadhi marehemu. Katika Biblia, manemane ni moja ya
vitu muhimu vinavyochanganywa kwenye mafuta matakatifu (Kutoka 30:23). Manemane yalitumika
pia kama dawa, kwa ajili ya kuponya au kupunguza maumivu, yasemwa hata Yesu alipokuwa
anateswa alipewa mvinyo uliotiwa manemane lakini hakupokea (Mk. 15:23). John anasema
Nikodemu alileta paundi 75 za manemane kumpaka Yesu alipoingizwa kaburini.
Siku
za leo manemane yangeweza kulinganishwa na dawa za kuhifadhia maiti. Katika maduka
mengi hasa huko ulaya yanauza dhahabu tu wameandika “Compro oro” yaani ninanunua dhahabu.
Kwetu uswahilini yako maduka mengi yanayouza ubani-uvumba au udi. Lakini maduka machache
yanauza “manemane” yaani mafuta ya kuhifadhia maiti.
Mababa wa kanisa, wametaka
tuone katika tunu hii ya manemane picha ya Kristu aliyekabili kishujaa mateso na kifo
chake kwa ajili ya kuwapenda watu wote. Kwa hiyo manemane ni alama ya mateso, ya kujihatarisha
hasa na hasa inamaanisha msiba. Mtu anayekabili mateso na kifo ipasavyo anaitwa shujaa
au askari hodari. Kwa hiyo manemane ni alama ya ushujaa wa imani.
Watu wengi
leo hatuna ushujaa isipokuwa tunao ushupavu. Ushupavu wa imani maana yake ni ile hali
ya kutetea imani yako hadi kufa lakini bila ya kuijua maana yake. Ushupavu aina hiyo
tunauita ushirikina. Ushirikina ni kule kuifuata dini na hasa kuitetea bila kuijua.
Huo ni uadui mkubwa na mbaya sana unaoweza kuidhurumu dini yako, afadhali mtu yule
anayeichukia dini yake lakini anaijua huyo anasaidia kuisafisha dini yake ili ing’ae.
Ushupavu mwingine uliojaa woga sana, ni ule wa kuteseka kishahidi kwa kulowa damu
za wengine uliowajerui au kuwaua, badala ya kulowa damu za majeraha yako mwenyewe
ya kutetea haki za watu na za kuwapenda wengine.
Ni rahisi sana kuiainisha
jamii ya leo inapenda aina gani ya maisha. Leo tunayo jamii iliyotawaliwa na utajiri,
mali au dhahabu. Yaani watu wanaopenda maraharaha, viongozi wanaojilundikia mali nk.
Jamii namna hiyo inapenda pia kusifiwa, kuabudiwa, kupendwa sana, kushabikiwa, yaani
kufukiziwa ubani unaonukia. Jumuia ya leo haipendi kusafishwa, wala kuunguzwa hasahasa
mateso na kifo kama manemane. Hakuna ushujaa wa kushuhudia imani yako au taifa lako.
Wakristu wa leo tunao woga wa kuonesha ushujaa.
Tunaficha imani yetu. Tuangalie
sana tusifanye kama wakuu wa makuhani na waandishi wanaojua kila kitu lakini hawafuati
ukweli. Kumbe majusi wa leo daima wanatafuta ukweli. Ukweli ambao Pilato anamwuliza
Yesu wakati wa kumhukumu “Ukweli ni kitu gani?”
Ndugu zangu, baada ya msafara
huu mgumu na Majusi, tunaona kuwa hii siyo tena Happy-funny, bali ni Epifania ngumu.
Basi pamoja na majusi hao tujaribu kufungua tunu zetu, na tumwombe mtoto Yesu azipokee.
Hata kama ni tunu dhaifu, lakini tumwombe pamoja na kanisa tukisali “Ee Bwana tunakuomba
usiziangalie dhambi zetu, bali angalia imani ya kanisa lako. Utujalie amani na umoja
kama yalivyo mapenzi yako. Unayeishi na kutawala daima na milele. Amina”.
Tafakari
hii imeandaliwa na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.