Yaliyojiri nchini Tanzania kwa Mwaka 2013, JK, "achonga na watanzania"
Salam za Mwaka Mpya kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, tarehe 31 Desemba
2014. Rais Kikwete katika salam zake kwa Mwaka Mpya amekazia pamoja na mambo mengine:
hali ya usalama, uhalifu, biashara haramu ya dawaza kulevya, ujambazi na ujangiri
na madhara yake; mchakato wa kuunda Katiba; hali ya uchumi; mazingira ya uwekezaji;
elimu, maji na afya; magonjwa ya moyo, saratani, figo na mafunzo: Nyumba, ujenzi wa
miundo mbinu, nishati: Ushirikiano wa Kanda; Jumuiya ya Afrika Mashariki na Medani
za Kimataifa; Miaka 50 ya Mapinduzi na Muungano. Utangulizi Ndugu zangu; Watanzania
Wenzangu; Niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa
rehema, kwa kutujalia uzima mpaka kufika na kuiona siku hii ya leo ya kuuaga mwaka
2013 na kuukaribisha mwaka 2014. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao hawakupata
bahati tuliyoipata sisi kwa vile wametangulia mbele ya haki. Tuendelee kumwomba Mola
wetu awape mapumziko mema na azilaze roho zao mahali pema peponi. Ameen.
Hali
ya Usalama Ndugu Wananchi; Tunaumaliza mwaka 2013 nchi yetu ikiwa salama
na tulivu. Mipaka iko salama na ile hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo kwa nyakati fulani
mwaka huu sasa haipo tena. Uhusiano wetu na majirani ni mzuri na tutaendelea kufanya
kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hali inaendelea kuwa hivyo au hata kuwa bora zaidi
mwaka 2014 na daima dumu. Hali ya usalama wa ndani ya nchi nayo ni nzuri. Hali
ya wasiwasi tuliyokuwa nayo mwaka wa jana na mwanzoni mwa mwaka huu kuhusu uhusiano
baina ya Wakristo na Waislamu haipo. Ni matumaini yangu kuwa haitajirudia tena. Pepo
mbaya amepita tuombe atokomee kabisa. Ndugu zangu; Watanzania wenzangu;
Napenda kurudia kuwasihi kuwa tuchague kuendelea kuishi pamoja kwa upendo, umoja,
kuvumiliana na kushirikiana. Tuepuke kugeuza tofauti zetu za kisiasa, kidini, rangi,
kabila au maeneo tutokayo kuwa chanzo cha uadui na mifarakano. Kwa sasa tuna mwelekeo
mzuri nawaomba tuudumishe. “Mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”.
Tuchague kuijenga nchi yetu badala ya kuibomoa. Tusiwasikilize watu hasidi wanaochochea
uadui na mifarakano miongoni mwetu. Watatuvurugia nchi yetu nzuri.
Uhalifu Ndugu
Wananchi; Katika mwaka 2013 vyombo vya dola vikishirikiana na wananchi viliendelea
kupambana na vitendo vya uhalifu. Mafanikio ya kutia moyo yameendelea kupatikana
ingawaje bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kufanya mwaka 2014 na miaka ijayo.
Dawa
za Kulevya Ndugu Wananchi; Kati ya Januari na Desemba 2013, kilo 1,261 za
heroin, kilo 3 za cocaine na kilo 89,293 za bangi zimekamatwa na watuhumiwa 1,631
wametiwa mbaroni. Tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na mapambano
yanazidi kuwa makali. Mafanikio yanaendelea kupatikana ingawaje bado tuna kazi kubwa
na ngumu ya kufanya mbele yetu. Ni makusudio yetu kuongeza maradufu nguvu ya kupambana
dhidi ya uhalifu huu. Tupo hatua nzuri katika matayarisho ya kuanzisha Kikosi
Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika mwaka wa fedha 2014/15. Pia tutaitazama
upya sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya dawa za kulevya ili kuifanya
iwe na meno makali zaidi. Vilevile, tutaongeza uwekezaji katika vituo vya tiba na
kuwarekebisha watu wanaotumia dawa za kulevya. Mafanikio yanayopatikana Muhimbili
na Mwananyamala yanatupa moyo wa kufanya zaidi.
Ujambazi Ndugu wananchi;
Jeshi la Polisi limeendelea kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio yameendelea
kupatikana. Matukio ya ujambazi yemepungua mwaka 2013 ukilinganisha na mwaka 2012.
Takwimu zifuatazo zinathibitisha ukweli huo. Mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa
yalikuwa 6,872 na kwa mwaka 2013 yameripotiwa matukio 6,409. Mwezi Julai mwaka huu,
niliamua kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika kupambana na ujambazi
wa kutumia silaha na utekaji wa magari katika Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma. Katika
Mikoa hiyo tatizo la ujambazi lilikuwa limefikia kiasi cha kulazimisha watu kusindikizwa
na Polisi kutoka Ngara kwenda Karagwe, Biharamulo kwenda Muleba na kutoka Nyakanazi
hadi Kakonko. Hali hii haikubaliki na hatuwezi kuiacha iendelee. Ndugu Wananchi; Uamuzi
wangu huo ndiyo ulioanzisha Operesheni Kimbunga ambayo imekuwa na mafanikio ya kutia
moyo. Hali ya usalama katika Mikoa hiyo inaelekea kuimarika ingawaje ni mapema mno
kusema tatizo limedhibitiwa. Silaha nyepesi na nzito zipatazo 650 zikiwemo za kijeshi
na za kiraia pamoja na mabomu ya kutupwa kwa mkono 11 zilikamatwa kwenye operesheni
hiyo. Aidha, watu 31,203 waliokuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria walirudi makwao.
Kati yao, watu 21,758 walirudi kwa hiari na 9,445 walirudishwa wakati wa Operesheni.
Ndugu Wananchi; Nimepata minong’ono kuwa baadhi ya watu walioondoka
wanarudi kinyemela. Napenda kuwatahadharisha kuwa wasifanye hivyo. Wanajisumbua bure.
Hawatadumu. Ushauri wangu kwao ni kuwa kama wanapenda kuishi Tanzania wafuate njia
halali za kufanya hivyo.
Ujangili wa Wanyamapori Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tuliongeza nguvu katika kupambana na ujangili wa wanyamapori na uvunaji
haramu wa rasilimali za misitu. Hili ni tatizo la siku nyingi lakini katika miaka
ya hivi karibuni limekuwa kubwa mno na kuwazidi nguvu Askari wa Wanyamapori na Maafisa
Misitu. Kwa nia ya kuwaongezea nguvu, mwaka 2010 niliagiza Jeshi la Polisi lisaidie
Idara ya Wanyamapori na Idara ya Misitu katika kupambana na uhalifu huo. Operesheni
kadhaa ziliendeshwa maeneo mbalimbali nchini na mafanikio ya kutia moyo yalipatikana.
