Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa
na mahangaiko ya watu wanaoteseka na baa la njaa sehemu mbali mbali za dunia kwa kusema
kwamba, matumizi bora ya chakula yanaweza kusaidia kuganga njaa kwa mamillioni ya
watu, kuliko tabia ya sasa ya kuputa chakula, wakati ambapo kuna watu wanakufa kwa
njaa!
Huu ni ujumbe wa video uliotolewa na Baba Mtakatifu kwa ajili ya kundi
la watu wanaojihusisha na kukusanya kadi zilizotumika nchini Argentina. Anasema, hii
ni kazi nzuri inayosaidia kutunza mazingira na inaweza pia kuwa ni mfano bora hata
katika matumizi ya chakula! Kuna haja ya kubadili mitindo na mfumo wa maisha kwa kujenga
na kuimarisha mshikamano wa upendo, kuliko tabia ya utandawazi usiojali wala kuguswa
na mahangaiko ya jirani.
Tabia hii si tu kwamba, inajionesha katika vitu la
hasha! Baba Mtakatifu anasema imeanza kuingia hata katika utu wa mtu; kwani mtu anathaminiwa
tu pale anapozalisha na kutoa huduma, nje ya hapo si mali kitu! Watu wajifunze kuheshimu
na kutunza chakula kwa ajili ya mafao ya wengine pia!