2013-12-24 08:07:24

Tembeeni katika mwanga angavu unaoletwa na Mtoto Yesu


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2013, linawatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema Mwanga angavu kutoka kwa Mtoto Yesu, ili aweze kuwapatia mwanga huu wote wanaoishi na kutembea katika giza na uvuli wa mauti. RealAudioMP3

Huu ndio ule mwanga waliotangaziwa wachungaji waliokuwa wanalisha wanyama wao kondeni. Mwanga huu ni Kristo mwenyewe kama anavyojitambulisha katika Maandiko Matakatifu.

Ni Mwanga angavu uliowaongoza Mamajusi kutoka Mashariki, waliokuwa wanamtafuta Masiha, hadi walipomwona amelazwa kwenye Pangoni, mjini Bethlehemu. Yesu mwanga wa dunia, anaujaza ulimwengu furaha na matumaini kwa wale waliokata tamaa!

Askofu mkuu Paul Andrè Durocher, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada anasema, kamwe waamini hawataweza kusherehekea Mwanga unaobubujika kutoka kwa Mtoto Yesu, ikiwa kama wataendelea kumezwa na malimwengu na kusahau kuguswa na mahangaiko ya watu wanaowazunguka.

Mwanga angavu, kamwe hauwezi kujificha na kutoguswa na mahangaiko ya maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni mwanga unaopenda kuwashirikisha wapweke, ili waweze kuonja furaha ya kukutana na wafuasi wa Kristo wanaosambaza furaha ya Noeli kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kwa maneno na matendo yao adili na yenye kujikita katika mshikamano wa dhati.

Ni mwanga unaowaangalia wote wanaoendelea kuteseka kutokana na majanga asilia, sehemu mbali mbali za dunia, watu ambao wamepoteza matumaini kwa kuondokewa na wenzi wao na hata kile kidogo walichokuwa wamejitahidi kukitafuta kwa udi na uvumba. Ni mwanga wa matumaini kwa vijana wanaotafuta fursa za ajira na majiundo makini katika maisha yao.

Maaskofu Katoliki Canada wanasema, kusherehekea Noeli kwa mwanga angavu ni kuhakikisha kwamba, mwanga huu unawagusa wale ambao wamesahaulika na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ni mwaliko wa kufungua moyo na mfuko ili kushirikishana na wengine, kile kidogo kilichopo. Ni fursa ya kuendelea kuwakumbuka kwa hali na mali wanaoteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, vitendo vya kigaidi, vita na kinzani za kijamii, kwa kutambua kwamba, Familia ya mwanadamu kwa sasa inaishi katika ulimwengu ambao umegeuka kuwa kama Kijiji.

Noeli iwe ni fursa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kuwa na kiasi kwa kubana matumizi yasiyokuwa na tija wala mashiko. Wasidanganywe na matangazo ya biashara yanayotolewa na Makampuni makubwa yanayoangalia Kipindi cha Noeli na Mwaka Mpya kama wakati wa mavuno makubwa! Noeli ya Mwaka 2013 iwe ni fursa ya kufanya mabadiliko katika mtindo wa maisha, kwa kuangaziwa na Mwanga mpya wa maisha ambao ni Kristo mwenyewe anayekuja kuwatembelea watu wake, kama nyota ya asubuhi.

Ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli. Huu ndio Ufalme uliotangazwa na kuzinduliwa na Yesu Kristo kwa njia ya Fumbo la Umwilisho na kukamilishwa kwa Fumbo la Pasaka.








All the contents on this site are copyrighted ©.