Lakini, kwa kutambua ukubwa wa tatizo na hasa kwa upande wa aina ya silaha na mbinu
zinazotumiwa na majangili niliamua kuhusisha vyombo vingine vya usalama likiwemo Jeshi
la Ulinzi. Nia ni kuongeza nguvu ya mapambano. Ndipo ilipoanzishwa “OPERESHENI TOKOMEZA”.
Ndugu Wananchi; Kazi nzuri imefanyika chini ya Operesheni hiyo. Mafanikio
ya kuleta matumaini yameweza kupatikana. Mitandao ya ujangili imeweza kutambulika
na wahusika wake kadhaa wametiwa nguvuni. Mitandao hiyo inahusisha watu wa aina mbalimbali.
Wamo raia wa kawaida, wapo watu maarufu, wapo watumishi wa idara mbalimbali za Serikali
wakiwamo wa Idara za Wanyamapori na Misitu. Watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha
za kijeshi 18, za kiraia 1,579 na shehena kubwa za meno ya ndovu na nyara nyingine
navyo vilikamatwa.Watu kadhaa tayari wameshafikishwa mahakamani. Ndugu Wananchi; Wahenga
wamesema “kwenye wengi pana mengi”. Katika utekelezaji wa Operesheni hii kumekuwepo
na taarifa za kufanyika makosa kinyume na malengo na madhumuni ya Operesheni. Niliagiza
baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza, zoezi lisitishwe kwa muda ili uchunguzi ufanyike,
kasoro zitambuliwe na waliofanya makosa wachukuliwe hatua zipasazo. Wakati kazi hiyo
inafanyika suala hilo lilijadiliwa Bungeni na Kamati Teule kuundwa. Matokeo yake
sote tunayajua. Mawaziri wanne wamewajibika kisiasa.
Ndugu Wananchi; Napenda
kutumia nafasi hii kuwapa pole Mawaziri wetu hao kwa matatizo yaliyowakuta. Nawapongeza
kwa uamuzi wa kukubali kuwajibika kwa makosa yaliyofanywa na maofisa wa chini yao.
Wameonesha ukomavu wa kisiasa na kiuongozi wa hali ya juu na moyo wa uzalendo.
Kama
mlivyosikia nitaunda Kamisheni ya Uchunguzi itakayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu.
Uchunguzi wa kina utafanywa kuhusu kadhia yote hiyo. Makosa yaliyofanyika yataainishwa
na waliofanya kutambuliwa ili wachukuliwe hatua zipasazo kwa mujibu wa sheria na kwa
mujibu wa kanuni za utumishi wa umma. Ndugu Wananchi; Ni muhimu kufanya hivi
ili haki itendeke ipasavyo. Mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa umma kubebwa
na viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja, siyo sahihi.
Lazima kila mtu abebe mzigo wake inavyostahili. Ni matumaini yangu pia kwamba katika
siku za usoni kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale hasa
waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe. Uwajibikaji wa wana-siasa peke yao hautoshi,
kwani huwaacha waharibifu waendelee na kazi isivyostahili. Mtindo huu utawafanya
watumishi wasione umuhimu wa kutokurudia makosa. Hata hivyo, pale kwenye ushahidi
wa wazi kwamba kiongozi wa kisiasa angeweza kuchukua hatua za kuzuia madhara lakini
hakufanya hivyo lazima kiongozi huyo awajibike.
Ndugu Wananchi; Tunakamilisha
matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza. Ni muhimu kuendelea nayo
kwani tusipofanya hivyo majangili wataendelea na vitendo vyao viovu. Hali ni mbaya
sana kwa upande wa uwindaji wa ndovu. Nilipolihutubia Bunge tarehe 7 Novemba, 2013,
nilieleza kuwa tutafanya sensa ya ndovu katika Pori la Hifadhi la Selous. Sensa hiyo
imekamilika lakini taarifa yake inatisha. Kuna ndovu 13,084 tu wakati mwaka 1976
walikuwa 109,419. Tusipoendelea na Operesheni hii baada ya miaka michache ijayo hakutakuwa
na ndovu hata mmoja. Halikadhalika, zoezi la kuondoa mifugo katika mapori ya hifadhi
ya taifa litaendelea. Katika awamu ya pili ya Operesheni hii, washiriki watasisitizwa
kutokutenda maovu yaliyofanyika katika awamu ya kwanza.
Mchakato wa Kuunda
Katiba Ndugu wananchi; Tumefika mahala pazuri katika mchakato
wetu wa kutayarisha Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jana Mwenyekiti
wa Tume, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, alitukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba, mimi
na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein. Kama nilivyosema jana kinachofuata
sasa ni kuitangaza Rasimu hiyo katika Gazeti la Serikali kwa kila mtu na hasa Wajumbe
wa Bunge la Katiba, kuiona na kuisoma. Baada ya hapo kitafuata kitendo cha kuifikisha
Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupatikana
Rasimu ya Mwisho itakayofikishwa kwa wananchi kupigiwa kura. Ndugu Wananchi; Mchakato
wa kupata Wajumbe 201 watakaoungana na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
kuunda Bunge Maalum la Katiba umeanza. Ni matarajio yetu kuwa katika wiki ya tatu
ya Januari, 2014, uteuzi utakamilika. Siku 21 baada ya hapo Bunge la Katiba litaanza.
Hii ni kwa nia ya kuwapa nafasi Wajumbe hao kusoma Rasimu ya Katiba. Baada ya Bunge
la Katiba kumaliza kazi yake, utaanza mchakato wa Kura ya Maoni itakayopigwa na wananchi
ndani ya siku 74 baada ya Rasimu ya Katiba kupitishwa na Bunge Maalum na kukabidhiwa
kwa Rais. Iwapo Rasimu itakubaliwa na wananchi hapo tutakuwa tumepata Katiba Mpya.
Lakini, iwapo Rasimu itakataliwa ina maana kuwa Katiba ya sasa itaendelea kutumika
mpaka hapo mchakato mwingine utakapoanzishwa na Katiba mpya kupatikana. Ni matumaini
yangu na, ni maombi yangu na rai yangu kuwa Rasimu hiyo itakubalika ili nchi yetu
isonge mbele.
