2013-12-27 09:29:45

Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu


Mpendwa mwana wa Mungu, leo tunasherehekea na kushangilia sherehe ya familia Takatifu. Masiha amezaliwa ndani ya familia hii. Ndani ya familia hii kuna majukumu ya kutekeleza ili Mwana wa Mungu akae mahali stahili na kwa namna hiyo atufundisha namna ya kutenda na kuishi kwenye familia zetu. RealAudioMP3

Somo la kwanza toka kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira linaweka mbele yetu fahari na heri ya kuwaheshimu wazazi na kuwatunza katika uzee wao. Heri ambazo ziko wazi kadiri ya somo hili ni kuwa na uzao, na si uzao tu bali kufurahia uzao huo. Kuwa na maisha marefu na uzee wa kusifika. Kwa kuwatunza wazazi na kuwapa heshima stahili mmoja afanya malipizi ya dhambi zake. Kwa hakika somo hili lasisitiza na kuweka mkazo juu ya amri ya nne ya Mungu. Waheshimu baba na mama upate miaka mingi na heri duniani.

Mtakatifu Paulo anapowaandikia Wakolosai anafafanua namna ya kuishi na kupendana katika familia. Anaweka wazi fadhila ambazo zajenga maisha ya familia yaani, unyenyekevu, utu wema, rehema na msamaha kwa kila mwanafamilia. Kilainisho cha fadhila hizi ni UPENDO kifungo cha ukamilifu. Kama familia na hasa kila mwanafamilia ataweza kuitikia mwaliko huu wa Mungu, basi familia nzima itakaa katika utulivu na amani ya kweli yaani inayokuza mshikamano. Mtume Paulo haishii tu kwenye upendo bila kuweka jambo la kutuweka pamoja yaani kusikia na kusikiliza sauti ya Mungu kwa njia ya Neno la Mungu. Kwa kutafakari Neno la Mungu tunajiweka tayari siku zote kukaa na Bwana aliye Neno wa Milele, aliye nuru angavu tuliyoipokea wakati wa siku ya Noeli.

Pamoja na fadhila nyingine, fadhila ya utii yatufaa kwanza kwa kutii Neno la Mungu na pili kutii mamlaka iliyowekwa na Kristu katika familia. Baba ni mkuu wa familia yafaa kumtiii na kumheshimu lakini yeye mwenyewe lazima aige mfano wa Kristu Mchungaji mwema anayewahangaikia kondoo wake, Yn 10. Ndiyo kusema aoneshe daima fadhila ya upendo kwa mke wake, watoto wake na watu wote .

Katika injili ya Matayo tunapata mfano wa familia iliyo katika mahangaiko ya maisha kama sisi. Familia inayolazimika kwenda uhamishoni Misri. Hivi leo katika ulimwengu watu wanakuwa wakimbii toka nchi zao kwa sababu za kisiasa kuichumi na mara zote wanapata mateso. Yafaa kuangalia mifumo yetu ya kisiasa na kiuchumi ili uweza kupunguza na hatimaye kutokomeza uozo huu. Mpendwa msikilizaji Mama Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu wanakimbilia Misri baada ya tangazo kuwa Herode alitaka kuangamiza Mtoto Yesu katika kundi la watoto wengine.

Jambo hili si geni kwa watawala kuwaangamiza watoto hivi leo.Tunakumbuka Farao jinsi alivyowaangamiza watoto wote wa kiume wa Waisraeli kwa kuagiza watupwe katika mto, Kut. 1:15-22 Katika maangamizi haya Musa atakuwa mtoto wa pekee atakayeponyoka katika mauaji hayo. Ni katika mantiki hiyo Herode anapoagiza wauwawe watoto wote katika Betlehemu Mtoto Yesu ataponyoka na kukimbiziwa Misri. Habari hii atapewa Mt Yosefu kwa njia ya Malaika katika ndoto.

Mpendwa msikilizaji, Musa kadiri ya simulizi katika kitabu cha Kut. 2:15 atakimbia tena kuuwawa na kisha ataambiwa na Mungu, rudi Misri kwa maana wale wote waliotaka kukuua wamekwishakufa! Na kwa namna hiyo, Musa atarudi huko, Kut. 4:19-20. Basi mpendwa msikilizaji maneno anayoambiwa Musa ndiyo tunayoyapata katika Injili, yaani baada ya kufa Herode, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema “kutoka Misri nalimwita mwanangu……kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto”.

Mpendwa mwana wa Mungu, Mwinjili Matayo ataka kutuambia yakuwa Masiha ni Musa mpya, ndiye atakayeongoza taifa la Israeli si toka Misri, bali toka ulimwengu kwenda mbinguni. Kwa maneno ya Injili yaani: kutoka Misri nalimwita mwanangu, mwinjili ataka kutuambia kuwa kama Waisraeli walivyosafiri kwa kuokolewa toka Misri mpaka nchini mwao, ndivyo Mwana wa Mungu alipenda kushiriki taabu hiyo, anachagua kuingia na kuchukua mwili wa mtu lakini pasipo kutenda dhambi na kwa njia hiyo kuweza kumkomboa. Kwa kuwa mtu Mwana wa Mungu atagusa furaha na mahangaiko ya mwanadamu yaliyo sehemu ya maisha yake. Oneni upendo wa Mungu kujishusha na kuwa mwanadamu wa ajili yako! Badilika basi kidogo angalau walau!

Mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, ni jambo gani jingine waweza kujifunza tokana na familia hii Takatifu? Jifunzeni kukaa pamoja na kujadiliana kama familia hii walivyofanya ili waweze kukimbia kifo ambacho kilikuwa kinamnyemelea mtoto wao. Hatari kama hiyo ni jambo la kawaida katika familia lakini je kuna mipango inafanyika kwa njia ya kuketi pamoja na kutafakari jinsi ya kutatua shida? Kwa upande wangu naona katika familia nyingi hakuna kukaa pamoja, hakuna majadiliano ya pamoja bali kila mmoja katika familia kufanya pekepeke! Hili limeua familia nyingi katika mazingira yetu.

Utemi katika mfumo dume ni hatari kubwa mno katika maisha ya familia zetu. Hebu basi mpendwa msikilizaji kuweni wa kwanza kuvunjilia mbali mfumo huo, kwanza kwa njia ya sala na pili kwa njia ya matendo. Nyenzo itakayokusaidia kufikia mabadiliko ya kweli ni kujiuliza swali hili daima: Hivi Yosefu na Maria waliwezaje kwendana pamoja, makubaliano yao yalisukumwa na nini? Kwa hakika wao walijikabidhi mikoni mwa Mungu na wakaweza kuongozwa na Neno la Mungu. Basi tunawaasa na kuwaonya wale watakaofunga ndoa wakumbuke si lelema bali wajibu na haki msingi katika ndoa vitekelezwe daima ili kuijenga na kuilinda ndoa mpaka mwisho wa nyakati.

Basi mpendwa mwana wa Mungu, hawa tuliowasikia katika Injili wakitenda kazi ya Bwana wanakuwa kichocheo cha wanafamilia kutenda vema katika familia zao daima wakilenga utukufu wa Kristu uliokwishafunuliwa kwetu na Bwana mwenyewe. Ninakutakieni heri tele wewe uliyemdau wa familia na hasa unapoweka nguvu yako kukuza tunu bora za familia, ukiangazwa na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Heri tena kwa jumuiya zote, parokia zote, mashirika ya kitawa mliojiweka chini ya usimamizi na ulinzi wa Familia Takatifu. Tumsifu Yesu Kristo Maria na Yosefu.

Tafakari hii inaletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.