2013-12-24 09:07:35

Dumisheni Injili ya Uhai dhidi ya Utamaduni wa kifo!


Noeli ni Siku kuu inayotoa nafasi kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu, kwake Yeye Bikira Maria akawa mwanadamu, katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi!

Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanalimwilisha Fumbo hili katika vipaumbele na uhalisia wa maisha yao. Noeli kiwe ni kipindi cha upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu; haki na amani kati ya mataifa! Noeli ni nafasi kwa waamini kuonja ule mshikamano wa upendo na ugudu kutoka kwa Kristo, ili kumkomboa mwanadamu aliyekuwa anatembea katika lindi la dhambi na uvuli wa mauti. Waamini wanakumbushwa kwamba, Mungu ni upendo, kumbe Noeli ni Siku kuu ya Imani, Matumaini na Mapendo.

Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, ili kutoa salam na matasgi mema kwa Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2013, anawaalika waamini kubadilika kwa kuthamini na kushuhudia Injili ya Uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo, unaokumbatia kwa namna ya pekee sera na vitendo vya utoaji mimba! Haya ni mambo ambayo yanaanza kuonekana kuwa ni kawaida, lakini ukweli ni kwamba, Jamii inakwenda kinyume cha ukweli wa Injili ya Uhai.

Waamini na watu wenye mapenzi mema wanaalikwa kusimama kidete kulinda na kutetea uhai ambayio ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wajitahidi kuyafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia pamoja na changamoto zake, ili wasimezwe na malimwengu kwa kukumbatia sera za utoaji mimba!

Sherehe za Noeli si kipindi cha kujirusha! Kufanya maasi kwa kutojiheshimu wala kuzingatia maadili na utu wema! Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa anasema kwamba, inasikitisha kuona kwamba, wakati wa Siku kuu kama Noeli, vitendo vya uvunjifu wa sheria, amani na maadili vinaongezeka kwa wingi. Hapana, huu ni mwelekeo potofu, Noeli kiwe ni kipindi cha kujitakatifuza kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu na matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji! Waamini wajitahidi kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na manyofu!

Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa anazipongeza taasisi na wale wote wanaosimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai. Anawataka waendelee kusonga mbele kwa ari na mwamko mkubwa zaidi bila ya kuogopa wala kuogopeshwa na wale wanaotaka kukumbatia utamaduni wa kifo! Jamii inapaswa kutambua na kuthamini zaidi uhai na kwamba, maisha ya binadamu si jambo la kuchezea!

Askofu msaidizi Nzigilwa amevishukuru na kuvipongeza vyombo vya hanari nchini Tanzania kwa kazi nzuri vinavyofanya kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi. Amevitaka vyombo hivi kuzingatia: taaluma na maadili ya kaz; weledi na utu wema. Vyombo vya habari visikubali kutumiwa na wajanja wachache kwa ajili ya kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo kwani hili linaweza kuwa ni janga la kitaifa kwa siku za usoni kama inavyojionesha kwa baadhi ya mataifa ambayo yalikumbatia utamaduni huu na kwa sasa yanajuta kufanya hivyo!

Noeli iwe ni Siku kuu ya Familia na Mshikamano wa Upendo kwa majirani! Watu wajifunze kuonesha na kuonjeshana ukarimu kwani jambo hili ni sehemu ya vinasaba vya tamaduni nyingi za Kiafrika!







All the contents on this site are copyrighted ©.