2013-12-30 09:57:51

Dhana ya Familia ya Mungu ndani ya Kanisa


Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu Katoliki Arusha, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema dhana ya Familia ya Mungu ndani ya Kanisa inapata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwa kutambua kwamba, Imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na upendeleo wa pekee kutoka kwa Kristo ambao mwamini anaupata kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. 00:04:54:86
Askofu mkuu Lebulu anasema, wote ni watoto wa Mungu na ndugu zake Kristo, licha ya mapungufu ya kibinadamu, lakini Kristo haoni haya kuwaita kuwa ni ndugu zake. Mwaka wa Imani imekuwa ni fursa muhimu sana kwa waami: kukiri, kuadhimisha, kuishi na kusali; sanjari na kukuza pamoja na kuitangaza Imani kwa watu wengine.
Familia ya Mungu inakumbushwa vizingiti vinavyoendelea kuikabili Familia katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hivyo haina budi kusimama kidete kulinda na kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Vikwazo na vizingiti hivi ni mambo yanayotaka kubomoa tunu bora za maisha ya ndoa na familia kadiri ya Mpango wa Mungu kwa mwanadamu.
Askofu mkuu Lebulu anaikumbusha Familia ya Mungu kwamba, inawajibu na dhamana ya kukuza na kuendeleza Imani kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili. Wao kama Familia ya Mungu ni wadau wakuu katika kukuza na kuendeleza kazi ya uumbaji na ukombozi. Kama Familia, wanapaswa kukuza ndani mwao fadhila za kimungu na kibinadamu; karama na mapaji ya Roho Mtakatifu.
Askofu mkuu Lebulu anaendelea kukazia kwamba, Familia ya Mungu haina budi kuwa na moyo na ari kuu ya kutambua na kuheshimu kwamba, ni watoto wa Mungu, wenye dhamana na wajibu wa kurithisha Imani kwa watoto wao. Waendelee kuwa ni mashahidi amini wa Imani inayojinesha katika hisia, maneno na matendo. Imani hii ishuhudiwe zaidi katika matendo kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu, ili watu wanapoyaona matendo yao mema, waweze kumtukuza Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.