2014-01-01 09:21:30

Msiwe watazamaji kutoka dirishani, shukeni chini kushiriki katika ujenzi wa Jiji la Roma kwa kuwajibika!


Baba Mtakatifu Francisko, Mwishoni mwa Mwaka 2013, amewaongoza waamini kusali Masifu ya Jioni kwa heshima ya Bikira Maria Mama wa Mungu; kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani, Te Deum pamoja na Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewakumbusha waamini kwamba, wanaishi katika nyakati za mwisho, zitakazofikia utimilifu wake pale ambapo Kristo atakuja mara ya pili kuwahukumu wazima na wafu ili kukamilisha kazi ya Ukombozi. Waamini watakuwa na fursa ya kumwona Mungu jinsi alivyo! Waamini watambue kwamba, upendo wa dhati wanaomwonesha Mwenyezi Mungu unachangia kwa namna ya pekee katika maisha yao ya uzima wa milele.

Nyakati kadiri ya Maandiko Matakatifu ni hija inayomwelekeza mwanadamu katika utimilifu wa matumaini yaliyoko mbele ya watu, ili kuweza kuonana uso kwa uso na Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ndiye chemchemi na sababu ya furaha ya watu wake. Mwaka 2013 umepita, lakini waamini na watu wenye mapenzi mema wanapaswa kujiuliza ni kwa jinsi gani ambavyo wamechangia katika maboresho ya Mwaka uliopita? Ni muda kiasi gani wameweza kuutenga ili kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu ili waweze kumwabudu?

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na wakazi wa Jiji la Roma kuchunguza dhamiri zao kwa ujasiri na kuona yale yanayotendeka, kwani kila mmoja wao ana mchango katika ustawi na maendeleo ya Jiji la Roma! Je, wameshiriki katika kudumisha maboresho ya Jiji la Roma, ili kulifanya Jiji hili liweze kukalika na kuendelea kuonesha moyo wa ukarimu kwa wageni na mahujaji. Kila raia anachangia kwa hali na mali kukuza au kubomoa Jiji la Roma.

Baba Mtakatifu anasema, Jiji la Roma lina uzuri wa pekee. Ni hazina ya maisha ya kiroho na kitamaduni. Lakini pia kuna watu wanaoteseka kutokana na umaskini wa hali na kipato; Roma ina mazingira ya kuvutia, lakini ina kundi kubwa la watu wanaokabiliana na hali ngumu kijamii. Roma ni Jiji lillosheheni watalii kutoka kila upande wa dunia, lakini kuna kundi kubwa pia la wakimbizi, watu wasiokuwa na makazi maalum.

Baba Mtakatifu anasema, kuna wafanyakazi wanaochakarika usiku na mchana kutekeleza wajibu wao, lakini pia kuna watu wanadhulumiwa kwa kupewa ujira kidogo, hata kama wote wanapaswa kutendewa haki, kwa kuzingatia utu na heshima ya kila binadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na wakazi wa Jiji la Roma kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu ili Jiji la Roma liendelee kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; mahali penye ukarimu na mshikamano wa dhati, kwa ajili ya mafao ya wengi! Baba Mtakatifu anawaonya waamini wasiwe watazamaji kutoka madrishani, bali washuke na kushiriki kikamilifu katika maendeleo na ustawi wa Jiji la Roma, kwa kutumia chachu ya Injili na kutambua kwamba, waamini kimsingi ni wajumbe wa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko ameukamilisha Mwaka 2013 kwa kumshukuru Mungu na kuomba msamaha hasa kutokana na uaminifu na uvumilivu ambao Mwenyezi Mungu anaonesha kwa waja wake. Bikira Maria Mama wa Mungu awasaidie waamini kuweza kumpokea Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kila siku iweze kupambwa na upendo wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.