Injili ya Kristo inatangazwa kwa njia ya Unyenyekevu, Udugu na Mapendo makuu!
Baba Mtakatifu Francisko, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Jina takatifu la Yesu,
Ijumaa tarehe 3 Januari 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la
Yesu mjini Roma kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka zake kwa
ajili ya kutangazwa Pietro Favre kuwa Mtakatifu. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu
anawaalika Wayesuit kumwiga Yesu Kristo katika fadhila ya unyenyekevu; kwa kuwaza,
kupenda na kutenda kama alivyofanya Yesu mwenyewe kama inavyojidhihirisha kwenye Fumbo
la Msalaba.
Baba Mtakatifu anawahamasisha Wayesuit kujitosa kimasomaso kwa
kumpatia Yesu na Kanisa lake kipaumbele cha kwanza badala ya kujitafuta wenyewe; kwa
kutenda yote kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, vinginevyo Shirika linaweza kuyumba
na hatimaye, kusambaratika!
Wayesuit wajitahidi kumtafuta Mwenyezi Mungu maadam
anapatikana, wakitambua kwamba, kama binadamu wana mapungufu yao, hivyo wanapaswa
kujipatanisha na Mungu, ili kuonja upendo na huruma yake. Wapige moyo konde na kutoka
kifua mbele kutangaza Injili ya Kristo kwa ari na ujasiri mkuu, kama alivyofanya Mtakatifu
Pietro Favre.
Katika maisha yake, alikuwa ni mtu wa kawaida, mwenye utajiri
mkubwa wa maisha ya ndani; akafanikiwa kujenga na kuimarisha urafiki na watu wa matabaka
yote ya kijamii. Kwa maongozi ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, alijifunza kufanya maamuzi
makubwa katika maisha yake. Alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti na mwenye mwono mpana
zaidi katika maisha na utume wake.
Baba Mtakatifu anawakumbusha Wayesuit kwamba,
nguvu ya Kanisa inatokana na uwezo wake kuratibu na kusimamia mambo chini ya maongozi
ya Mwenyezi Mungu. Wawe tayari kusikiliza na kuitambua sauti ya Mungu, kwa kusaidiana
wao kwa wao kama inavyobainisha Katiba yao ya Shirika na kama alivyofanya Mtakatifu
Favre.
Katika mawazo na matendo yake, alitoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi
Mungu, akawa tayari kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ari na moyo mkuu. Injili
ya Kristo inatangazwa kwa njia ya unyenyekevu, udugu na mapendo makuu na wala si kwa
fitina wala kijicho! Moyo wa binadamu hauna budi kutamani mambo makuu na yale ya maana
zaidi; yaani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo, ili kushiriki kikamilifu
katika mchakato wa kumtafuta Mungu; tayari kwenda pembezoni mwa Jamii kuwashirikisha
wengine huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake.
Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu
Favre alifanikiwa kuwa ni msafiri, akiwa amesheheni kiu na njaa ya kumtangaza Kristo,
changamoto na mwaliko kwa waamini kufanya tafakari ya kina, katika hali ya sala na
ukimya, ili kumwomba Mtakatifu Pietro Favre aweze kuwasaidia kupata ari na mwamko
kama wake. Licha ya mapungufu yao ya kibinadamu, bado kama Wayesuit wanayo hamu ya
kutembea katika mwongozo wa Yesu mwenyewe; wakiendelea kuishi maisha yenye ari kuu:
kwa kuwaza na kuishi kama alivyoishi Kristo kwa njia ya kujitosa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.