2014-01-01 15:11:01

Amani inajikita katika unyenyekevu, ukweli na upendo!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, tarehe Mosi, Januari 2014, amewatakia waamini na watu wote amani na maendeleo kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ni kiini cha historia ya mwanadamu. Alizaliwa, akafa na kuzikwa na utimilifu wa historia hii ni Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika amani, haki, uhuru na upendo na kwamba, Roho Mtakatifu ndiyo nguvu inayoongoza mchakato huu hadi kufikia utimilifu wake.

Roho Mtakatifu ni kiini cha upendo uliomwezesha Bikira Maria kupata mimba na kielelezo cha wajenzi wa amani. Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani ni matukio yanayokwenda sanjari, ili kuweza kuimba "Utukufu kwa Mungu juu mbinguni na amani kwa watu wenye mapenzi mema". Ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuyahifadhi haya yote ili kuyatumia kwa Mwaka Mpya wa 2014.

Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana amewakabidhi waamini na watu wote ujumbe wake wa kuombea Amani kwa Mwaka 2014 unaoongozwa na kauli mbiu "Udugu ni msingi na njia ya amani". Watu watambue kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja na wanaunda Familia moja ya binadamu, wote wanalengo moja, changamoto ya kila mtu kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa dunia mpya ambamo watu wanaheshimiana, wanakubaliana na kusaidiana.

Watu watambue uwepo wa vitendo vya uhalifu, ukosefu wa misingi ya haki na amani; mambo ambayo kamwe hawawezi kuyafumbia macho, mwaliko wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika msingi wa haki na mshikamano.

Tarehe Mosi, Januari, waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanapaaza sauti zao kwa jili ya kuombea amani duniani, changamoto ya kutembea katika njia ya haki na amani na Roho Mtakatifu alegeze mioyo migumu, ili hatimaye, amani iweze kutawala. Amani inajikita katika hali ya unyenyekevu, ukweli na upendo.

Baba Mtakatifu anawaweka waamini na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, ili kilio cha watu wanaoteseka na kudhulumiwa kwa vita, kiweze kusikika na watu wawe na ujasiri wa kuanzisha mchakato wa majadiliano na upatanisho badala ya kumezwa na hali ya kutaka kulipiza kisasi, kiburi na rushwa. Anawaalika waamini kushuhudia Injili ya Amani kwa vitendo.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, amemshukuru Rais Giorgio Napolitano wa Italia kwa salam na matashi mema kwa Mwaka 2014. Anawatakia heri na baraka viongozi na wananchi wa Italia ili waweze kutekeleza dhamana yao kwa kuwajibika barabara, huku wakijenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu, daima wakiwa na imani na matumaini.

Baba Mtakatifu amewashukuru waamini na wote walioshiriki kikamilifu katika mikseha ya sala ili kuombea amani sehemu mbali mbali za Italia. Kwa namna ya pekee amewatakia watoto kutoka Ujerumani kheri na baraka za Noeli na Mwaka Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.