2014-01-03 09:45:50

Changamoto za maisha ya kifamilia katika ulimwengu mamboleo!


Mama Kanisa anapoendelea kufanya tafakari ya kina kama sehemu ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha tafakari ya kina iliyotolewa na Padre Stefano Kaombe, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Jimbo kuu la Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.
Kuna mtoto jana alimuuliza mama yake, “Kwa nini Yesu, ambayae ni Mungu alimkimbia Herode, mwanadamu anayetak kumuua? Ina maana Mungu anamuogopa mwanadamu?” Swali hili ungeulizwa wewe leo ungejibu nini?

Ndivyo leo tulivyo, wanadamu tunataka kujikweza, tufanane na Mungu. Matokeo yake tunataka kusifiwa, ukienda kwenye sherehe utasikia “itifaki imezingatiwa”, ni lazima utambue uwepo wa mtu fulani. Kwa kutaka kufanana na Mungu mwanadamu anajilimbikizia mali, anatafuta mali kwa kila namna hata ikibidi kuwa fisadi. Kuna wengine matajiri na bado wanakuwa mafisadi, hawaridhiki. Mko huku kanisani! Mnajilimbikizia mali ili mfanane na Mungu!

Tuanze na Yosefu:
Yosefu Mtii kabisa- anatii maagizo yote ya malaika, haulizai wala hatoi sababu ya kutotii. Mtu mwingine aliyewahi kupewa maagizo kama Yosefu ni Musa. Alitokewa na Mungu katika kijiti kinachowaka moto, akaambiwa “Musa nakutuma chukua taifa langu ulitoe Misri, ulipeleke nchi ya ahadai.” Musa akaanza kuto visingizio, kwa Mungu kwamba “Waisrael wana mioyo migumu, pia mimi nina kigugumizi, nitaongeaje nao?” Mungu akamwambia nitakupa mdogo wako awe masaidizi wako, nitakuwa nawe nikifanya miujiza mbalimbali. Ndipo Musa akakubali, lakini pamoja na hayo yote, tunajua Musa hakufika nchi ya Ahadi. Yosefu hatoi sababu yoyote, kwamba labda katika safari atafanyaje akipambana na majambazi, wanyama wakali au atafikia wapi. Anatii na kutekeleza maagizo ya malaika.

Katika Biblia nzima ukisoma hakuna sehemu Yosefu anapozungumza, yeye anasikiliza na kutii. Ukimya unatuingiza ndani kabisa ya uwepo wa Mungu. Yosefu anasikia sauti ya Mungu kutokana na ukimya wake. Ndio maana leo hii watu wengi hawapendi kuwa kimya, maana wataingia nadani zaidi ya uwepo wa Mungu, watasikia sauti ya Mungu ikiwaagiza waache vitu fulani na kutenda impendezavyo Mungu, nao hawataki kuacha wanvyoambiwa wache, hivyo wanaamua kuwa watu wa kelele, ili wasisikie maagizo ya Mungu.

Maria:
Anamwamini Yosefu kuliko hata malaika. Malaika alipoongea naye, alimuuliza, “Itakuwaje jambo hili na mimi simjui mume?” Mpaka alipoelezwa ndipo alipokubali. Lakini hatuoni popote Maaria anapomuuliza Yosefu itakuwaje huko tuendako, tunaona anakwenda na Yosefu kule ambako Yosefu anampeleka. Wanandoa mnatakiwa lenu liwe moja. Umuamini mwenzio. Nawe baba uwe mlinzi wa familia yako.

Leo katika ndoa zetu, tunaaminiana hivyo? Letu ni moja kama wanandoa? Leo wewe Yosefu unailinda familia yako? Mnakuwa na muda wa kuwa pamoja kama wanafamilia?

Watoto wengi siku hizi wanalelewa na televisheni. Baba na mama hawapo nyumbani wanatafuta pesa. Yale waliyotakiwa wafundishwe na wazazi sasa wanafundishwa na programu za televisheni. Leo hii unaambiwa kuna kazi mbili uchague moja, utachagua ipi? Ya kwanza unapata mshahara mnono sana, ila unapata asilimia tano tu ya muda wa kukaa na familia yako; ya pili, unapata muda wa asilimia hamsini wa kukaa na familia yako, ila mshahara sio mnono sana, ni kama laki chahce hivi, utachagua kazi ipi?
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, baada ya timu yake kuchukua kombe la dunia, timu nyingi zilimuita zikiwa tayari kumlipa pesa nyingi sana, lakini yeye alikataa, akasema kuwa kwa miaka miwili aliyoiandaa timu kwa kombe la dunia, hakupata kabisa muda wa kuwa na familia yake. Alichotaka ilikuwa nchi yake ipate kombe la dunia, na hili alikuwa ameshalifanikisha, hivyo ulikuwa ni wakati wa yeye kwenda kukaa na familia yake. Kwa hiyo alikataa ofa zote. Je wewe leo ungechagua nini? Pesa au familia?

Tunapoadhimisha sherehe ya familia takatifu, tumuombe Mungu leo atubadilishe, familia zetu ziige mfano wa familia takatifu. Hivyo basi tukae kimya kwa dakika moja tukitafakari hali ilivyo katika familia zetu.








All the contents on this site are copyrighted ©.