Umuhimu wa kukuza majadiliano ya kina kama njia ya kutafuta suluhu ya kinzani na migogoro
ya kijamii!
Kanisa Katoliki nchini Mali limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi
na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao kutokana na vita pamoja
na kinzani za kijamii, kisiasa na kidini. Kwa sasa hali inaonekana kuwa shwari kidogo,
lakini bado watu wana wasi wasi mkubwa wa usalama wa maisha na mali zao.
Ni maneno
ya Askofu Laurent Biefuorè Dabirè wa Jimbo Katoliki Dori, nchini Mali, wakati akizungumza
na viongozi wa Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji, kufuatia machafuko
ya kisiasa yaliyojitokeza hivi karibuni nchini Burkina Faso. Hali ya usalama si shwari
sana Kaskazini wa Burkina Faso, kiasi kwamba, Wamissionari kutoka nje ya Burkina Faso
wanatekeleza dhamana na maisha yao katika mazingira hatarishi na kwamba, wanaweza
kutekwa nyara.
Vita na kinzani za kijamii na kisiasa nchini humo zimepelekea
wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaoyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama
wa maisha na mali zao. Zaidi ya wakimbizi 40, 000 wanahudumiwa katika kambi mbili,
lakini hali ni ngumu ikizingatiwa kwamba, hili ni eneo ambalo linakabiliwa na ukame
wa muda mrefu.
Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Mali linaendelea
kutoa msaada wa hali na mali kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Burkina Faso. Askofu
Laurent Dabirè anasema kwamba, hali ya usalama ni tete nchini Bukrina Faso tangu mwaka
1991, baada ya Seneti kufungwa kutokana ukata, hali ambayo imepelekea demokrasia kuwekwa
“rehani”.
Kanisa Katoliki pia limekuwa mstari wa mbele kuendeleza mchakato
wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam wanaounda asilimia kubwa ya
wananchi wa Burkina Faso. Lengo ni kutaka kudumisha misingi ya haki, amani, upendo
na mshikamano wa kidugu, daima waamini wakiwa mstari wa mbele kulinda na kutetea utu
na heshima ya binadamu pamoja na uhuru wa kuabudu. Kanisa pia linatoa huduma isiyokuwa
na ubaguzi katika sekta ya elimu na afya.
Jitihada za waamini na wafadhili
mbali mbali zinalenga kuchangia katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, dhamana inayovaliwa
njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.