2014-01-03 12:08:31

Ungeni mkono juhudi za Papa Francisko dhidi ya baa la njaa duniani!


Kardinali Sèan Brady kutoka Ireland anawaalika waamini, viongozi, taasisi na mashirika mbali mbali ya misaada, wanaoamini katika dhana ya dunia inayotawaliwa kwa misingi ya haki, amani na mshikamano, kuunga mkono juhudi za Baba Mtakatifu Franciko katika mchakato wa kupunguza na hatimaye kutokomeza kabisa baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2025.

Jambo hili linawezekana ikiwa kama watu watashirikishana upendo kwa kutambua kwamba, binadamu wote wanaunda familia moja, inayopaswa kusaidiana kwa hali na mali. Kardinali Sèan Brady katika ujumbe wake kwa Mwaka Mpya 2014 anafanya rejea kampeni iliyozinduliwa hivi karibuni na Shirikisho la Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha unaoendelea kusababisha majanga kwa mamillioni ya watu duniani.

Caritas Internationalis katika kampeni yake dhidi ya baa la njaa iliyozinduliwa hapo tarehe 9 Desemba 2013 inaongozwa na kauli mbiu "Familia moja ya binadamu. Chakula kwa wote". Kardinali Sèan Brady anasema, matashi yake kwa Mwaka Mpya wa 2014 yanajikita katika furaha na matumaini yanayopania kujenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu na wote wanaoteseka kutoka sehemu mbali mbali za dunia hasa kutokana na baa la njaa na utapiamlo.

Kuna watu wanateseka kutokana na maafa asilia yaliyojitokeza katika siku za hivi karibuni huko Ufilippini; watu wanaendelea kunyanyasika na kudhulumiwa utu na haki zao msingi huko DRC na Syria; bado kuna mamillioni ya watu ambao amani na utulivu vinaendelea kuwa ndoto, kwani hawafahamu ni siku gani ambapo mtutu wa bunduki utaweza kutulia na kuwapatia fursa ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu.

Ni matumaini ya Kardinali Sèan Brady kwamba, waamini wataendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu, lakini pia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wataonesha utashi wa kisiasa wa kutaka kupata suluhu ya migogoro na kinzani za kivita na kijamii inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Watu wanataka kuonja ukombozi ulioletwa kwa kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu, Mfalme wa Amani.

Baa la umaskini na njaa kwa mamillioni ya watu, bado halijapata ufumbuzi wa kutosha kutokana na ubinafsi, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka mambo ambayo hayazingatii wala kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kila mtu akitekeleza dhamana na wajibu wake katika Jamii, baa la njaa na umaskini linaweza kupewa kisogo! Ni matumaini ya Kardinali Sèan Brady kutoka Ireland kwamba, Mwaka 2014 utakuwa ni Mwaka wa Amani, inayobubujika kutoka kwa Kristo, Mfalme wa Amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.