Pongezi Ndugu Wananchi; Niruhusuni nitoe pongezi
zangu za dhati kwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Tume kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya.
Najua haikuwa kazi rahisi hata kidogo lakini wameweza. Kwa namna ya pekee nawashukuru
wananchi kwa ushiriki wao mzuri uliowezesha zoezi la mabadiliko ya Katiba kufikia
hatua tuliyofikia sasa. Ndugu Wananchi; Ni matumaini yangu na ndiyo matumaini
ya Watanzania wote kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wataijadili Rasimu ya Katiba
kwa makini na kufanya kila wawezalo kuiwezesha nchi yetu kupata Katiba nzuri itakayoimarisha
na kudumisha Muungano wetu. Katiba itakayoendeleza umoja, upendo, udugu, mshikamano
na ushirikiano miongoni mwa wananchi wa Tanzania. Katiba itakayoihakikishia nchi yetu
amani, utulivu na ustawi wa kiuchumi na kijamii. Ni imani yangu na ya Watanzania
wote kuwa Wajumbe wa Bunge la Katiba wataweka mbele maslahi mapana ya taifa na watu
wake. Wasiweke mbele maslahi yao binafsi au ya vikundi vyao vya kisiasa au kijamii.
Wakifanya vinginevyo kuna hatari ya kupata Katiba isiyokidhi haja na itakuwa hasara
kubwa kwa taifa letu na kwao pia.
Uchumi Ndugu wananchi;
Katika mwaka tunaoumaliza leo, Tanzania iliendelea kupata mafanikio katika nyanja
mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Jambo la kufurahisha ni kuwa mafanikio
hayo yamepatikana licha ya kuwepo changamoto kadhaa hapa nchini na hali ya uchumi
wa dunia kuwa bado haijatengemaa vya kutosha. Pato la taifa limekua kwa asilimia
7.1 ukilinganisha na asilimia 6.9 mwaka jana. Tunategemea kuwa mwaka 2014 pato la
taifa litakua kwa asilimia 7.3. Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 12.1, Desemba,
2012 hadi asilimia 6.2, Novemba 2013. Lengo letu ni kufikia asilimia 5 mwezi Juni,
2014. Ndugu Wananchi; Hadi Novemba, 2013, Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa
na huduma zenye thamani ya dola za Marekani milioni 7,720.8 ukilinganisha na dola
milioni 7,916.6 za mwaka ulioishia Novemba 30, 2012. Kushuka kwa bei za kahawa, pamba,
katani, chai, karafuu na dhahabu ndiko kulisababisha kupungua kwa mapato yetu ya fedha
za kigeni. Hali hii inatukumbusha umuhimu na uharaka wa kuendeleza viwanda vya kuongeza
thamani mazao na bidhaa zetu tunazouza nje. Jambo hili tutalipa msukumo maalum mwaka
2014 na kuendelea. Pamoja na kushuka kidogo kwa mapato ya mauzo yetu ya nje akiba
yetu ya fedha za kigeni iliendelea kuwa nzuri. Hadi Novemba 30, 2013 akiba yetu ilikuwa
dola za Marekani 4,538 milioni. Hata hivyo, akiba hiyo inatuwezesha kuagiza bidhaa
toka nje wa miezi 4.4 ni chini ya lengo letu la miezi 4.5. Sina wasiwasi kuwa mwaka
2014 tutaliziba pengo hilo. Ndugu Wananachi; Sekta zilizochangia sana katika
kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2013 ni pamoja na mawasiliano asilimia 20.6, huduma
ya fedha asilimia 13.2, uzalishaji viwandani asilimia 8.2, madini asilimia 7.8, ujenzi
asilimia 7.8, biashara asilimia 7.7 na uchukuzi asilimia 7.1. Bado kasi ya ukuaji
wa sekta ya kilimo ilikuwa ndogo kwani ilikuwa asilimia 4.3. Pamoja na hayo,
kilimo kinaendelea kutoa mchango mkubwa kwa ustawi wa uchumi wa Tanzania na watu wake.
Kilimo kinachangia asilimia 24.7 ya pato la taifa na asilimia 10.7 ya mapato ya fedha
za kigeni. Kilimo kimeiwezesha nchi yetu kujitosheleza kwa chakula na kuvipatia viwanda
malighafi. Kwa upande wa mazao ya chakula, kwa mfano, mwaka huu uzalishaji ulikuwa
tani 14,383,845. Ukilinganisha na mahitaji yetu ya chakula ya tani 12,149,120 hivyo
tunajitosheleza na kuwa na ziada kidogo. Ziada hii ni kidogo mno hivyo inatulazimu
mwaka ujao tuongeze maradufu juhudi na uwekezaji katika kutekeleza shabaha na malengo
ya kilimo. Ndugu Wananchi; Kwa ajili ya uzalishaji wa chakula kuwa mzuri, mwaka
huu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula wameweza kununua tani 233,689.8 za nafaka
hadi kufikia Desemba 27, 2013 kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa miaka ya nyuma. Mwaka
2012 wakati kama huu Wakala ilikuwa na kiasi cha tani 93,047.8 tu na kutulazimisha
kutafuta chakula nje ya nchi. Kwa ajili hiyo tulilazimika kuruhusu wafanyabiashara
kuagiza mahindi, mchele na sukari kutoka nje kwa nafuu ya kodi. Uamuzi huo umesaidia
nchi kuwa na chakula cha kutosha na kuuzwa kwa bei nafuu kwa walaji.
Ndugu
Wananchi; Ni matarajio yangu, na ndiyo hasa dhamira yetu, kwamba mwaka
2014 tutapata mafanikio makubwa zaidi kwa upande wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Naamini tutaweza kwa vile tumejipanga vizuri. Tunayo miradi ya kimkakati iliyoainishwa
vizuri katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na chini ya Utaratibu wa Matokeo
Makubwa Sasa. Miradi hiyo kama itatekelezwa kama ilivyopangwa uchumi utakua kwa kasi
kubwa zaidi, ajira nyingi zitapatikana na huduma za kiuchumi na kijamii zitaboreka
sana. Bahati nzuri tumeweka utaratibu mpya na mzuri wa kufuatilia utekelezaji
wa mipango, miradi na shughuli za Serikali. Katika Ofisi ya Rais kumeanzishwa Ofisi
maalum ya ufuatiliaji ijulikanayo kama Presidential Delivery Bureau. Na, kila Wizara
ina kitengo cha namna hiyo kijulikanacho kama Ministerial Delivery Unit. Kwa ajili
hiyo utekelezaji wa miradi ya kimkakati na shughuli za Serikali utakuwa mzuri zaidi.
