2013-12-20 13:38:40

Jengeni utamaduni wa kukutana ili kuimarisha utamaduni wa upendo, umoja na mshikamano kati ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 20 Desemba 2013 amekutana na wafanyakazi wa kidiplomasia kutoka Italia na wale wa Vatican na kuwashukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya hata wakati mwingine katika hali ya unyenyekevu na kimya kikuu.

Baba Mtakatifu bado anakumbuka jinsi walivyojisadakisha tarehe 19 Machi 2013 alipokuwa anaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anawashukuru kwa ushirikiano wao na Sekretarieti ya Vatican pamoja na Nyumba ya Kipapa, kwa kuzingatia maadili na maisha ya kiroho wanapotekeleza wajibu wao.

Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi katika diplomasia kujenga na kuimarisha utamaduni wa kukutana na watu kutoka katika mataifa na mashirika mbali mbali ya kimataifa, ili kujenga na kuimarisha mahusiano chanya kwa kufahamiana, kuheshimiana daima wakishirikiana kutafuta njia za maendeleo na amani.

Baba Mtakatifu anawasihi wanadiplomasia kutoka Italia kuendeleza utamaduni wa amani kwa njia ya sanaa na makumbusho ya kitaifa ambayo ni urithi mkubwa nchini Italia. Siku kuu ya Noeli ambayo iko karibu sana ni fursa ya Mungu kukutana na binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anawatakia matashi mema ya Siku kuu ya Noeli, ili upendo wa Kristo uweze kugusa undani wa mioyo na maisha na huduma wanayoitoa kwa Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.