Neno la Mungu ni nguvu inayosukuma kwa kasi kubwa zaidi mchakato wa Uinjilishaji Mpya,
katika ulimwengu mamboleo, ambamo watu wanaonekana kumezwa zaidi na malimwengu. Kutokana
na ukweli huu, Neno la Mungu halina budi kuwa ni dira na mwongoz wa shughuli na mikakati
ya kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa.
Hii ni sehemu
ya barua ya kichungaji iliyoandikwa na Askofu mkuu Andrew Soo-jung wa Jimbo kuu la
Seol, Korea ya Kusini kwa ajili ya Mwaka 2014, Mwaka wa Uinjilishaji Mpya Jimbo kuu
la Seoul. Waamini wanahamasishwa kujenga na kukuza utamaduni wa kupenda: kusoma, kulitafakari
na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo
cha Imani tendaji.
Waamini wajenge ujasiri wa kutaka kushirikishana na kumegana
Injili ya Furaha kwa kuanzia katika: Familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na mahali
pa kazi. Waamini wajitahidi kulifahamu kwa kina Neno la Mungu ili liweze kuwa ni dira
na mwongozo wa maisha adili na matakatifu.
Askofu mkuu Andrew Soon-jung anasema,
imani inapata chimbuko lake katika Neno la Mungu; inakuwa na kukomaa kwa kuboreshwa
na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kutoa harufu
nzuri inayojikita katika matendo ya huruma na mapendo, kama anavyohimiza Baba Mtakatifu
Francisko.
Waamini wanaendelea kuhimizwa kuhakikisha kwamba, matunda ya neema
na baraka walizojipatia wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yanaendelezwa kwa
ari na moyo mkuu zaidi, ili watu waguswe na ushuhuda unaotolewa na waamini sehemu
mbali mbali za Jimbo kuu la Seoul. Ndiyo maana, umuhimu wa Neno la Mungu unapewa kipaumbele
cha kwanza katika mikakati ya shughuli za kichungaji Jimboni humo.
Waamini
wasome na kulitafakari Neno la Mungu. Mapadre katika mahubiri yao, wahakikishe kwamba,
Kristo anakuwa ni kiini cha mahubiri yao na wala si vinginevyo. Familia ya Mungu inahamasishwa
kujifunga kibwebwe ili kuwatangazia Watu wa MataifaInjili ya Furaha, inayosimikwa
katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani.