2013-12-26 10:29:07

Benin yafutwa kutoka katika orodha ya nchi zinazofaidika na misaada ya Marekani!


Serikali ya Marekani inayosimamia Shirika la Changamoto za Millenia, MCC, limeamua kuifuta Benin kutoka katika mataifa yanayofaidika na misaada ya maendeleo inayotolewa na Shirika hili kuanzia Mwaka 2014 kutokana na kukithiri kwa rushwa na ufisadi wa mali ya umma nchini humo!

Shirika la Changamoto za Millenia linasisitizia pamoja na mambo mengine umuhimu kwa nchi wanachama kuzingatia: utawala bora, ukweli na uwazi pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi unaolenga kuwanufaisha watu wachache ndani ya Jamii. Shirika hili lilianzishwa na Rais mstaafu George W. Bush ili kusaidia kuharakisha mchakato wa maendeleo kwa nchi changa zaidi duniani.

Kuanzia mwaka 2005, Benin imekuwa ikifaidika na misaada ya maendeleo iliyokuwa ikitolewa na Shirika la Changamoto za Millenia. Kufutwa kwa Benin kutoka katika orodha ya nchi wanachama wa MCC kutakwamisha harakati za maendeleo endelevu kwa wananchi wa Benin, ikiwa ni pamoja na kukosa fedha za maendeleo. Uamuzi huu unataka kuwa ni fundisho kwa viongozi wa Afrika kuhakikisha kwamba, fedha ya misaada inatumika kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya wajanja wachache!







All the contents on this site are copyrighted ©.