2013-12-28 15:25:07

Miaka 10 imepita tangu Askofu mkuu Michael Aiden Courtney alipouwawa kikatili nchini Burundi


Ilikuwa ni tarehe 29 Desemba 2003 siku ambayo Askofu mkuu Michael Aiden Courtney, Balozi wa Vatican nchini Burundi alipouwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Hadi leo hii hakuna mtu yeyote ambaye ametiwa nguvuni kwa kuhusika na mauaji haya! Baraza la Maaskofu katoliki Burundi, kwa takribani miaka minne wamekuwa wakitumia tarehe 29 Desemba ya kila mwaka, kufanya kumbu kumbu ya mauaji ya Askofu mkuu Courtney.

Hayati Askofu mkuu Courtney aliteuliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa Balozi wa Vatican nchini Burundi tarehe 18 Agosti 2000. Bado waamini wengi wanakumbuka mahubiri ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, aliyoyatoa tarehe Mosi, Januari 2004 kwa kusema kwamba, Askofu mkuu Michael Aidan Courtney alikuwa ni shahidi wa amani; aliyeuwawa kikatili wakati akitekeleza utume wake kama Mwakilishi wa Vatican nchini Burundi, katika mchakato wa kujenga na kudumisha majadiliano na upatanisho wa kitaifa.

Ni matumaini ya wapenda amani kwamba, damu ya Askofu mkuu Courtney na wapenda amani nchini Burundi, itakuwa ni mbegu ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa nchini Burundi na duniani kwa ujumla. Naye Kardinali Francis Arinze, siku mbili baada ya mauaji ya Askofu mkuu Courtney nchini Burundi, alisema kwamba, Askofu mkuu katika utume wake kama Mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, alikuwa anatangaza Injili ya upendo, upatanisho, amani na utulivu kati ya watu wa mataifa.

Ni kiongozi aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya ushuhuda kwa Kanisa la Kristo kwa njia ya Uinjilishaji; haki, amani na upatanisho nchini Burundi na sehemu mbali mbali za dunia ambako bado mtutu wa bunduki bado unaendelea kurindima na kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao!







All the contents on this site are copyrighted ©.