Askofu mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 19 Desemba 2013 ameadhimisha
Ibada ya Misa takatifu kama kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Korea ilipoanzisa uhusiano
wa Kidiplomasia na Vatican. Katika mahubiri yake Askofu mkuu Parolin amekazia umuhimu
wa Korea ya Kusini na Kaskazini kuheshimu haki msingi za binadamu na kuanza mchakato
wa majadiliano ya kina yatakayowezesha pande hizi mbili kuzika tofauti zao za kisiasa
na kuanza kujenga mshikamano wa kitaifa kwa kutambua kwamba, wao ni ndugu wamoja!
Waendelee
kusaidiana katika kukabiliana baa la njaa na ukame unaotishia maisha ya mamillioni
ya watu badala ya kuelemewa mno na kinzani za kisiasa zinazotishia amani na utulivu
miongoni mwa wananchi wa Korea. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kikanisa cha Chuo cha
Korea kilichoko mjini Roma na kuhudhuriwa na viongozi kutoka katika ubalozi wa Korea
mjini Vatican.
Askofu mkuu Parolin amepongeza jitihada zinazofanywa na Kanisa
Katoliki nchini Korea kwa kudumisha mshikamano wa kichungaji kati ya Makleri na Waamini
walei ili kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwa kuyatakatifuza malimwengu,
kwa kuzingatia Neno la Mungu, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii
ya Kanisa Katoliki. Waamini walei nchini Korea wamekuwa mstari wa mbele katika kushuhudia
imani yao kwa Kristo na Kanisa lake ndani na nje ya Korea yenyewe, jambo ambalo linapaswa
kuigwa!
Jumuiya ya Kikristo nchini Korea, imekuwa na kukomaa taratibu na katika
hali ya ukimya licha ya madhulumu na nyanyaso za kidini walizokuwa wanatendewa; hawa
wakawa ni ile mbegu iliyoanguka ardhini na kuzaa matunda mengi. Damu ya mashahidi
kutoka Korea imekuwa ni mbegu ya kukua na kukomaa kwa Ukristo nchini humo. Leo hii
kuna jumla ya waamini wa Kanisa Katoliki wapatao millioni tano waliogawanyika katika
Majimbo kumi na tisa na kwa sasa Kanisa linaendelea kucharuka katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya.
Askofu mkuu Parolin anasema, katika kipindi cha miaka 75 iliyopita,
uhuru wa kidini umechangia kwa kiasi kikubwa kukua na kupanuka kwa Kanisa nchini Korea,
kiasi kwamba, Kanisa limeendelea kuwa ni mdau mkuu katika kuchagia ustawi na maendeleo
ya wananchi wa Korea.
Amewasihi waamini kuendelea kuombea haki, amani, upendo,
mshikamano na upatanisho wa kitaifa, ili siku moja, Korea zilizogawanyika ziweze tena
kujisikia kuwa ni taifa moja. Injili iwe ni chachu ya upendo, matumaini na furaha
ya kweli, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu!