2013-12-24 10:19:24

Bikira Maria ni kioo cha imani, matumaini na mapendo!


Padre Faustin Kamugisha katika Kitabu chake cha "Hakuna Krismas bila Mama... Bikira Maria" anasema baraka zitasimama ikiwa kama Jamii itamsahau mama. Mama ni nambari moja na wala hana mpinzani. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Bikira Maria Mama wa Mkombozi, siku moja Mama mmoja alipaza sauti akamwambia Yesu, "heri tumbo lililokuchukua na maziwa uliyonyonya"

Hizi ni sifa kwa Bikira Maria Mama wa Mungu, anayestahili kuheshimiwa hasa wakati huu, tunapoadhimisha Siku kuu ya Noeli. Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili aliwahi kusema kwamba, wanawake ni walimu wa amani. Hawa ni wale wanaosimama kidete kupinga nyanyaso na kutoheshimiwa; ni watu wanaokumbatia Injili ya Uhai. Bikira Maria Mama wa Yesu, amepewa sifa ya kuitwa Malkia wa amani. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, alitunza zawadi ya Uhai, changamoto kwa wanawake wote kusimama kidete ili kulinda na kutetea Injili ya Uhai.

Mama Theresa wa Calcutta aliwahi kusema kwamba, wavurugaji wa amani leo hii ni wale wanaokumbatia utamaduni wa kifo unaokumbatia sera za utoaji mimba na kutowajali wanyonge na watu wasiokuwa na mtetezi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Siku ya Kuombea Amani kwa Mwaka 2014 anasema, Fumbo la Msalaba linawawajibisha binadamu kutaabikiana na kusumbukiana katika maisha kwani udugu unazima vita na madhara yake; udugu unaponya na kuganga mapungufu ya binadamu.

Kipindi cha Noeli kiwasukume wanawake kutolea ushuhuda wa sifa njema za kimama, kwa kuiga mfano wa Bikira Maria. Umama ni kazi nzito kama ambavyo aliwahi kusema Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili; kwani hawa ni wadau wakuu wa matunzo na makuzi kwa watoto wao: kiroho na kimwili. Mwanamke anayetunza watoto wake nyumbani kwa imani na mapendo makuu anafanya kazi halisi na yenye thamani kubwa katika Jamii. Wanawake wawe mstari wa mbele kutangaza Injili ya Uhai kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao; na kwa kutimiza nyajibu zao kwa Familia na Jamii na Jamii pia ioneshe hali na moyo wa kuwajali na kuwasaidia wanawake.

Bikira Maria awe ni mfano wa tunza bora ya kimama kwa watoto kama alivyofanya kwa Mtoto Yesu, tangu alipozaliwa hadi pale aliposimama chini ya Msalaba akamwona Mwanaye akihitimisha kazi ya Ukombozi. Bikira Maria ni mwanamke wa imani na mfano bora wa kuigwa. Kwa kumwangalia Bikira Maria, mwamini anaweza kujifunza tena kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu; ni Mama wa Matumaini hata pale ambapo hakuna tena cheche za matumaini.

Kwa kumwangalia Bikira Maria, waamini wajifunze kumpenda Mtoto Yesu na kwa njia hii, Bikira Maria anakuwa kweli ni Mama wa Mungu na Kanisa. Hongera Bikira Maria kwa kutuzalia Mtoto mwanaume, mwenye Ufalme na ukuu mabegani mwake!







All the contents on this site are copyrighted ©.