Mpendwa Mwana familia ya Mungu katika Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo! Tukiwa
katika masaa ya mwisho kuelekea kufunga mwaka wa 2013 tangu kuzaliwa kwake YEYE aliyetumwa
na BABA; sote tunajawa na shauku ya kuuanza mwaka Mpya wa 2014. Na wengi tunasali
kumwomba Mungu mkarimu, atujalie kuuanza mwaka mpya salama. Wapendwa Kanisa
la nyumbani, Uhai ni zawadi kutoka kwa Muumba wetu. Na muda pia ni zawadi kutoka kwake
aliyepo na anayependa tuwepo. Ni Mungu peke yake ndiye anayejua muda wetu wa kuwapo
hapa duniani, kwa sababu ni yeye mwenyewe ndiye ametupatia; na ndiyo maana twakiri
kwamba; “ndani yake yeye tunaishi, tunajimudu, na kuwa na uhai wetu” [Mdo. 17:28].
Kwetu sisi, tunaupokea UHAI na MUDA kama zawadi. Ni mwito kwa kila mmoja wetu kuitumia
zawadi hii kwa shukurani. Zawadi hii, izae matunda, na iwafaidie wengine. Na mahali
pa kwanza kabisa pa kuienzi zawadi ya muda na uhai ni KATIKA KANISA LA NYUMBANI, YAANI
KATIKA FAMILIA. Iwapo katika familia kwa bahati mbaya kabisa, watu hawafundishwi kuheshimu
na kutunza zawadi ya uhai na muda, daima tutakuwa ni watu wasiojali uhai wa wengine
na hivyo kuwasababishia mateso, na sisi wenyewe kujiletea shida na ugumu wa maisha.
Tunapoomba Mungu atujaalie kuuona mwaka mpya, au wengine tunaomba tujaaliwe maisha
marefu duniani. Ni jambo zuri sana unaliomba. Swali linakuja; unaomba maisha marefu
ili uwe unafanya nini? Ni nini haswa kinakuthibitisha wewe uendelee kuishi maisha
marefu? Kuna mafaa yoyote kwako na kwa jamii inayokuzunguka? Ni swali dogo, lakini
ni la muhimu. Endapo sote tunatambua thamani ya uhai na muda, basi tutajitahidi sana
kutumia uhai na muda wetu kwa kuwafaidia wengine. Na ukitaka ujifaidie mwenyewe na
wale wanaokuzunguka jifunze kutunza uhai, kutumia karama zako na muda vizuri. Muda
ni zawadi na zawadi hutumiwa kwa shukurani. Na muda hauji mara mbili. Mpendwa,
zawadi ya mwaka mpya ipo mbele yako. MAISHA NA MIPANGO. Ni dhambi kuishi tu, bila
mpango wowote wa maisha. Una mpango gani wa maendeleo ya kimwili au ya kiroho kwa
mwaka ujao? Wapendwa, kwa sababu ya kukosa dhamiri ile ya kujali na kuutumia vizuri
muda; wengi sana katika maeneo yetu, tumeendekeza utamaduni wa uvivu. Katika familia
kuna uvivu uliyo kithiri. Mashuleni kuna uvivu uliokithiri, halafu watu wanataka wafaulu
tu; maofisini huko kuna uvivu uliokithiri, lakini watu wanataka mishahara ya juu na
marupurupu. Yaweza kuwa bahati mbaya hata makanisani tukawa na watu wavivu kupita
kiasi, wasiojua thamani ya muda. Matokeo ya uvivu huo, ni kukosa ufanisi katika mambo
mengi. Jambo mojawapo ambalo linatupelekea kuwa na maisha magumu kwa viwango mbalimbali,
NI KUKOSA MATUMIZI SAHIHI YA MUDA. Tunapokosa ufanisi sasa, wengi TUNAJENGA UTAMADUNI
WA KULALAMIKA TU. Katika familia ya wavivu, baba atalalamika maisha magumu, mama naye
atalalamika siku nzima maisha magumu, watoto wote watalalamika nao, mwisho hata jiko
na viti vitaanza kulalamika, na hakuna siku wanapotafuta muda kuketi na kuona namna
gani wajikwamue na ugumu huo. Ni kulalamika tu, na kuzungukazunguka kutafuta miujiza.
Iwapo kila mmoja analalamika SASA NANI MWENYE KUTIMIZA WAJIBU? Wavivu na walalamishi,
wanatabia ya kutoridhika na kutoona jema kutoka kwa yeyote. Daima wataona wanaonewa
au wanadhulumiwa tu. Kumbe wanajidhulumu wenyewe kwa kuendekeza uvivu na kukosa kuutumia
muda kwa shukurani. Ndugu Mpendwa, kama mwaka huu unaoisha haukutumia kwa shukurani,
tuliitumikisha midomo kwa kulalamikalalamika tu; na tukaiadhibu miili yetu kwa kuendekeza
uvivu, basi, kwa mwaka ujao, TUFANYE MAPINDUZI YA FIKRA, yatakayotupelekea katika
MAPINDUZI YA MAISHA NDANI YA FAMILIA ZETU. Uvivu awe ni adui yetu mkubwa na tumpige
vita kwa moyo wote. Mzee wetu alitufundisha, KAZI NI KIPIMO CHA UTU. Na sisi tunaongeza
hapo, UVIVU NI KIPIMO CHA USHETANI. Fanya kazi kwa juhudi sahihi na maarifa sahihi
ndani ya muda sahihi. Wapendwa, tuipokee zawadi ya mwaka mpya, na tuwe tayari kutumia
muda vizuri kwa faida yetu na ya wengine pia. Tukwepe utamaduni wa uvivu, unaozaa
tabia ya kulalamika mpaka midomo inapinda. Tukwepe tabia ya uvivu inayotuletea madeni
yasiyolipika. Muda ni mali. Kutoka Studio za Radio Vatican, kukuletea kipindi hiki
ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.