Mazingira
ya Uwekezaji Ndugu Wananchi; Ni makusudio yetu kuwa kuanzia sasa tutaihusisha
sekta binafsi kwa nguvu zaidi katika utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo.
Nimeagiza Presidential Delivery Bureau ishughulikie suala la uboreshaji wa mazingira
ya uwekezaji nchini. Sifa ya nchi yetu kuhusu mazingira ya uwekezaji siyo nzuri.
Kwa mujibu wa tathmini inayofanywa kila mwaka na Benki ya Dunia, mwaka 2007 nchi yetu
ilikuwa kati ya nchi 10 bora duniani kwa kufanya mageuzi makubwa ya kupunguza gharama
za kufanya biashara. Mwaka huo tulikuwa nchi ya 142 kati ya nchi 175. Mwaka 2008
tukapanda na kuwa wa 130 kati ya nchi 176, mwaka 2012 tulikuwa wa 134 kati ya nchi
185 na sasa ni wa 145 kati ya nchi 185. Hali hii si nzuri hata kidogo kwa uchumi
unaokusudiwa kujengwa kwa kutegemea uwekezaji wa sekta binafsi. Tunategemea PDB itatupa
ushauri mzuri wa nini kifanyike kurekebisha mambo. Ndugu Wananchi; Utekelezaji
wa miradi ya Big Result Now (BRN) katika kilimo, umeme, reli, barabara, bandari, maji,
elimu na kuongeza mapato ya Serikali umeanza kwa kasi inayoleta matumaini. Kama upande
wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali utakwenda inavyotarajiwa tutegemee mambo mengi
mazuri kufanyika kuanzia mwaka 2014 mpaka 2016. Mpaka sasa hali ya ukusanyaji
wa mapato ya Serikali si mbaya. Wastani kwa mwezi unakaribia shilingi bilioni 700
kuelekea shilingi bilioni 800. Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa miezi ya Julai
hadi Novemba yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,008.1 kipindi kama hicho mwaka
2012 hadi shilingi bilioni 3,555.5 mwaka 2013. Hata hivyo makusanyo ya Julai hadi
Novemba, 2013 ni asilimia 88.1 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 4,036.8. Lengo
halijafikiwa kwa sababu ya kuchelewa kutekelezwa kwa baadhi ya marekebisho ya mfumo
wa kodi, hususan tozo ya simcard, kodi za mishahara kutokana na kutokupandishwa kwa
kima cha chini katika sekta binafsi na ya uhawilisho wa fedha (money transfer). Pia
kuendelea kwa mvutano baina ya TRA na wafanyabiashara kuhusu bei za mashine za kodi.
Ni matumaini yangu matatizo hayo yatashughulikiwa na kumalizwa mapema iwezekanavyo
ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali
mwaka 2014.
Elimu Ndugu Wananchi; Kwa upande wa elimu tumeendelea
kupata mafanikio katika kupunguza tatizo la upungufu wa walimu wa shule za msingi
na sekondari. Mwaka huu tuliajiri walimu 28,666. Kwa ajili hiyo upungufu wa walimu
ni 57,755 kati yao 20,625 wa shule za msingi na 37,130 wa shule za Sekondari. Mapema
mwaka ujao tutaajiri walimu wapya 36,100 kati yao 18,100 wa shule za msingi na 18,000
wa sekondari. Kufanya hivyo kutafanya pengo lililopo liwe dogo zaidi.
Kwa
upande wa shule za sekondari, tatizo la walimu wa masomo ya sanaa tunakaribia kulimaliza.
Changamoto yetu kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya sayansi. Upungufu ni walimu
26,998 na uwezo wa vyuo vyetu ni kutoa walimu wa sayansi 2,300 kwa mwaka. Mapema
mwaka 2014 tutakutana na wadau wa elimu nchini kujadiliana juu ya mkakati wa haraka
wa kulikabili tatizo hili. Nilipanga tufanye hivyo mwaka huu lakini mambo yaliingiliana
sana hatukuweza. Ndugu Wananchi, Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu
na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Tuliongeza fedha katika bajeti ya elimu kwa
ajili ya vitabu. Hivi sasa usambazaji wa vitabu vyenye thamani ya shilingi bilioni
76 za bajeti ya mwaka 2012/13 unaendelea. Kwa sababu hiyo hivi sasa upungufu wa vitabu
umeshuka na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi 3. Naamini shilingi bilioni 49 zilizotengwa
katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya vitabu itafanya mambo kuwa nafuu
zaidi. Tukiendelea kuwekeza kama tufanyavyo sasa shabaha yetu ya kila mwanafunzi wa
msingi na sekondari kuwa na kitabu chake kwa masomo yote ifikapo 2016 itatimia. Ndugu
Wananchi; Mwaka huu tumeanza utekelezaji wa mpango mkubwa wa kujenga nyumba za
walimu. Kwa kuanzia tumetenga shilingi milioni 500 kwa kila Halmashauri. Tumeanza
na Halmashauri 40, mwaka ujao na miaka inayofuata tutaongeza fedha zinazotengwa na
kuzifikia Halmashauri zote. Kwa upande wa ujenzi wa maabara katika sekondari za kata
napenda kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya
na Miji, kuwa kila mmoja ahakikishe kuwa ifikapo Novemba, 2014 malengo yanatimia.
Wasisubiri kuulizwa.
Maji Ndugu Wananchi; Kwa kutambua umuhimu
wa maji kwa maisha ya wanadamu na uchumi katika bajeti ya mwaka huu wa fedha sekta
ya maji imepewa upendeleo katika mgao wa fedha. Tutaendelea kuongeza fedha katika
bajeti mbili zinazofuata ili watu wengi zaidi mijini na vijijini wapate maji safi
na salama. Kama fedha zitapatikana kama ilivyopangwa na utekelezaji ukasimamiwa vizuri
tunatarajia kuwa katika mwaka 2013/14 watu milioni 7.1 watapata maji. Katika mwaka
ujao wa fedha 2014/15 tumepanga kuwapatia maji watu wengine milioni 7 na mwaka utaofuata
(2015/16) tutaongeza tena huduma hiyo kwa watu milioni 1.3 na kufanya tufikie asilimia
74 ya Watanzania wanaopata maji safi na salama ifikapo 2015/2016.
Afya Ndugu
wananchi; Tumeendelea kupata mafanikio katika kuendeleza upatikanaji
wa huduma ya afya kwa wananchi wa Tanzania. Zahanati, vituo vya afya na hospitali
zimeendelea kujengwa kote nchini. Aidha, hospitali za wilaya, mikoa, kanda na Hospitali
ya Taifa Muhimbili zimeendelea kuboreshwa. Kwa ajili hiyo idadi ya Watanzania wanaoweza
kupata huduma ya afya iliyo bora inazidi kuongezeka. Hali kadhalika, wataalamu wa
afya wa fani mbalimbali wameongezeka na hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba
imezidi kuboreshwa. Pamoja na yote hayo bado kuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu.
Kufanya hayo ndiyo dhamira yetu kuu kwa mwaka 2014. Ndugu wananchi; Tumeendelea
kupata ushindi katika mapambano dhidi ya magonjwa yanayoua watu wengi nchini. Kwa
upande wa malaria, kwa mfano, maambukizi ya ugonjwa huo kwa watoto na mama wajawazito
yamepungua kutoka asilimia 18 hadi 9.5. Tutaendelea kugawa vyandarua kwa wajawazito
na watoto kwa kutumia hati punguzo pamoja na kusisitiza matumizi ya dawa mseto na
kupulizia dawa ya kuua mbu majumbani. Aidha, tunatarajia kupata mafanikio zaidi
miaka ijayo kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluilui vya mbu wanaoeneza malaria
kitapoanza kazi. Ndugu Wananchi; Mambukizi ya UKIMWI yameshuka hadi asilimia
5.1. Inaleta faraja kuona watu wengi wamejitokeza kupima afya zao kwa hiari. Mpaka
sasa watu milioni 18 wamepima. Tunao watu 1,298,402 walioorodheshwa kwa ajili ya kupata
huduma ya tiba na kati yao 485,715 wanapata dawa. Waliosalia watapata wakati wao
ukifika.
Mpaka sasa vituo 4,603 vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi
ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto vimeanzishwa nchini kote tangu mpango huo
uzinduliwe tarehe 1 Desemba, 2012. Idadi yake inaendelea kuongezeka. Ni dhamira yetu
kuendeleza jitihada za kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa Watanzania.
Mafanikio ya kampeni hii pamoja na ile dhidi ya malaria ndiyo chachu ya mafanikio
tuliyopata katika kupunguza vifo vya watoto nchini na kufikia lengo la Milenia mwaka
huu.
Magonjwa ya Moyo Ndugu Wananchi; Katika mwaka
2013 tunaoumaliza leo, tumeshuhudia mambo kadhaa mazuri yakifanyika yanayoelezea mafanikio
tunayoendelea kuyapata katika jitihada zetu za kujenga uwezo wa tiba kwa maradhi tunayopeleka
wagonjwa nje ya nchi. Niruhusuni niyataje baadhi yake. La kwanza, ni kuanza kazi
kwa Kituo cha Tiba na Mafunzo ya Magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Hiki ni kituo kikubwa na cha aina yake cha matibabu ya maradhi ya moyo hapa nchini.
Huduma za kisasa za uchunguzi na matibabu ya maradhi ya moyo ambazo zamani zilikuwa
zinapatikana nje ya nchi sasa zinaweza kupatikana hapa hapa nchini. Kwa kuwa na vitanda
100 vya kulaza wagonjwa, Watanzania wengi wataweza kuhudumiwa na maisha yao kuokolewa.
Ndugu Wananchi; Katika kituo hiki watu wanaweza kufanyiwa upasuaji mkubwa
wa moyo (open heart surgery), uwekaji wa mashine ya kuongezea nguvu kwenye moyo (pacemaker),
uwekaji wa vyuma vidogo katika mishipa ya damu ya moyo ambayo imebanana (stent).
Tangu kituo kianze kazi rasmi tarehe 30 Aprili, 2013 mpaka sasa watu 347 wamefanyiwa
upasuaji wa moyo na watu watatu wamewekewa pacemaker tangu huduma hiyo ianze Novemba,
2013. Mapema mwakani kituo kinatarajiwa kuanza huduma ya kuweka stent. Kituo
hiki ni kipya hivyo katika mwaka 2014 tutaendelea kukijengea uwezo wa vifaa tiba,
wataalamu na mahitaji mengine muhimu ili kulipunguzia taifa mzigo wa kupeleka wagonjwa
nchi za nje. Serikali, pia itaendeleza ushirikiano wake na uongozi wa Hospitali ya
Kanda ya Bugando kuboresha huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo katika hospitali hiyo.
Huduma hiyo ilizinduliwa tarehe 26 Oktoba, 2013 na Makamu wa Rais Mheshimiwa Daktari
Mohamed Ghalib Bilal.
Saratani Ndugu Wananchi; Kwa upande
wa maradhi ya saratani, Februari, 2013 jengo jipya la kulaza wagonjwa 170 lilifunguliwa
katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Kufunguliwa kwa jengo hilo kumeongeza uwezo
wa taasisi yetu hiyo kulaza wagonjwa 290 badala ya 120 tu kabla ya hapo. Ujenzi wa
jengo hili jipya umesaidia sana watu wengi zaidi kuhudumiwa na kupunguza msongamano
mkubwa wa wagonjwa uliokuwepo.
Figo Ndugu Wananchi; Kuhusu maradhi
ya figo mwaka huu pia tumeshuhudia huduma ya usafishaji wa figo zenye matatizo ikipanuliwa.
Huduma hiyo imeanzishwa tena katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya na imeanzishwa kwa
mara ya kwanza katika Chuo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Pale Mbeya tayari
wagonjwa 93 wamehudumiwa mwaka huu na kuwapa matumaini mapya ya maisha yao. Kwa pale
Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa kituo kikubwa kitakachobobea kwa magonjwa ya figo
unaendelea na unategemewa kukamilika mapema mwaka 2014.
Mafunzo Ndugu
Wananchi; Katika mwaka 2013 tumefungua ukurasa mpya katika jitihada zetu za kuongeza
wataalamu wa afya nchini. Chuo cha Sayansi ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma kimefanya
mahafali yake ya kwanza ambapo wanafunzi 50 wa Shahada ya Uuguzi walihitimu. Tunatarajia
kuanza kupata madaktari kuanzia mwaka 2014. Kwa upande wa mchakato wa kujenga
makazi mapya ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kule Mloganzila
mchakato umeanza. Ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na umeme unaendelea hivi
sasa. Mwaka 2014 ujenzi wa Hospitali ya kisasa ya kufundishia yenye vitanda 650 utaanza.
Ujenzi wa Mlonganzila ukikamilika Chuo Kikuu cha Muhimbili kitaweza kuchukua wanafunzi
15,000 wa fani zote ukilinganisha na 3,060 wa sasa. Hatua hiyo itaongeza sana uwezo
na kasi yetu ya kupunguza uhaba wa Madaktari, Wauguzi na wataalam wengine wa afya.
