2013-12-21 13:07:12

Maisha Mchanganyiko: Nani kama Mama!


Zikiwa zimebaki siku tatu, kuadhimisha tukio la Mama Bikira Maria kutuzalia Mtoto Yesu , Emannuel, Mkombozi wa Dunia, inafaa kwa wakati huu kumtafakari Mwanamke, mama mzazi, hadhi yake, wajibu wake na Kanisa lasema nini juu mwanamke mama mzazi.
Ni wazi kipindi cha Krismas, ni wakati wa hekaheka nyingi za katika jamii , na familia pia. Nyuso nyingi huonekana kuwa na furaha, na pia ndani ya familia, huonekana mshikamano zaidi, ambamo licha ya hamu ya kusubiri ibada ya kusisimua ya Mkesha wa Noel, pia kihali kuna mengi yanayofanyika. Baba anawazia familia watavaa nini na familia itasheheka vipi, wakati mama nae akilini mwake amememezwa na mahangaiko ya maandalizi ya mapochopocho ya mezani, na jinsi gani atawezesha familia yake kupendeza siku hiyo, hata kama hawana fedha za kununua nguo mpya , bado atajitahidi zile walizo nazo kuziweka katika hali nzuri, atazifua na kuzipiga pasi na kweli wote watatoka katika hali ya utanashati. . Pongezi kwa hayo.
ili kuweza kushirikishana mawazo vyema katika kujadili mada hii ya Mama, na awaalika tuunganishe uchambuzi wetu na maoni yaliyo andikwa na Mwenye Heri Papa Yohane Paulo II, katika waraka wake juu ya Hadhi ya Mwanamke” Muliers Dignitatem ”.
Katika kipengere cha 18 cha waraka huo, alisema, ”ili tuweze kuelewa maana ya kuwa mama (motherhood), ni lazima kwanza zaidi ya yote , kujaribu kupata uelewa wa kina juu ya ukweli wa mtu binadamu kama ilivyotajwa katika Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican, kwamba Binadamu , awe mke au mme, ni kiumbe kilichoumbwa na Mungu kwa namna ya kipekee, kwa ajili yake Mwenyewe Mungu. Baba wa Milele aliyeumba ulimwengu kwa azimio la hiari na la siri, lenye hekima na wema , akamuinua binadamu hadi kumshirikisha uhai wake wa Kimungu. Na pindi wanadamu wanapoanguka na kumwasi, hawaachi kabisa bali huwapatia siku zote misaada ya wokovu kupitia imani kwa mwanae pekee Yesu Kristu, aliyemwilishwa na kuja kukaa kwetu, Yesu Kristu Mkombozi.

“Binadamu ni kiumbe pekeee aliyejaliwa utashi , wa kujiamulia mambo yake mwenyewe. Hata hivyo, pia binadamu huyu hawezi kujiona amekamilika bila ya kuwa karibu wa binadamu mwingine, kama ambavyo ufafanuzi huu wa mtu unavyokwenda sambamba na msingi wa ukweli wa Biblia, kuhusu uumbaji wa binadamu - mwanamume na mwanamke - katika sura na mfano wa Mungu . Hii si tafsiri ya kinadharia, wala kuwa kifungu cha maneno yaliyo nakiriwa kutoka mahali, lakini yanatoa maana halisi na kweli, maana ya kuwa binadamu , na wakati huohuo ikisisitiza thamani ya zawadi ya binafsi , zawadi ya utu wa mtu. Katika mtazamo huo wa mtu, tunaweza pia kupata kiini cha maadili ya jamii au taifa, “ ethos " ambayo kwa pamoja na ukweli wa uumbaji, unakamilishwa na kitabu cha agano jipya”..
Mwenye Heri Yohane Paulo II, anaendelea kufundisha kwamba, Ukweli huu juu ya mtu, pia unafungua njia ya ufahamu kamili wa umama wa mwanamke, kwamba umama ni matunda ya ndoa, muungano wa mwanamume na mwanamke, kama ilivyoelezwa katika kitabu cha Biblia kwamba muungano huu wa wawili watakuwa mwili mmoja " ( Gn 2:24). Na hili linaturejesha kumwona mwanamke kama sehemu zawadi ya binafsi maalum, na pia kama kielelezo cha upendo wa wawili wanaoungana na kuwa mwili mmoja , na kutimizwa yale yaliyoandikwa katika kitabu kitakatifu cha Biblia.

Zawadi hii ya pande mbili za watu kuungana na kuwa mtu mmoja kupitia sakramenti ya ndoa hufungua zawadi ya maisha mapya, binadamu mpya , yaani mtoto , ambaye ni nakala ya wa wazazi wake . Umama ina maana , tangu mwanzo wake ni majitoleo maalum kwa ajili ya kuleta mtu mpya. Ni majitolea ya wazi ya mwanamke mwenyewe. Katika uwazi huu wa mke na mme waliokuwa mwili mmoja , mimba hutungwa , na kuzaliwa mtoto. Na hapo mwanamke hugundua mwenyewe thamani hii ya zawadi binafsi ya majitoleo katika upendo wa kina.

