2013-12-30 10:46:29

Changamoto za kifamilia katika ulimwengu mamboleo!


“Ondoka, mchukue mtoto na mama yake, mkimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie..” [Mt 2:13 - 15]` Ni juzi tu tumesherehekea Sikukuu ya Krismasi. Bado tuna joto joto la Sikukuu hii njema na yenye wingi wa baraka. Na wengine hata keki au vijizawadi vya Krismasi vipo bado katika makabati au majokofu yao.

Dominika ya leo tunavutwa kujifunza mengi kutoka kwa familia hii takatifu ya Yosefu, Maria na Yesu. Kutoka kwa Adam na Eva tulirithi mtindo mbaya wa familia isiyoishi pamoja, isiyopanga pamoja, isiyomsikiliza mwenziye kwa jema litokalo kinywani mwa Mungu. Ilikuwa familia yenye kutega sikio kwa ya malimwengu, kwa nyoka, kwa marafiki tu.
Tulionja ndani ya familia hii mgawanyiko, lawama, wivu, kudhaniana vibaya na hata kuuana. Adam na Eva walipokosea, Adam alilaumu moja kwa moja Mungu wake, “..ni huyu mwanamke uliyenipa..” Na Watoto wao, Kaini na Abeli katika ujana wao na kazi zao hapakuwa na jicho la kujifunza kutoka kwa mwenziwe bali wivu na hasira hadi kumuua ndugu yake.

Leo katika Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yosefu, Maria na Mtoto Yesu wanatufunza misingi ya ukaaji pamoja wa familia, kuamua pamoja, kusikiliza sauti ya Mungu kwa pamoja, haidhuru imesikika kwa sikio la mmoja kwanza katika ndoa. Hakuna ubishi wala mahojiano. Mafunuo ya Mungu ni kweli hakika. Na hali hii inaalika mmoja kumheshimu mwenziye kwa kile alichoona au kufunuliwa na Mungu kuwa ni chema. Misingi hiyo inabeba roho ya kupendana, kuheshimiana, kujaliana, kuchukuliana katika hali zao na kusameheana.

Yosefu anaambiwa mchukue mtoto na mama yake aende kule anakoambiwa na malaika. Hii ni changamoto kwa kwake kwa vile Yosefu toka kuzaliwa hajawahi kufika Misri. Lakini kwa Neno la Mungu anatii. Ni kama Abrahamu mwingine anayenyofolewa katika nchi aliyoizoea ya Uria na kwenda nchi asiyoijua.


Leo sisi Mungu anatuambia kama Yosefu haya yafuatayo:
- Mchukue mwanao mpeleke shule nzuri apate elimu bora. Hujui fedha ya ada utapata wapi, shule yenyewe ipo wapi, na je utamudu hadi mtoto afikie darasa la saba au kidato cha nne ? kwa mzazi wenye kuthubutu wanajua safari hiyo itawalazimu kupunguza kinywaji au starehe ili mtoto afikie lengo lake. Wazazi wengi wameishia njiani katika hili kwa kuchanganya maisha na starehe zilizopitiliza. Watoto wangapi wamefukuzwa shule kutokana na kutokuwa na karo au mahitaji ya shule? Kusomesha, Matibabu ya Watoto na Mahitaji mengine ya kifamilia ni safari yetu ngumu ya Misri. Ni lazima tuwe na uthubutu na kujisadaka katika maisha yetu.

- Yosefu anaambiwa mchukue “mtoto na mama yake”. Hivi ni wangapi katika Krismasi hii, walitoka na wake zao pamoja kwenda kwa chakula cha pamoja nje mgahawani au kwa ndugu na jamaa wakaribu ? Wengi waliwaacha wake zao nyumbani kama pazia au stuli sebuleni. Wengi tunaanza kuona aibu kutoka nje na wake zetu kwa sababu ya muonekano wao, kupungua viwango au kutokana na kuepuka kuonekana na yule mwingine wa nje tunayemjali.

Yosefu aliondoka na Maria mguu kwa mguu hadi Misri. Maana yake, sisi katika tukio la kutoka nje ni vyema kuenda na ubavu wetu kama si kuwabeba hata watoto wetu. Mungu anayeokoa familia anaokoa familia yote – yaani, baba, mama na mtoto. Na ili sote waonje wokovu wa Mungu mambo madogo madogo hubeba wokovu na huwa na ni matendo ya kimungu. “..nilikuwa na kiu, msininyweshe..”(Mt 25:42)

- Watoto hujifunza kutoka kwa wazazi kila tufanyacho pindi tunapokuwa nao pamoja kwa mandali (picnic) au ufukweni mwa bahari au kwenda kutembelea ndugu. Na mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Na ndio maana somo la Kwanza la Yoshua bin Sira linamtaka mtoto aleyefunzwa vizuri na mamaye au babaye achukue wajibu wa kuwatunza wazazi wake “..Mwanangu msaidie baba yako katika uzee wake, wala usipate kumuhuzunisha siku zote za maisha yake..”(Yoshua Bin sira 3:12). Wazazi tusipolifanya hili mapema, watoto wengi watashindwa hata kuwazika wazazi wao.
Ni watoto wangapi leo wana nafasi nzuri ya maisha hapa Dar Es Salaam au mikoani – lakini wanashindwa kumpelekea kibaba cha unga au kilo ya sukari nusu kilo kwa mzazi wake ? Ni wangapi wanaishi katika nyumba mithili ya makasri ya kifalme Wakati wazazi wanaishi katika kijumba cha tope na manyasi juu ? Hii ni matokeo ya kutoonja maisha ya upamoja au kujaliana toka kwa baba na mama. Tukitaka tulilelewe vizuri na Watoto wetu tuliowasomesha kwa gharama kubwa, tuanze kuonesha upamoja na mama zao na wao wenyewe wakiwa wadogo. Kinyume chake, tusipoziba ufu tutajenga ukuta.

Tusali kwa ajili ya familia zetu za nchi yetu ya Tanzania ambazo zinakabiliwa na changamoto ya malezi, baba wa familia wawe Yosefu mwingine – na mama wa familia wabebe unyenyekevu na isikivu kama wa mama Bikira Maria. Na matokeo yake ya wazazi wapendanao yawe yale aliyoona mama mmoja kwa Yesu, “.. heri tumbo lililokuzaa, na maziwa uliyonyonya..”(Lk 11:27)

Jumapili Njema !
Padre Benno Michael Kikudo.
Jimbo kuu la Dar es Salaam.









All the contents on this site are copyrighted ©.