2014-01-03 08:58:50

Mtakatifu Pietro Favre, SJ.


Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 77 tangu alipozaliwa, aliridhia ombi la Kardinali Angelo Amato la kutaka Pietro Favre atangazwe kuwa mtakatifu kwa kufuata kanuni mlinganyo! RealAudioMP3
Takwimu zinaonesha kwamba, ni watakatifu 40 tu ambao wametangazwa kwa kuzingatia sheria hii katika historia ya Kanisa. Kati yao ni Mtakatifu Gregori VII, Getrude wa Helfta. Petro Damian, Cyril na Metodi; Yohane wa Damascene, Mwenyeheri Beda, Albert Mkuu, Thomas More na Yohane wa Avila.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 9 Oktoba 2013 ametumia kanuni hii kumtangaza Mwenyeheri Angela wa Foligno, kuwa Mtakatifu. Kardinali Amato anasema kwamba, ili mwamini aweze kutangazwa kuwa Mtakatifu kwa kuzingatia kanuni mlinganyo kuna haja ya kuwa na sifa kuu zifuatazo: Ibada kwa mtakatifu husika. Kwa miaka mingi waamini walimkimbilia Mwejnyeheri Pietro Favre kama mwombezi mwema mbele ya Mwenyezi Mungu. Watu waliokimbilia msaada wa maombezi yake walijaliwa kupata yale waliyoomba.
Pili, Mwenyeheri anapaswa kuwa na kumbu kumbu za kihistoria zinazoonesha alama na karama zake za utakatifu, kwa mwenyeheri Pietro Favre, Myesuiti, kuna nyaraka mbali mbali zinazoonesha karama na utakatifu wake wa maisha. Tatu ni ushuhuda wa miujiza inayotendeka kwa maombezi ya mwenyeheri Pietro Favre imeendelea kusikika hadi nyakati hizi.
Sifa zote hizi zimemwezesha Baba Mtakatifu Francisko kutumia kanuni ya mlinganyo kumtangaza Mwenyeheri Pietro Favre kuwa mtakatifu na mwombezi wa Kanisa zima; kwa kusali kwa ajili ya maombezi yake; kwa kuonesha katika nia ya misa, bila ya kuwa na hati maalum wala maadhimisho ambayo kwa kawaida yanafanywa na Mama Kanisa.
Historia inaonesha kwamba, Pietro Favre ni kati ya wanafunzi wa mwanzo kabisa wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Alipadrishwa tarehe 15 agosti 1534 na kuwa mwanashirika wa kwanza wa Wayesuiti kuweka nadhiri zake. Akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 40 tu. Tangu wakati huo, watakatifu na watu mashuhuri ndani na nje ya Kanisa waliwataka Wayesuit kutoa heshima na upendeleo wa pekee kama walivyokuwa wanafanya kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola, mwanzilishi wao.
Alikuwa ni mtu wa mageuzi, aliyeshiriki kikamilifu katika kufundisha Katekesi; Maandiko Matakatifu na kuhubiri. Alishiriki katika Mtaguso wa Trenti. Alikuwa mtiifu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu kwa kusali, kusoma na kutafakari; akaonesha fadhila na moyo wa shukrani. Alikuwa ni mnyenyekevu na mtiifu; akachagua kumwilisha ndani mwake nadhiri ya Ufukara kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kudharauliwa na wengi. Alijitoa bila ya kujibakiza katika huduma wala hakupenda kupoteza wala kuwapotezea wengine muda, kwani kwake hiki kilikuwa ni kipimo cha uungwana.
Mtakatifu Pietro Favre ni mfano na kielelezo cha Upadre; mtawa na mtu wa sala, mwaliko kwa Makasisi kuwa kweli ni wahudumu wa Neno, Sakramenti na Maisha ya Watu wa Familia ya Mungu; daima wakijitahidi kuiga mfano wa Yesu Kristo mchungaji mwema; ili kuendeleza mchakato wa kazi ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri watumie vyema karama na vipaji vyao kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, Kristo na Kanisa.
Alitumia vyema milango yake ya fahamu kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu; changamoto kwa wakleri kujenga na kuimarisha moyo wa udugu na urafiki na: waamini walei, watawa, maskini na matajiri. Wawe tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na Jirani zao.
Mtakatifu Pietro Favre ni mfano na kielelezo cha mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika maisha ya sala, upatanisho na mshikamano wa kidugu. Wakati wa masomo na majiundo yake ya Kikasisi alionja Mafundisho ya Kiluteri, lakini akasimama imara katika imani yake. Ni mtakatifu aliyependa maisha ya Kijumuiya, kwani kwake, Jumuiya ilikuwa si tatizo la kutafutiwa ufumbuzi, bali Fumbo linalopaswa kukumbatiwa.
Ni mtakatifu aliyetegemea tunza, msaada na maongozi ya Kimungu. Kwa hakika anasema, Kardinali Angelo Amato, Mtakatifu Pietro Favre ni mfano na kielelezo cha kuigwa katika maisha ya Kipadre na Kitawa na kwamba, ni “Jembe” la nguvu katika Uinjilishaji Mpya; tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kutangaza Ufalme wa Mungu. Alijiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwa ni chombo cha kuyatakatifuza malimwengu.








All the contents on this site are copyrighted ©.