Zawadi ya utayari wa ndani wa kumkubali mtoto na kumleta duniani,kupitia muungano wa ndoa. Kulingana na Biblia, kutunga mimba na kuzaa binadamu mpya , ni tukio la hali ya juu sana ambalo kama mwanamke alivyosema, Nimeleta binadamu mpya kwa msaada wa Bwana" (Mwa 4:01 ) Haya ni maneno ya Eva , Mama wa viumbe wote. Yanaonyesha furaha ya mwanamke na ufahamu wake wa kushiriki katika siri kubwa ya mwendelezo wa binadamu, kuendelea kuumbwa kizazi na kizazi, kupitia muungano wa ndoa , katika nguvu ya ubunifu wa Mungu !

Nani kama Mama ! Ni maneno yanayogusa mioyo ya watu wote duniani, katika kumzungumzia mama mzazi. Pamoja na hali ya mwanamke katika kipindi cha kati ya mimba na mtoto kuzaliwa katika njia ya kawaida , kimwili na kisaikolojia humpitia mengi, ambayo kwa wakati huu yanaeleweka vyema zaidi kisayansi kuliko ilivyokuwa siku za nyuma, uchambuzi yakinifu wa kisayansi unathibitisha kwamba , mwanamke ameumbwa na asili ya kuwa mama. Na hivyo kutunga mimba kama matokeo ya muungano wa ndoa na mtu mme, huenda sambamba na muundo wa kisaikolojia na mwili wa mwanawake . Watafiti waliofanya uchunguzi juu ya ukweli hu, wanathibitisha kwa kusema, ebu waweke watoto wadogo mchanganyiko wa kike na kiume pamoja , wape vitu mbalimbali vya kuchezea, utaona kwamba watoto wa kike wanapendelea kuchezea vitu vya kimama zaidi kuliko watoto wa kiume, ikionyesha asili ya umama kwa mwanamke.

Mwenye Heri Yohane Paulo II katika waraka wake wa Mulieris dignitatem, anasema, "umama ni mahusiano maalum ya muungano katika fumbo la maisha yanayoanza na kukua ndani ya tumbo la mwanamke . Mama wakati wa kulea mimba, hujawa na fikira nyingi na mshangao wa kile kinachoendelea ndani mwake, na katika mwanga wa matumaini ya kutoa maisha mpya duniani, hukubali na kumpenda mtoto anayembeba ndani mwake kwa kipindi cha meizi tisa. Haya ni mapenzi ya ajabu na ya kipekee".
Ingawa wanaume pia hushiriki kwa namna moja au nyingine, katika kulea mimba, , wanasaikolojia wanasema zaidi sana kwa mama ambaye katika kipindi hiki hujifunza mengi katika kumjali binadamu mwingine, ambaye hata hajamwona kwa macho yake na hivyo huunda moyo huu wa kimama.
Na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican , ukitazama ushiriki wa mwanamke katika ukombozi wa binadamu umeandika kwamba , Mungu wa huruma alitaka Umwilisho utanguliwe na ukubali wake yeye aliyeteuliwa tangu milele awe mama , ili kama mwanamke alivyoshiriki kuileta mauti pia kadhalika asaidie kuuleta uzima.

Hayo yamhusu kwa namna ya pekee Mama wa Yesu aliyeuzalia ulimwengu uzima wenyewe. Hivyo Maria , kwa kulikubali Neno la Mungu amekuwa mama wa Yesu. Bikira Maria kwa kipaji na dhima ya umama wa kimungu unamwunganisha na mwanaye Mkombozi, na kwa neema zake na huduma za kipekee ameunganika pia katika undani wa Kanisa. Mama wa Mungu anakuwa ni kielelezo cha Kanisa katika imani , mapendo na umoja kamili na Kristo.

Na hivyo , Kanisa Katoliki , limeitolea tarehe Mosi Januari kila mwaka kuwa siku ya kumuenzi Mama wa Mungu, ambayo pia ni Siku ya Kuombea amani duniani.

Kijamii pia, huadhimishwa Siku ya Mama, katika tarehe mbalimbali , mbayo husherehekewa kwa heshima ya akina mama na kutoa shukrani kwao kwa kuvumilia shida na taabu wanazo pambana nazo katika kulea mtoto. Historia ya maadhimisho ya Siku ya Mama, imetambuliwa kwa namna ya kipekee tangu enzi za zama za fahali za Ugriki ya kale na imedumu hadi leo hii. Na kwa sasa inasherehekwa kwa kishindo katika mataifa zaidi ya 40 duniani kote.

Mfano nchini Marekani, Azimio la kuwa Siku ya kumuenzi Mama lilitiwa saini na Rais wa Marekani Woodrow Wilson Mei 8, 1914, kuheshimu akina mama na wanawake wajawazito, na ushawishi wa akina mama katika jamii. Ni siku ya kumtafakati Mama mwalimu wa kwanza wa binadamu. Afrika Kusini Siku ya Mama husherehekewa kitaifa kila Jumapili ya pèili ya mwezi Mei. Na huiadhmisha Siku hii kaika roho wa kweli anayeonyesha kutambua umuhimu wa mama ktika maisha yakilamtoto na hivyo ni siku ya kumshukuru mama kwa upendo wao usiokua na kipimo na kwa huduma yao zuri ya siku zote katika maisha ya mtoto, hata kama mtoto amekuwa mtu mzima, mama ni mama , wala hakuna wa kulingana nae.

Imeandaliwa na T.J, Mhella.







All the contents on this site are copyrighted ©.