Nyumba Ndugu Wananchi; Katika mwaka 2013 ujenzi wa nyumba 35
za kuishi watumishi wa afya katika mikoa ya Mtwara (5), Rukwa (20) na Singida (10)
umekamilika. Ujenzi wa nyumba 100 unaendelea. Nyumba hizo ni sehemu ya mpango wa
ujenzi wa nyumba 580 zinazojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Global Fund
kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza zinajengwa nyumba 310 ambapo taasisi ya Benjamin
William Mkapa Foundation ndiyo mtekelezaji wa ujenzi huo. Napenda kutumia nafasi
hii kutoa shukrani za dhati kwa Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin Mkapa kwa mchango
wake mkubwa alioutoa na anaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Ujenzi wa Miundombinu Ndugu wananchi; Katika mwaka
2013, tumeendelea kupata mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri
wa ardhini, majini na angani. Kasi ya ujenzi wa barabara imeendelea kufanyika kote
nchini. Kazi ya ujenzi ingekuwa nzuri zaidi kama mtiririko wa malipo kwa Wakandarasi
ungekuwa mzuri. Tatizo hili tutalitafutia ufumbuzi mwaka 2014 ili kasi ya ujenzi
wa barabara za lami nchini iwe nzuri zaidi. Pamoja na hayo mwaka huu kilomita
877 za barabara zimekamilika. Ujenzi wa daraja la Malagarasi nao umekamilika kinachosubiriwa
ni sherehe za uzinduzi. Ujenzi wa daraja la Kilombero umeanza na ule wa daraja la
Kigamboni unaendelea vizuri. Tunatarajia kuwa mwakani tutaongeza zaidi kasi ya ujenzi
wa barabara zilizosalia ikiwa ni pamoja na kujenga baadhi ya barabara kwa ubia na
sekta binafsi. Kwa kasi na mwenendo tunaoendelea nao sasa naamini ifikapo mwaka 2015
tutakuwa tumefikia hatua ya juu sana katika shabaha yetu ya kuunganisha mikoa yote
nchini kwa barabara za lami.
Ndugu Wananchi; Jitihada za kupunguza
msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam zimeendelea kutekelezwa. Barabara
kadhaa zilipanuliwa na kazi inaendelea. Ujenzi wa njia ya kupita mabasi yaendayo
haraka umeendelea kwa kasi ya kuridhisha. Mchakato wa ujenzi wa barabara za juu ya
nyingine katika njia panda za TAZARA na Ubungo umeshaanza. Mwaka ujao huduma ya usafiri
wa treni kusafirisha abiria Dar es Salaam itaongezwa ili watu wengi zaidi wanufaike.
Ndugu wananchi; Mwaka huu, kwa upande wa reli ya kati, kazi ya kuboresha
njia ya reli imeendelea kufanyika na itaendelea mwaka 2014. Mwakani (2014) Shirika
la Reli litapokea injini mpya 13, mabehewa ya mizigo 274 na breki 34 hivyo kuboresha
sana huduma katika reli ya kati. Kuhusu ujenzi wa reli mpya ya upana wa kimataifa
ni matarajio yetu kuwa kama kila kitu kitaenda sawa mchakato wa ujenzi utaanza katika
nusu ya pili ya mwaka 2014. Ndugu Wananchi; Tumetoa kipaumbele cha juu katika
kuboresha huduma ya usafiri wa anga nchini. Mwaka huu, tumeendelea na ukarabati,
upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mikoa ya Kilimanjaro, Kigoma, Tabora, Mwanza,
Arusha, Mtwara na Kagera. Ni jambo la kufurahisha kuona Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Songwe ukianza kutumika. Hatimaye ndoto imetimia. Mwaka wa 2014 ujenzi wa majengo
mengine ya kuhudumia abiria, mizigo na ndege utaendelea katika uwanja huo. Pia
ni furaha iliyoje kwamba upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na ujenzi wa gati la
Kilindoni vimekamilika. Kero ya miaka mingi imepatiwa ufumbuzi. Kazi ya ujenzi wa
jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere itaanza
rasmi mwaka 2014.
Nishati Ndugu wananchi; Dhamira
yetu ya kutaka Tanzania iwe na umeme wa uhakika na unaonufaisha watu wengi imepata
sura na mwelekeo mzuri mwaka huu 2013. Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo
kuja Dar es Salaam umeanza na utekelezaji unakwenda vizuri. Kama ujenzi wa bomba
utakamilika kama inavyotarajiwa na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme Kinyerezi
utaenda kama ilivyopangwa, ifikapo mwaka 2015 Tanzania itafikia lengo la kuzalisha
megawati 3,000 za umeme. Ndugu Wananchi; Bahati nzuri mwaka huu, kufuatia kuongezewa
fedha za bajeti, kasi ya usambazaji umeme imekuwa nzuri. Tunaumaliza mwaka huku idadi
ya Watanzania waliounganishiwa umeme ikiwa imefikia asilimia 24 ukilinganisha na asilimia
21 mwaka 2012 na asilimia 10 mwaka 2005. Haya si mafanikio madogo. Kwa mwelekeo huu,
kufikia lengo la asilimia 30 ya Watanzania kupata umeme mwaka 2015 ni jambo la uhakika
kabisa sasa. Tena kuna uwezekano mkubwa wa kulivuka lengo hilo.
Ushirikiano
wa Kanda Watanzania Wenzangu; Katika mwaka 2013, nchi yetu imeendelea
kushiriki vizuri katika shughuli za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo sisi ni wanachama. Mwezi wa Agosti,
2013 tulikabidhi Uenyekiti wa chombo cha SADC kinachoshughulikia Siasa, Ulinzi na
Usalama kwa Namibia. Tulikuwa tumemaliza kipindi chetu cha mwaka mmoja. Katika
kipindi chetu cha uongozi tulishiriki kwa ukamilifu kutafuta suluhu kwa mizozo na
migogoro ya kisiasa na kiusalama nchini Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
na Madagascar. Tunafurahi kuona kwamba mambo katika nchi zote hizo sasa yanakwenda
vizuri. Nchini Zimbabwe utulivu umerejea baada ya kufanyika kwa uchaguzi mwezi Julai,
2013. Nchi ya Madagascar nayo imemaliza duru ya pili ya uchaguzi wa Rais kwa usalama.
Matokeo yanatarajiwa kutangazwa tarehe 7 Januari, 2014. Ni matumaini yetu kuwa watu
wa nchi hiyo watayapokea matokeo hayo na wataelekeza nguvu zao katika kujenga umoja
na maridhiano ili wajenge upya uchumi wa nchi yao. Kwa upande wa Mashariki ya
Kongo, tishio kubwa la usalama kutokana na vitendo vya kundi la waasi la M23 limezimwa
na Jeshi la Kongo kwa kushirikiana na Jeshi la Umoja wa Mataifa. Kama mjuavyo Tanzania
ni moja ya nchi zinazochangia maafisa na askari wa Jeshi hilo.
