Jipatanisheni, ili kujenga misingi ya haki na amani Sudan ya Kusini
Viongozi wa Makanisa nchini Sudan ya Kusini wanawataka viongozi wa Serikali na Kisiasa
nchini humo kusitisha mara moja vita na kuanza majadiliano yanayopania kujenga na
kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho na maendeleo ya wengi. Wanasiasa waistumie
migogoro ya kisiasa ndani ya vyama vyao kuwasababishia wananchi majanga kwa kuendekeza
ukabila usiokuwa na tija wala mashiko kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wa Sudan
ya Kusini.
Viongozi wa Makanisa wanasema, wanasiasa hawana budi kujipatanisha
kwanza na kwamba, vita si suluhu ya migogoro ya kisiasa na kwamba, wao kama viongozi
wa kidini wanapenda kukazia kwa namna ya pekee upatanisho miongoni mwa wanasiasa na
wananchi wa Sudan ya Kusini katika ujumla wao! Upatanisho ni ufunguo wa migogoro na
chanzo cha maendeleo ya wengi na kwamba, vita inayoendelea nchini humo itakuwa na
madhara makubwa ndani na nje ya Sudan ya Kusini.
Watu wanaendelea kupoteza
maisha yao kutokana na vita; baadhi ya vijana wamejiingiza katika vitendo vya uporaji
wa mali za watu na uvunjifu wa misingi ya haki na amani na kwamba, watu wengi wanahofia
usalama wa maisha yao. Serikali haina budi kuhakikisha kwamba, inadhibiti vitendo
vya majeshi ya ulinzi na usalama kwa ajili ya mafao ya wengi. Wananchi, majirani na
marafiki wajitafutie hifadhi katika maeneo salama na wapewe ulinzi wa kutosha!
Viongozi
wa Makanisa nchini Sudan wanaendelea kuuomba Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Misaada
Kitaifa na Kimataifa kuendelea kutoa huduma hii msingi kwa wananchi wa Sudan ya Kusini
wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha kwa sasa.