Jengeni urafiki wa dhati na Yesu ili kumtolea ushuhuda katika medani mbali mbali za
maisha!
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 20 Desemba 2013 amewashukuru wanachama wa
Umoja wa Vijana Wakatoliki Italia waliofika mjini Vatican kumtakia matashi mema ya
Noeli na kuwataka daima kuendelea kuwa ni mawe hai, hali wakiwa wameungana na Yesu
Kristo, rafiki na mwenza wa maisha!
Baba Mtakatifu amewakumbusha vijana hawa
kwamba, Noeli ni Siku kuu inayoonesha ujio wa Mungu kati ya watu wake ili kuwaokoa,
kama ilivyotokea mjini Bethlehemu takribani miaka elfu mbili iliyopita. Imani inamwezesha
mwamini kumtambua Mwana wa Mungu aliyezaliwa na Bikira Maria kama kielelezo cha upendo
wa Mungu kwa binadamu.
Yesu ni sura ya Mungu asiyeonekana; mwenye nguvu lakini
anajionesha katika hali ya mtoto mchanga, kielelezo cha ukarimu na upendo wa Mungu
kwa kila binadamu. Hii ndiyo sadaka inayofanywa na wazazi na walezi kwa ajili ya watoto
wadogo, wagonjwa na maskini.
Vijana hawa wamekumbushwa kwamba, wanapendwa
sana na Yesu anayetaka kujenga urafiki wa kudumu pamoja nao, ili hatimaye, waweze
kushirikisha furaha ya kukutana na Yesu katika medani mbali mbali za maisha; daima
wakiwa mstari wa mbele kuitolea ushuhuda kama Wakristo kweli wasiokuwa na mawaa!
Wawe
tayari kuwasaidia wale wanaohitaji msaada wao; bila kuhukumu wala kuwateta jirani
zao. Baba Mtakatifu, mwishoni, amewatakia hija njema ya kutembea wakiwa wameungana
na Yesu pamoja na Noeli njema kwa Mwaka 2013.