Ndugu Wananchi; Napenda
kutumia nafasi hii, kwa mara nyingine tena kutoa pongezi zangu za dhati kwa wanajeshi
wetu kwa kazi yao nzuri na iliyotukuka waliyoifanya huko Mashariki ya Kongo. Pia nawapongeza
wanajeshi wetu walioko Darfur na Lebanon kwa kazi yao njema waifanyayo. Wote nawaomba
waendelee kudumisha nidhamu na weledi, mambo yaliyowafanya wapewe sifa nyingi na kuheshimiwa.
Wameiletea nchi yetu heshima kubwa. Bahati mbaya, katika kutimiza wajibu wao
huo wa kimataifa tumepoteza vijana wetu 10, saba Darfur na watatu Kongo. Narudia
kutoa pole kwa Jeshi letu na familia za marehemu kwa msiba mkubwa uliowakuta. Napenda
kuwahakikishia kuwa daima tutauthamini na kuuenzi mchango wao. Wanajeshi wote tunawatakia
heri na fanaka tele katika mwaka 2014.
Jumuiya ya Afrika Mashariki Ndugu
Wananchi; Mwaka huu, ushiriki wetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umepita katika
mtihani kidogo kufuatia ndugu zetu wa Uganda, Rwanda na Kenya kufanya mambo ambayo
yalijenga hisia ya kuwepo mifarakano. Pia yalileta hofu kuwa hata uhai wa Jumuiya
yenyewe ulikuwa mashakani. Katika mkutano uliopita wa Wakuu wa Nchi wanachama wa
Jumuiya uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2013 mambo hayo tuliyazungumza kwa uwazi na
kidugu. Tumeelewana kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Ndugu Wananchi;
Katika mkutano wa Kampala tuliamua mambo matatu makubwa na muhimu katika kuendeleza
agenda ya utangamano wa Afrika Mashariki. La kwanza, tulikubaliana kuhusu Itifaki
ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki na kutia saini. Hii ndiyo hatua ya
juu ya utangamano wa kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tumekuwa tunashirikiana
katika kuwianisha sera za uchumi, fedha na bajeti, kwa uamuzi huu sasa tunaelekea
kwenye kuwa na sera moja ya fedha na bajeti kwa mambo hayo na hatimaye sarafu moja.
Baada ya hatua hii, inayofuata ni ile ya utangamano wa kisiasa, yaani Shirikisho la
Kisiasa. Katika mkutano wetu wa Kampala tulikubaliana kuwa nchi wanachama ambazo
hazijakamilisha kutoa maoni yao, zifanye hivyo kisha baada ya hapo tuzungumzie jambo
hilo na kulipa mwelekeo. Ndugu Wananchi; Vilevile katika kikao chetu cha Kampala,
tuliridhia mpango wa utekelezaji wa uamuzi wetu wa awali wa kuanzisha Himaya Moja
ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la mfumo au utaratibu huu ni kufanikisha
utekelezaji wa malengo na madhumuni ya Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki. Utaratibu
huu utarahisisha na kuharakisha uingizaji na utoaji wa bidhaa katika bandari na mipaka
ya nchi za Afrika Mashariki. Pia, utaondoa vikwazo visivyokuwa vya kodi katika uingizaji
na usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi wanachama kwenda nchi nyingine. Kwa jumla, Himaya
Moja ya Forodha itasaidia biashara kukua na hivyo uchumi wa nchi wanachama kukua na
kuboresha ustawi wa wananchi wa Afrika Mashariki. Narudia kuwakumbusha wenzetu
wa Wizara ya Afrika Mashariki na Wizara ya Fedha kutengeneza utaratibu mzuri wa kuelimisha
jamii kuhusu Umoja wa Fedha na Himaya Moja ya Forodha. Nawataka Wizara ya Fedha,
Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani,
Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya Mapato na Jeshi
la Polisi, kuhakikisha kuwa taratibu zote husika kuhusu Himaya Moja ya Forodha zinakamilishwa
mapema. Nia yangu na yetu sote ni kuona utekelezaji unaanza mara moja. Hili ni jambo
lenye maslahi makubwa kwa nchi yetu.
Medani za Kimataifa Ndugu Wananchi;
Katika medani za kimataifa, mwaka 2013 ulikuwa mzuri kwa Tanzania. Nyota ya nchi yetu
iliendelea kuangaza vizuri. Tumeendelea kuwa na uhusiano mwema na mataifa yote duniani
na hakuna nchi ambayo tuna uadui nayo. Pia tuna uhusiano mzuri na mashirika ya kimataifa
na kikanda yanayoshughulikia masula ya siasa, fedha na maendeleo. Vile vile, tuna
uhusiano mzuri na watu mashuhuri na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulikia
masuala ya maendeleo na ya kibinadamu. Kwa sababu hiyo tumepata misaada mingi
ya maendeleo na ya kibinadamu iliyochangia katika mafanikio tuliyoyapata katika maendeleo
ya kiuchumi na kijamii mwaka 2013. Napenda kwa niaba yenu nitumie nafasi hii kutoa
shukrani zangu za dhati kwa nchi, mashirika na watu waliochangia katika maendeleo
ya nchi yetu mwaka huu. Wakati tukiwashukuru, napenda kuwakumbusha kuwa misaada yao
bado tunaihitaji mwaka ujao (2014) na miaka inayofuatia. Ndugu Wananchi; Kwa
upande wa wageni, mwaka huu ulikuwa wa baraka sana kwa Tanzania. Tumepata heshima
ya aina yake ya kutembelewa na Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jiping tarehe 24 – 25
Machi, 2013 na Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama tarehe 01 - 02 Julai, 2013.
Pia tulitembelewa na Rais wa Sri Lanka Mheshimiwa Mahinda Rajapaksa tarehe 26 – 27
Juni, 2013. Waziri Mkuu wa Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra tarehe 30 Julai
mpaka Agosti 1, 2013 Pamoja na hao, tulipokea Wakuu wa Nchi na Serikali 19 waliokuja
kushiriki mkutano wa Smart Partnership Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28
Juni, 2013. Ndugu Wananchi; Vilevile, tulitembelewa na Marais Wastaafu wa
Marekani, Mheshimiwa Bill Clinton na Mheshimiwa George W. Bush. Nchi yetu inanufaika
na misaada inayotolewa na mashirika yao katika nyanja za afya na kilimo. Napenda
kutumia nafasi hii kuwashukuru wageni wetu wote hao kwa uamuzi wao wa kuja kututembelea.
Wameipa nchi yetu heshima kubwa. Ni matumaini yetu kuwa mwaka 2014 utaendelea kuwa
wa baraka kama huu tunaoumaliza leo. Pia nawashukuru sana Watanzania wenzangu kwa
kuwapokea vizuri wageni wetu. Wameondoka nchini wakiwa na furaha kubwa na kumbukumbu
nzuri kuhusu nchi yetu. Licha ya kutembelewa, mimi na viongozi wenzangu Wakuu wa
Nchi yetu tulialikwa na kufanya ziara katika nchi mbalimbali duniani. Pia tumeshirikishwa
katika mikutano mbalimbali ya kimataifa. Ziara hizo zimekuwa na manufaa makubwa
kwa nchi yetu. Ndugu Wananchi; Katika kikao cha Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika
kilichofanyia mwezi Januari, 2013 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu
wa Nchi za Afrika ya kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi. Mwenyekiti
wa Kamati hiyo ndiye huwa mwakilishi na msemaji wa Bara la Afrika katika majukwaa
ya kimataifa ambapo masuala hayo yanazungumzwa au kushughulikiwa.
Kwa ajili
hiyo nilikwenda Warsaw, Poland kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 19 wa Mabadiliko ya Tabia
Nchi uliofanyika tarehe 11 – 22 Novemba, 2013. Katika mkutano huo hatukufanikiwa
vya kutosha. Hivi sasa matumaini yetu yapo katika mkutano wa mwakani (2014) nchini
Peru. Iwapo tutafanikiwa tutakuwa tumejenga msingi mzuri utakaowezesha Mkutano wa
Paris mwaka 2015 kufanikiwa kupatikana Mkataba wa Kimataifa unaozifanya nchi ziwajibike
kisheria kwa masuala yahusuyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi. Ikishindikana
Peru na kama mataifa yataendelea kukaidi katika mkutano wa Paris, hatma ya dunia yetu
itakuwa mashakani kwani hali si nzuri hata kidogo. Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tunaoumaliza nchi za SADC tumepoteza mmoja wa viongozi wetu mashuhuri, shujaa
Nelson Mandela. Nilipata nafasi ya kuwawakilisha katika sala ya kitaifa, kutoa heshima
za mwisho na mazishi yake. Kule Qunu, nilipewa nafasi ya kuzungumza ambayo niliitumia
kuelezea uhusiano wetu na shujaa Mandela, ANC na mchango wa Tanzania kwa ukombozi
wa kusini mwa Afrika. Hotuba yetu ilipokelewa vizuri sana na wenyeji kwani niliwaelezea
baadhi ya mambo ambayo walikuwa hawayajui. Watu wengi wa Afrika Kusini na duniani
kwa jumla sasa wanaufahamu vizuri mchango mkubwa wa nchi yetu kwa ukombozi wa Afrika
Kusini. Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema, peponi roho ya shujaa
Nelson Mandela.
Miaka 50 ya Mapinduzi na Muungano Ndugu Wananchi;
Mwaka ujao (2014) ni wa aina yake katika historia ya nchi yetu. Ni mwaka ambao tunatimiza
miaka 50 tangu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12,1964 na miaka 50 ya Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika ziungane na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Aprili 26, 1964. Ni mwaka wa kutambua na kusheherekea mafanikio tuliyoyapata.
Lakini, ni mwaka wa kuweka nadhiri ya kupata mafanikio makubwa zaidi miaka 50 ijayo
na kuendelea. Tutakiane heri katika kusheherekea siku hizo adhimu.
Shukurani Ndugu
Wananchi; Napenda kuchukua nafasi hii adhimu kuwashukuru kwa dhati Makamu
wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda,
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd. Viongozi Wakuu wenzangu
hao nawashukuru kwa msaada mkubwa walionipa na wanaoendelea kunipa katika kuiongoza
nchi yetu mwaka 2013. Naomba tuendelee hivyo mwaka 2014 kwa maslahi ya nchi yetu na
watu wake. Nawashukuru pia Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali zetu mbili
kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuongoza na kusimamia utekelezaji wa miradi na shughuli
mbalimbali za Serikali. Kazi yao nzuri ndiyo iliyotupatia mafanikio tunaojivunia
leo. Naomba sote tutambue kuwa bado zipo mbele yetu kazi nyingi na changamoto kubwa
na nzito za kushughulikia katika jitihada zetu za kuwaletea wananchi na nchi yetu
maendeleo. Tunao wajibu wa kudumisha umoja, mshikamano, amani na utulivu wa nchi
yetu. Hatuna budi kuendelea kushirikiana na kusaidiana pamoja na kufanya kazi kwa
bidii zaidi mwaka ujao 2014 kwa niaba na kwa maslahi ya watu waliotuchagua. Ndugu
Wananchi; Kwa namna ya pekee nawashukuru sana Watanzania wote po pote
pale walipo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali na kufanya kazi kwa bidii na maarifa
kujiletea maendeleo. Hali kadhalika nawapongeza kwa uelewa wenu ulioiwezesha nchi
yetu kuendelea kuwa kisiwa cha amani. Nawaomba tuendelee na moyo huo wa kuipenda nchi
yetu na kujitolea kwa ajili ya utulivu wake na maendeleo yake na yetu sote. Naomba
pia nimalize kwa kuwashukuru viongozi wetu wa dini wa madhehebu mbalimbali pamoja
na waumini wao kwa sala na maombi katika kipindi chote cha mwaka unaoisha leo. Sala
zao na maombi yao yametupa nguvu na faraja katika vipindi vigumu ambavyo tumevipitia.
Naomba muendelee kuliombea taifa letu ili lipate baraka na neema ya Mwenyezi Mungu.
Mwisho
Ndugu Wananchi; Naomba tuzidi kuombeana heri ili mwaka ujao uwe wa baraka
na mafanikio makubwa zaidi. Twendeni tukasherehekee mwaka mpya kwa amani na utulivu.
Nawatakia heri na fanaka tele katika mwaka mpya wa 2014. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu
Ibariki Afrika. Asanteni sana kwa kunisikiliza.