2013-12-30 10:16:42

Mshikamano wa upendo, imani na matumaini na wananchi wa DRC


Kipindi cha Noeli ni wakati muafaka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuachana na mazoea, ili kutoka kifua mbele kutangaza Injili ya Furaha, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ameamua kuandamana na mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani, kwa Neno wa Mungu kufanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu, changamoto kwa waamini kumwilisha ndani mwao, upendo na majitoleo ya dhati kwa wote wanaoteseka na kusumbuka katika maisha! RealAudioMP3

Ni mwaliko wa kuwa ni wajumbe wa Injili ya Furaha kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa kujikita katika mshikamano wa upendo, ukarimu na umoja. Yesu ni njia, ukweli na uzima, mwaliko wa kukumbatia, kukiri na kushuhudia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Yesu bado anaendelea kujionesha kati ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jami; wakimbizi na wahamiaji; wagonjwa na waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya!

Yesu aliyezaliwa katika hali ya umaskini mjini Bethlehemu anawaonesha waamini utajiri unaofumbatwa katika imani na hija inayobubujika matumaini na mapendo, mwaliko wa kujenga na kuimarisha urafiki na udugu unaopata chimbuko lake kutoka katika undani wa maisha ya mwamini anayejitahidi kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu. Noeli ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa watu wake na mwanzo mpya wa imani na matumaini!

Hivi ndivyo Askofu Antonio Stagliano wa Jimbo Katoliki Noto anavyoandika katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2013. Huu ni mwaliko wa kuanza hija ya kumwendea Yesu, ili kukutana na hatimaye kumfahamu vizuri zaidi; tayari kumshuhudia kwa njia ya imani tendaji sanjari na kutangaza Injili ya Furaha kwa watu wa Mataifa kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Huu ndio mwelekeo wa kimissionari unaopaswa kufanyiwa kazi wakati wa Kipindi cha Noeli; yaani Kanisa lijenge utamaduni wa kujadiliana na walimwengu kwa uwazi na umakini mkubwa; tayari kumwachia nafasi Yesu ili aweze: kuganga na kuponya; kusafisha na kuokoa!

Waamini wajifunze kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; kwa kuwapokea na kuwakirimia jirani zao ule upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo; ili kwa pamoja, waweze kujenga na kuimarisha Familia ya Mungu inayowajibika. Kipindi cha Noeli ni wakati muafaka wa kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu: kwa kujikita katika huruma, ukarimu na heshima; kila mwamini awajibike barabara katika utekelezaji wa majukumu na dhamana yake kwa Familia, Jamii na Kanisa.

Askofu Antonio Stagliano anasema, ukarimu ni fadhila inayopaswa kutolewa ushuhuda, kwani Mungu ni upendo. Jimbo Katoliki la Noto, lililoko nchini Italia, linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na Jimbo Katoliki la Butembo- Beni, lililoko nchini DRC kwa njia ya huduma ya mapendo.

Waamini wanaoishi katika maeneo haya bado wanaendelea kuteseka kutokana na vita, migogoro na kinzani za kijamii. Jimbo Katoliki la Noto, linataka kuwashirikisha Injili ya Furaha kwa kuzindua Kituo cha Tiba ya Moyo kijulikanacho kwa jina la “Pino Stagliano” Kumalizia ujenzi wa Chuo cha Kilimo cha Nino Baglieri”.

Huu ndio Uinjilishaji Mpya unaofanywa kwa njia ya ushuhuda wa upendo unaobubujika kutoka kwa Yesu Kristo, anayeendelea kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha: misingi ya haki na amani; majadiliano na upatanisho, ushirikiano na mshikamano wa dhati, katika uhuru na sala.








All the contents on this site are copyrighted ©.