2013-12-19 09:38:40

Watoto wagonjwa kutoka Bambino Gesù wanasubiri kukutana na Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 21 Desemba 2013 anatarajiwa kutembelea na kuzungumza na watoto wanaotibiwa kwenye Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Hii ni kati ya Hospitali kubwa kuliko zote Barani Ulaya inayowahudumia watoto kutoka ndani na nje ya Italia.

Ni hospitali ambayo imeunganishwa na wataalam pamoja na watafiti wa kimataifa kuhusu magonjwa ya watoto na tiba zake. Hadi sasa kuna jumla ya wafanyakazi 2600 walioajiriwa hospitalini hapo. Hawa ni madaktari, wauguzi, watafiti, mafundi mitambo na wafanyakazi wa kawaida.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto millioni moja wanaotibiwa hospitalini hapo kwa ajili ya huduma za kawaida. Watoto 27, 000 walilazwa; watoto 25, 000 walifanyiwa upasuaji na watoto 71, 000 wamepata tiba kwenye kitengo cha dharura hospitalini hapo.

Historia ya Hospitali ya Bambino Gesù ilianzishwa kunako mwaka 1869 kama Hospitali ya kwanza kwa ajili ya watoto wagonjwa nchini Italia. Kunako mwaka 1924, wamiliki wa Hospitali hii wakatoa zawadi kwa Vatican na tangu wakati huo ikaanza kufahamika kama Hospitali ya Bambino Gesù, Hospitali ya Papa kwa ajili ya watoto wagonjwa.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea na kusalimiana na watoto wagonjwa, kama alivyowahi kufanya Papa Yohane wa Ishirini na tatu wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 1958. Baba Mtakatifu atakapowasili, atatembelea kwanza Kikanisa cha Hospitali ya Bambino Gesù na baadaye ataanza ziara ya kuwatembelea na kuzungumza na watoto waliolazwa Hospitalini hapo.

Baba Mtakatifu anapania kuhakikisha kwamba, anapata nafasi ya kuzungumza na watoto wengi zaidi. Wagonjwa, madaktari, ndugu na jamaa ya watoto wanasubiri kwa hamu kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, mtu wa watu!







All the contents on this site are copyrighted ©.