2013-12-31 09:50:51

Hakuna haki wala amani, ikiwa kama utu, heshima na utakatifu wa maisha ya mwanadamu havithaminiwi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na mwendelezo wa mchakato wa Uinjilishaji Mpya kwa njia ya huduma makini za kijamii, hivi karibuni, limezindua Chama cha Madaktari Wakatoliki nchini Kenya. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakazia pamoja na mambo mengine, mafao ya wengi na mshikamano unaoongozwa na kanuni ya auni ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani.

Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu katoliki Kenya katika hotuba yake ya uzinduzi wa Chama cha Madaktari Wakatoliki, anakazia kwa namna ya pekee maneno ya Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014 kwamba, hakuna amani ikiwa kama: utu, heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu hauthaminiwi. Hii ndiyo sababu msingi inayolifanya Kanisa Katoliki kujikita katika huduma ya afya kwa Jamii, ili kuendeleza ile kazi ya uponyaji iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe.

Kardinali Njue anasema kwamba, Kanisa linatoa huduma za afya katika mazingira magumu, mahali ambapo hata hakuna miundo mbinu ya barabara, lengo ni kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini kama alivyofanya Kristo mwenyewe, kwa kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utakatifu wa maisha ya binadamu. Maisha yanaanza pale mtu anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Lakini katika ulimwengu mamboleo, maisha ya binadamu yanakumbana na vitisho vingi.

Kardinali Njue anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuunga mkono juhudi za kulinda na kutetea zawadi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo. Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kutekeleza wajibu huu msingi kwa kuwahamasisha wafanyakazi katika sekta ya afya, kuzingatia maadili, kanuni na sheria za kazi; daima wakijitahidi kutimiza mapenzi ya Mungu katika shughuli zao na Mafundisho ya Kanisa Katoliki.

Kanisa linaendelea kuwahamasisha wanataaluma katika medani mbali mbali za maisha, kujiunga pamoja ili kutolea ushuhuda wa imani yao; kwa njia ya sala, tafakari ya kina pamoja na kubadilishana mawazo na wanataaluma wengine, kwa ajili ya mafao ya wengi. Ni matumaini ya Kanisa Katoliki nchini Kenya kwamba, Chama cha Madaktari kilichozinduliwa, kitaendeleza hija ya imani na kuishi kadiri ya changamoto zinazotolewa na Kristo mwenyewe.

Madaktari wanakumbushwa kwamba, wao ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, kumbe wawe kweli ni mashahidi amini ili watu wengine waweze kuyaona matendo yao makuu na hivyo kumshukuru Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, inayopaswa kufanyiwa kazi na Familia ya Mungu kwa kujikita katika maisha ya utakatifu, ili kukabiliana na changamoto pamoja na madhulumu mbali mbali yanayoendelea kuelekezwa kwa Kanisa, kutokana na baadhi ya watu kumezwa mno na malimwengu.

Uzinduzi wa Chama cha Madaktari Wakatoliki Kenya ni sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguzo mkuu wa Pili wa Vatican na miaka 20 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo II alipochapisha kwa mara ya kwanza Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Kanisa litaendelea kuwasindikiza katika maisha na utume wao kama Madaktari, kama sehemu ya mchakato wa ushuhuda unaopewa kipaumbele cha kwanza katika azma ya Uinjilishaji Mpya.

Madaktari Wakatoliki wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuinjilisha sekta ya afya kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha sanjari na huduma makini kwa wagonjwa; daima wakisimama kidete kulinda na kutetea utu na utakatifu wa maisha ya kila mgonjwa. Heri za Mlimani, ambazo kimsingi ni Muhtasari wa Mafundisho ya Yesu, ziwe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao kama Madaktari.








All the contents on this site are copyrighted ©.