2013-12-21 09:09:54

Wanandoa watarajiwa kukutana na Papa Francisko, hapo tarehe 14 Februari 2014, Siku ya Wapendanao!


Agano la ndoa, ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya ya maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili ya mafao yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili kati ya wabatizwa, limeinuliwa na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti.

Umoja wa ndoa ya mume na mke hauvunjiki kwani kile alichounganisha Mungu mwanadamu hana ruhusa ya kukitenganisha! Sakramenti ya Ndoa ni ishara ya umoja wa Kristo na Kanisa lake. Inawapatia wanandoa neema ya kupendana kwa mapendo ambayo kwayo Kristo amelipenda Kanisa lake. Neema ya Sakramenti ya Ndoa hukamilisha mapendo ya kibinadamu kati ya mume na mke; huthibitisha umoja usiovunjika na kuwatakasa wanandoa katika safari ya uzima wa milele!

Ni kwa kutambua umuhimu wa ndoa na familia pamoja na changamoto zake katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuitisha Sinodi maalum ya Maaskofu itakayofanyika hapo Oktoba, 2014. Katika mchakato huu, Baba Mtakatifu Francisko, katika Siku kuu ya Mtakatifu Valentino, hapo tarehe 14 Februari 2014, Siku ya Wapendanao, atakutana na kuzungumza na wanandoa watarajiwa mjini Vatican majira ya asubuhi.

Baraza la Kipapa la Familia linasema, walengwa ni wanandoa watarajiwa wanaoendelea kujiandaa kwa ajili ya kufunga ndoa ndani ya Kanisa. Kwa wale wanaotaka kushiriki tukio hili la aina yake katika historia ya Kanisa, wanaalikwa kuwasiliana na Idara ya familia katika Parokia, Majimbo na Mabaraza ya Maaskofu au katika vyama vya kitume kwa ajili ya ndoa na familia. Kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaweza kuwasiliana moja kwa moja na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Familia kwa anuani ifuatayo: events@family.va

Baba Mtakatifu Francisko mara kadhaa amewataka wanandoa kuendelea kuishi ile furaha ya ndoa kwa kukazia uaminifu na mapendo, daima wakisaidiana katika mchakato wa utakatifu wa maisha, huku wakijitahidi kuiga Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu; kwa kupokea na kukumbatia Injili ya Uhai, kila mtu akijitahidi kujisadakisha kwa ajili ya mwenzi wake wa ndoa.

Wanandoa watarajiwa wanakumbushwa kwamba, ndoa ya Kikristo ni Wito Mtakatifu na Sakramenti kama ilivyo kwa wito wa Kipadre na Kitawa. Wanandoa kwa upendo na uthabiti wa moyo wanaamua kuwa mwili mmoja na roho moja katika safari ya maisha yao yote, hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Sakramenti ya Ndoa inafumbata zawadi hii inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Wanandoa wanaalikwa kusaidiana ili kuweza kukabili "majanga" ya maisha ya ndoa na familia.








All the contents on this site are copyrighted ©.