Tekelezeni dhamana na utumishi wenu kwa kuzingatia: weledi, huduma na utakatifu wa
maisha!
Majilio ni kipindi ambacho kina utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na viashiria vya
kiliturujia vinavyowaandaa waamini kuadhimisha Fumbo la Umwilisho, kielelezo makini
cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu
wake kwa ajili ya huduma kwa Kanisa; huduma ambayo inafanywa kwa majitoleo makubwa;
kwa kuzingatia kipaji cha ugunduzi; kwa kusikiliza na kusikilizana; kwa kujadili na
kuheshimiana.
Hizi ni salam na matashi mema ya Noeli kutoka kwa Baba Mtakatifu
Francisko alipokutana na wasaidizi wake wa karibu, siku ya Jumamosi, tarehe 21 Desemba
2013. Anawaalika kuendelea kusali na kumwombea Askofu mkuu Pietro Parolin aliyeanza
kutekeleza utume wake hivi karibuni kama Katibu mkuu wa Vatican. Anawatakia kheri
na baraka wale wote wanaohitimisha huduma na utume wao mjini Vatican tayari kuanza
maisha ya pensheni ya uzee, ili kupata muda zaidi wa kusali na kuwahudumia waamini
watakaokutana nao!
Baba Mtakatifu anawapongeza viongozi vijana wanaoendelea
kutekeleza dhamana na utume wao kwa Kanisa la kiulimwengu kwa kufuata mifano bora
ya "Wazee wa Kanisa". Hawa ni vijana wanaofanya kazi kwa ari na moyo mkuu; kwa weledi
na umakini wa ajabu, daima wakijitahidi kutekeleza wajibu wao wa kila siku. Baba Mtakatifu
anasema, angependa kuwataja kwa majina, lakini anaogopa kwamba, anaweza kusahau wengine
na hivyo kushindwa kuwatendea haki na mapendo. Viongozi hawa ni mashahidi muhimu sana
katika hija inayotekelezwa na Mama Kanisa.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake
anakazia umuhimu wa kutekeleza wajibu si kwa sababu ya ukuu wa kitengo alichokabidhiwa
mtu, bali huduma inayozingatia weledi kwa kujikita katika utekelezaji makini wa majukumu,
kusoma na kujiendeleza zaidi na zaidi kwani elimu haina mwisho. Hii ni sifa muhimu
sana kwa wafanyakazi wa Vatican, jambo linalohitaji msingi thabiti.
Baba Mtakatifu
anasema, sifa kuu nyingine ni huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu, Kanisa
la kiulimwengu na kwa ajili ya Makanisa mahalia yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia.
Kwa wale wanaofanya kazi mjini Vatican wanapaswa kuhisi hali hii badala ya kufanya
kazi kwa mazoea, bila kuweka chachu ya maisha yenye mwono na mwelekeo mpana zaidi.
Bila kuwa na sifa hizi, wafanyakazi wa Vatican wanakuwa ni mzigo mkubwa wa urasimu
usioweza kubebeka; wanageuka na kuwa ni wapelelezi na wachunguzi; watu wasiotoa nafasi
kwa Roho Mtakatifu wala ukuaji wa Watu wa Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, sifa
nyingine kwa wafanyakazi wa Vatican inajikita katika utakatifu wa maisha, moja ya
tunu msingi katika maisha ya Kikristo; ubora na huduma. Utakatifu unaonesha ile hali
ya mtu kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu; akiwa na moyo wazi kwa ajili ya Mungu;
ni hali inayomwezesha mtu kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu kwa njia ya
Sala; unyenyekevu wa ndani, daima akijitahidi kuwa karibu zaidi na Watu wa Mungu.
Hii ni sifa muhimu sana kwa kila Padre.
Baba Mtakatifu anasema, utakatifu wa
maisha unaongozwa na dhamiri nyofu ili kufuata ukweli badala ya kukumbatia "maneno
ya mitaani au uzushi". Dhamiri nyofu inapaswa kufanyiwa kazi katika uhalisia wa maisha
na wala isibaki kuwa ni nadharia tu! Baba Mtakatifu anasema, uzushi unaharibu ubora
na sifa ya mtu; unaharibu kazi na mazingira.
Baba Mtakatifu anawaalika wasaidizi
wake wa karibu katika hotuba ya matashi mema kwa Siku kuu ya Noeli kumtafakari Mtakatifu
Yosefu, mtu wa haki; mkimya na muhimu sana, aliyekuwa bega kwa bega na Bikira Maria
katika hija ya maisha yake hapa duniani; akasimama kidete kutoa ulinzi na tunza kwa
Mtoto Yesu. Mtakatifu Yosefu ni mfano wa huduma kwa Kanisa. Baba Mtakatifu anawashukuru
kwa kazi, lakini zaidi kwa sala wanazoendelea kutolea kwa ajili ya maisha na utume
wake; hata Yeye anawakumbuka katika sala zake.