Vita na kinzani za kikabila ni mambo yanayokwamisha maendeleo ya watu!
Viongozi wa kidini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kusali kwa ajili
ya kuombea: haki, amani na upatanisho wa kitaifa nchini Sudan ya Kusini ambayo kwa
sasa inaelekea kutumbukia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe na hivyo kuzima kabisa
ndoto ya uhuru, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini.
Hivi karibuni,
Kardinali Peter Tukrson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, Askofu mkuu Justin
Welby wa Jimbo kuu la Cantebury, na Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kiangalikani duniani;
Lorna Hood, Mkuu wa Kanisa la Scotland, waliweka sahihi kwenye tamko la pamoja kwa
ajili ya kuombea amani Kusini mwa Sudan kwa kuwasihi viongozi wanaohusika kuweka silaha
zao chini na hivyo kuanza mchakato wa majadiliano ya kina ili kupata ufumbuzi wa mgogoro
huu unaoweza kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wa Sudan ya Kusini ambao waliokuwa
na matumaini ya kuona haki, amani na maendeleo vikishika kasi.
Noeli ni siku
kuu ya kuonesha mshikamano kwa maskini, wanyonge na wote wanaoteseka na kusukimizwa
pembezoni mwa Jamii, ili nao pia waweze kuonja haki na amani inayoletwa na Yesu Kristo,
Mfalme wa Amani. Viongozi hawa wa kidini wanakumbusha kwa namna ya pekee, ujumbe wa
Baba Mtakatifu Francisko unawataka binadamu kutambua kwamba, wao ni ndugu wamoja,
walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wanapaswa kupendana na kusaidiana kwa dhati.
Vita, kinzani na migogoro ya kikabila haina tena nafasi, bali waamini na watu
wote wenye mapenzi mema wanapaswa kujikita katika kutafuta, kudumisha na kuendeleza
amani ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini inamwajibisha binadamu.
Viongozi hawa wa kidini wanawapongeza viongozi wa Makanisa nchini Sudan ya
Kusini wanaoendeleza mchakato wa kutafuta suluhu ya mgogoro huu ambao tayari umekwisha
sababisha watu kadhaa kupoteza maisha yao na wengine wengi kuyakimbia makazi kwa kuhofia
usalama wa maisha yao!