2013-12-23 11:37:07

Ombi la Papa Francisko kwa niaba ya familia zisizo na nyumbani.


Baba Mtakatifu Francisko , Jumapili iliyopita, baada ya sala ya Malaika wa Bwana, alitoa ombi kwa watu wote, binafsi, Taasisi, Makampuni na mamlaka, kujali mahangaiko na mateso ya watu wasiokuwa na makazi maalum yaani wasiokuwa na nyumbani. Papa aliotoa ombi hili kwa niaba ya familia zisizo na makazi , mbele ya mahujaji na wageni waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa kanisa kuu la Mtakatifu Petro,Vatican.

Taarifa inabaini Papa alitoa wito huo kwa kuhamasishwa na bango kubwa lililokuwa limebebwa na baadhi ya watu lenye maneno “ maskini hawawezi kusubiri”. Maneno yalimgusa Papa Francisko, na kwa huruma ya kibaba, alizungumzia matatizo makubwa yanayopambana na familia zisizo kuwa na makazi ya kudumu, akizifananisha na Familia Takatifu, ambamo Bwana Yesu alizaliwa katika hori la ng'ombe, na pia jinsi walivyolazimika kuondoka katika nchi yao na kukimbilia Misri.

Papa alieleza familia na nyumbani huenda pamoja , na hivyo alitoa wito kwa kila mmoja , watu binafsi, vyombo vya kijamii na mamlaka, kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kwamba kila familia ina mahali pa kuishi yaani nyumbani.

Kabla ya kusali sala kwa heshima ya Mama Bikira Maria , Baba Mtakatifu alitafakari kwa ufupi, Injili ya siku, sura ya kwanza ya Injili Mtakatifu Mathayo ambamo mna elezea matukio ya kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, katika maoni ya Mtakatifu Yoseph, mchumba wa Bikira Maria.

Papa Francis alisema, maelezo hayo, yanatuonyesha umuhimu na kina cha matukio yaliyotokea , ambamo Yosefu, anapata taarifa za Maria kuwa mja mzito, na anaamua kumwacha kwa siri , kabla ya kuitoa nafsi yake yote katika mapenzi na maongozi ya Mungu. Papa alisema, hili linatuonyesha ukuu wa Roho ya Mtakatifu Yosefu, kuwa alikuwa ni mtu muelewa, ambaye daima aliisikiliza sauti ya Mungu. Na alikuwa mtu mwenye kujali masuala yake ya siri , alikuwa mtu makini katika kusikiliza ujumbe toka moyo na kutoka juu.

Baba Mtakatifu alihitimisha maelezo yake kwa kuhimiza waamini wote wafurahie Siku Kuu ya Noel kwa kumtafakari Maria na Yosefu. Maria aliyejaaa neema , mwanamke jasiri, aliye weka mategemeo yake yote kwa neno la Mungu ; na Yusuf, mwaminifu na mwenye haki ambaye aliisikiliza na kuamini sauti ya Bwana badala ya kusikiliza sauti za uzushi na kiburi cha binadamu. Pamoja nao, alisema , katika maandalizi ya siku hii sisi kutembea pamoja nao kuelekea Bethlehem.










All the contents on this site are copyrighted ©.