Bikira Maria Mama wa Mungu ni chemchemi ya matumaini na furaha ya kweli!
Bwana awabariki na kuwalinda, Bwana awaangazie uso wake na kuwahurumia, Bwana awainulie
uso wake na kuwapa amani. Ni maneno ya Baraka kwa mwanzo wa Mwaka Mpya kutoka katika
Maandiko Matakatifu.
Ni maneno yaliyosheheni nguvu, ujasiri na matumaini yalisiyo
danganya kwani matumaini haya yanapata chimbuko lake kutoka kwa baraka ya Mwenyezi
Mungu na matashi mema ambayo Mama Kanisa anapenda kumpatia kila binadamu, kwa kukimbilia
tunza na upendo wa Mungu. Matashi haya yanapata utimilifu wake kwa Bikira Maria, Mama
wa Mungu. Hali inayoonesha ubora, dhamana katika imani ya Kikristo.
Hii ni
sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mama wa mungu,
sanjari na Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014. Mtaguso mkuu wa Efeso
ndio uliotamka na kufundisha kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu, Theotokos na mwangwi
wake ukaonekana mjini Roma kwa ujenzi wa Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu. Hapa waamini
wanayo nafasi ya kuheshimu Picha ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Ni kilio cha waamini
waliowataka Mababa wa Kanisa kutamka wazi kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria daima amekuwa mioyoni mwa waamini, katika
Ibada lakini kwa namna ya pekee katika hija ya imani ambayo ilifanywa na Bikira Maria
katika maisha yake na waamini wanajitahidi kuifuatilia. Bikira Maria ni kielelezo
makini cha fadhila ya imani, kwani katika maisha yake hapa duniani ametembea katika
njia ya maisha na matatizo kama binadamu wengine, lakini daima amekuwa ni hujaji wa
imani ambaye Yesu alimkabidhi kuwa ni Mama wa Kanisa pale chini ya Msalaba.
Baba
Mtakatifu anasema pale ambapo Yesu aliona imani ya wafuasi wake inatindika kutokana
na matatizo na kinzani akawakabidhi kwa Mama yake Bikira Maria, mwamini wa kwanza
kuamini, Mama ambaye imani yake haikupungua hata kidogo! Bikira Maria akawa Mama wa
wote pale alipomwona Mwanaye wa pekee akiyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi
wa ulimwengu.
Moyo Mtakatifu wa Maria ukafunuliwa wazi, ili utoe hifadhi kwa
wema na wabaya, kwa kupenda kama vile Yesu mwenyewe alivyopenda. Kielelezo makini
cha ushuhuda wa imani pake kwenye arusi ya Kana ya Galilaya, alipofanikiwa kuwaonesha
watu wa mataifa utukufu wa Mungu. Pale Mlimani Kalvari, moto wa imani uliendelea kuwaka
katika Ufufuko wa Mwanaye Mpendwa kwa kuwashirikisha wengine, kwa njia hii, Bikira
Maria akawa ni chemchemi ya matumaini na furaha ya kweli!
Baba Mtakatifu Francisko
anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Bikira Maria Mama wa Mkombozi anawatangulia
waamini ili kuwaimarisha katika imani, wito na utume wa Kanisa. Kwa njia ya mfano
wake wa unyenyekevu, utayari katika kutekeleza mapenzi ya Mungu anawawezesha waamini
kumwilisha imani yao katika hija ya Injili ya Furaha bila mipaka. Kwa njia hii, utume
wa Kanisa utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwani unaratibiwa na na Umama wa Bikira
Maria.
Baba Mtakatifu anawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria waamini
wote katika hija ya imani, matamanio yaliyomo mioyoni mwao bila kusahau mahitaji yao
msingi na yale ya ulimwengu katika ujumla wake; hasa kwa wale wenye njaa na kiu ya
haki na amani.