2013-12-26 08:50:25

Jubilee ni kipindi cha toba, upatanisho na furaha ya ukombozi! Jimbo kuu Arusha, kumekucha!


Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu Katoliki Arusha baada ya kufafanua kwa kina na mapana lengo la Maadhimisho ya Jubilee ya Dhahabu ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki Arusha, leo katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha mafanikio ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo kuu la Arusha, Tanzania. RealAudioMP3

Askofu mkuu Lebulu kwa unyenyekevu mkubwa anabainisha kwamba, Jimbo kuu la Arusha lilijiwekea malengo na mikakati iliyopaswa kutekelezwa kuanzia kwenye Familia hadi katika ngazi ya Kijimbo. Kuna viashilia kama vile ujenzi wa: Makanisa, Maeneo ya Ibada, Shule za awali na huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Mwaka wa Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu la Arusha sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kimekuwa ni kipindi cha neema na baraka kubwa. Watu wamesali, wametafakari na kuimba sana. Waamini wamefanya semina, warsha na makongamano kuhusu Sakramenti za Kanisa na Mafundisho Jamii ya Kanisa na hatimaye, kutambua kwamba, Jubilee kimsingi ni: toba, upatanisho na furaha ya ukombozi. Makundi mbali mbali yanayounda Familia ya Mungu yamesali na kutafakari matendo ya Mungu, Jimbo kuu Katoliki Arusha na kumshukuru Mungu kwa kila jambo!

Askofu mkuu Lebulu anasema, tarehe 5 Mei 2013, ilikuwa ni siku ya kutabaruku Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Olesti, Jimbo kuu la Arusha, lakini furaha ya Familia ya Mungu ikatibuliwa na mlipuko wa bomu uliosababisha maafa na hofu kubwa miongoni mwa waamini waliokuwa wamekusanyika katika Ibada ya Misa Takatifu. Pamoja na yote haya, Jimbo kuu Katoliki la Arusha, linamshukuru Mungu, kwani si bure!

Askofu mkuu Josephat Lebulu kwa ari na moyo mkuu anasema, Jimbo kuu Katoliki Arusha limeandika historia; limeona na kuonja juhudi, sadaka na mjitoleo ya: Makatekista, Watawa na Mapadre kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita. Jambo kubwa ambalo kimsingi ndiyo mafanikio ya Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu la Arusha ni neema na baraka za uwepo wa Mungu na utendaji wake katika maisha na utume wa Jimbo kuu la Arusha katika kipindi chote hiki cha miaka 50. Leo hii Familia ya Mungu Jimbo kuu Katoliki Arusha, iko imara na thabiti, tayari kutoka kifua mbele kushuhudia Injili ya Furaha kwa watu wa Mataifa!

Hongereni sana Jimbo kuu la Arusha! Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican bado inaendelea kula sahani moja na Baba Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, anapoendelea kutushirikisha changamoto katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki Arusha linapojiandaa kuadhimisha kilele cha Jubilee hii hapo tarehe 29 Desemba 2013. Tafadhali mshirikishe na jirani yako!







All the contents on this site are copyrighted ©.