Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amebariki maamuzi ya wabunge na kutengua nyadhifa
za mawaziri wanne wa Baraza la Mawaziri kufuatia kashfa ya Operesheni Tokomeza Majangili
na Operesheni Kimbunga. Hii ni mara ya tatu kwa Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya
Kikwete kujiuzulu kufuatia kashfa mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2008 – 2013.
Uamuzi
wa kujiuzulu kwa mawaziri hao ulitangazwa jana Bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
baada ya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, kusimama bungeni na kutangaza mwenyewe
kujiuzulu na kufuatiliwa na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo,
ambaye pamoja na kutakiwa na wabunge ajiuzulu, aligoma kutangaza uamuzi huo.
Rais
Kikwete alitoa uamuzi huo akiwa nchini Marekani kwa matibabu baada ya Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda kumpelekea maoni yaliyotolewa na wabunge. Waliowajibishwa ni Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David, Waziri wa Maliasili na Utalii,
Balozi Khamis Kagasheki , Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emmanuel Nchimbi na Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Hata hivyo, Dk. Nchimbi
na Waziri wa Ulinzi, Nahodha, hawakuwepo ukumbini , wakati uamuzi huo ukitolewa. Hatua
ya Rais ilitangazwa Ijumaa saa 2:30 usiku bungeni na Waziri Mkuu Pinda , aliyekuwa
anatoa msimamo wa serikali kuhusiana na hoja hiyo ya kuwawajibisha kutokana na uovu
uliofanywa na watekelezaji wa operesheni hiyo uliosababisha mauaji ya watu 19.
Waziri
Mkuu ambaye naye alitakiwa na wabunge kujiuzulu hakuwa tayari kujizungumzia wala kujibu
hoja zilizomtuhumu. Alisisitiza kuwa operesheni hiyo imesimamiwa na wizara tatu za
Maliasili na Utalii, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mambo ya Ndani hivyo awali
alizungumza na mawaziri wote wanne na kukubalina kuwa katika mazingira hayo na kauli
za wabunge walizoshauri wachukulie kwa msingi kuwa ni busara wakubali ushauri wa Bunge
wakukubali kuwajibika.
“Waheshimiwa wote wanne wamekubali kujiuzulu na kilichofanya
walikubali kufanya hivyo ni kwamba vyombo vilivyohusika viko chini ya usimamizi wao.”
DK.
MATHAYO Akizungumzia Dk. Mathayo alisema kwa maana ya operesheni tokomeza ni vigumu
kusema kuwa alihusika moja kwa moja kwani hakuwa na vyombo vilivyosimamia operesheni
hiyo na kwamba hakuhusika na vitendo vilivyojitokeza . Lakini kwa msingi huo alitakiwa
kujiuzulu kwa kuwa anasimamia Wizara ya Mifugo na ambayo inaweza kuchukuliwa kuwa
alishindwa kusimamia mifugo ambayo imeingia kwenye hifadhi. “Nilimueleza kuhusu Mathayo
kuwa anaweza asihusike moja kwa moja na operesheni tokomeza lakini pengine aangaliwe
kama yeye ni msimamizi wa mifugo. Hii inaweza kuchukuliwa kuwa ndiyo maana ameshindwa
kusimamia mifugo inayoingia kwenye hifadhi za taifa”. Alichosema hapana ni kwamba
hakuna haja ya kugombana kwenye jambo hilo ambalo ni kubwa hivyo si vibaya na yeye
akaliona kwa mtizamo huo na kujiuzulu kama wengine.
TUME
Akizungumzia
kuhusu kuundwa kwa tume aliongea na Rais na hilo ameliunga mkono na kushauri tume
iundwe na matokeo yake yapatikane kwa muda mfupi ili watendaji wote waliohusika bila
kujali ni wa ngazi gani au taasisi gani wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu.
RIPOTI
Akiizungumzia matukio yaliyoibuliwa na kamati hiyo ya unyanyasaji, udhalilishaji
na mauaji ya watu na mifugo haukubaliki na serikali itachukua hatua. Na kusisitiza
kuwa kikwazo kikubwa ni namna operesheni iliyotekelezwa na kusimamiwa. Aliwataka mawaziri
hao waone kuwa ni sehemu ya jukumu lao na anakubaliana na wabunge wanaotaka mawaziri
wabebe lawama kwa hiari yao wenyewe. Nimejaribu kutizama maelezo yaliyotolewa taarifa
hizo zinahitaji kuthibitishwa zaidi. Ushauri wa Mwanasheria umezingatia zitakuwepo
hatua za kiutawala na za kisheria.
Kuna uvunjifu mkubwa wa sheria na kunahitajika
tume ya kimahakama kuwachunguza ili wahusika washughulikiwe, naamini muda mfupi kadri
ya mwezi mmoja tupate taarifa ya uchunguzi na hatua kwa kila mmoja zichukuliwe. Hata
hivyo alisisitiza umuhimu wa kutunza mali asili hasa wanyama pori akieleza kuwa sensa
inaonyesha kuwa katika hifadhi ya Selous kulikuwa na 55,000 lakini sawa wamebakia
tembo 13,000.
WAZIRI KAGASHEKI AIBUKA SHUJAA Akitoa maelezo ya kujiuzulu
bungeni Balozi Kagasheki alisema “mimi ni mtu mzima nimesikia hisia na sauti za wabunge
na mimi nasema .. Mheshimwa Rais Dk. Jakaya Kikwete, aliponiteua ilikuwa ni katika
furaha yake naamini kabisa aliniamini kuwa ningeweza kufanya kazi kama alivyotegemea”
“Lakini kutokana na operesheni hii kuna mabaya yametokea naamini uchunguzi utafanyika
kuwafahamu waliohusika….niombe tu nimeseme kuwa mimi mwenyewe nimewasikia kwa kauli
yangu natamka wazi kuwa ni nia yangu kushuka ngazi hii ya uwaziri, ninajiuzulu.”
Alisema
na kushangiliwa na Bunge na kuahidi kuwa atachukua hatua ya kuzitaarifu mamlaka zilizompa
jukumu hilo.
Mathayo ‘ninaonewa’Alilalamika kuwa anahukumiwa kuwa mtuhumiwa
bila kuhojiwa. Alisema ripoti nzima haikutaja kuwa amehusika na operesheni tokomeza
na kuongeza kuwa hakuitwa kuhojiwa na kamati na kwamba hajawahi kuona mahakama inayomhukumu
mshitakiwa bila kumhoji. Alisisitiza kuwa ameonewa na Mungu mwenyewe atawashughulikia
hao wanaotaka ang’oke na kwamba alikuwa anasali zaburi ya 72.
Aliiponda ripoti
hiyo ya kamati kwa kutoa taarifa za uongo kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa mifugo
lakini haina sera na mipango ya muda mrefu ya kuendeleza mifugo. Alisema sera ipo
na ilipitishwa na Bunge mwaka 2006 na pia kuna mipango ya muda mrefu na mfupi ya kuendeleza
mifugo. “Kwangu haingii akilini mimi kuambiwa sina sera sina mipango , alisema na
kujitetea kuwa matatizo ya sekta ya mifugo ni ya kitaasisi”.