2014-01-01 08:23:43

Wekezeni kwenye tunu msingi za kimaadili na utu wema ili kupambana na majanga ya kumong'onyoka kwa maadili!


Kardinali Paul Poupard, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, ili kukabiliana na majanga yanayotokana na kumong’onyoka kwa tunu msingi za utu na maadili mema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inawekeza zaidi na zaidi katika tunu msingi za kimaadili kwa njia ya elimu makini. RealAudioMP3

Vijana wafundwe kutambua na kuthamini tunu msingi za maisha ya adili na utu wema badala ya kung’ang’ania haki ambazo wakati mwingine zinasigana na maadili. Ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Kardinali Paul Poupard mjini Paris, Ufaransa wakati akichangia mada kwenye warsha iliyokuwa imeandaliwa na Taasisi ya Robert Schuman kwa ajili ya Ulaya, wakati wa Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu alipofariki Bwana Schuman ambaye ni kati ya waasisi wa Umoja wa Ulaya.

Bara la Ulaya lilibarikiwa kuwa na tunu msingi za maisha ya kiutu, kiroho na kijamii, lakini kadiri siku zinavyokwenda mbio anasema Kardinali Poupard, mambo yanakwenda mrama! Jambo la kushangaza ni kuona kwamba, kuna baadhi ya wanasiasa wanapenda kuridhisha kundi la watu wachache, kwa ajili ya mafao yao binafsi, huku kilio cha wengi kuhusu: fursa za ajira na matarajio ya watoto wao kwa siku za usoni, hayasikilizwi wala kushughulikiwa.

Mabadiliko kutoka katika Jumuiya ya Ulaya na kuelekea Umoja wa Ulaya yamesababisha wananchi wa Bara la Ulaya kuzamisha Meli ya mshikamano na upendo na kung’angania Meli ya umoja wa kiuchumi, ambayo kwa sasa kimekuwa ni kilio cha wengi kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Mshikamano wa dhati, mafao ya wengi ni kati ya vipaumbele vilivyotolewa na waasisi wa Umoja wa Ulaya, kwa wakati huo. Inasikitisha kuona kwamba, ubinafsi, upweke na mafao binafsi yanapigiwa debe zaidi kuliko hata mambo msingi yanayowaunganisha wananchi wa Bara la Ulaya na jirani zao.

Wananchi wengi Barani Ulaya hawaridhiki na mwenendo wa maisha kwa sasa. Kuna malalamiko mengi yanayowafanya watu kuanza kukata tamaa ya maisha hasa kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa: hasa ukosefu wa fursa za ajira ambalo kwa sasa limekuwa ni janga la wananchi wengi Ulaya; wafanyabiashara wanakata tamaa na kuanza kufunga shughuli za uzalishaji mali hali ambayo inawanyima vijana wengi kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kodi na mapungufu yake; rushwa na ufisadi, mmong’onyoko wa maadili na utu wema miongoni mwa viongozi wa kisiasa ni kati ya mambo ambayo yanawachanganya wananchi wengi Barani Ulaya. Watu wamekosa imani na masuala ya kisiasa kwani huko wanaingia watu kwa ajili ya kutafuta masilahi binafsi. Mambo yote haya yamepelekea watu kukosa imani na wanasiasa pamoja na serikali zao, kiasi kwamba, migomo na maandamano dhidi ya Serikali ni mambo ambayo yamekuwa ni chakula cha kila siku kwa wananchi wengi.

Kardinali Paul Poupard anasema, kuna haja kwa Bara la Ulaya kutafuta tena utambulisho na sura mpya katika masuala ya kiuchumi, kifedha na kisiasa, kwani ile ndoto ya ufanisi katika utawala inazidi kutoweka siku hadi siku katika Jumuiya ya Kimataifa kama inavyojionesha hata kwenye Umoja wa Mataifa.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika elimu na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, kwani wao ndio waathirika wakubwa wa ukosefu wa fursa za ajira na mmong’onyoko wa maadili na utu wema.








All the contents on this site are copyrighted ©.