2013-12-19 07:56:14

Mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu


Kanisa ni mdau mkubwa katika mapambano dhidi ya biashara ya utumwa mamboleo, hii ni kutokana na dhamana yake ya kimaadili na maisha ya kiroho. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia umesheheni vielelezo vingi vya utumwa mamboleo vinavyoendelea kunyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. RealAudioMP3

Kati ya mambo haya ni: biashara haramu ya ngono inayowatumbukiza wanawake, wasichana na watoto katika vitendo vinavyokwenda dhidi ya utu na heshima ya mwanadamu. Kuna mwelekeo wa kuongezeka kwa biashara haramu ya binadamu kwa ajili ya kutafuta viungo, jambo linalosadikiwa kwamba, kwa siku za usoni, linaweza hata kuzidi biashara haramu ya dawa za kulevya na silaha katika soko la kimataifa.

Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna mamillioni ya wagonjwa wanaoendelea kusubiri kupandikiziwa viungo, lakini bado hawajafanikiwa kwa njia halali. Jumuiya ya KImataifa kwa miaka mingi imelifanyia kazi suala hili, lakini kwa miaka ya hivi karibuni inaonekana kana kwamba, limepuuzwa, lakini madhara yake ni makubwa kwa watu wengi hasa kutoka katika nchi maskini zaidi duniani.

Kwa kutambua madhara yanayosababishwa na utumwa mamboleo, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni aliitisha mkutano wa wataalam kutoka katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, ili kwa pamoja waweze kukaa na kujadili kuhusu tatizo, changamoto na mbinu za kisayansi zinazoweza kutumika kupambana dhidi ya biashara hii haramu inayoenea kwa kasi ya ajabu; kwa kukazia haki msingi za binadamu, utu na heshima yake.

Baraza la Kipapa la Taasisi za Kisayansi kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Madaktari Wakatoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, walikusanyika hivi karibuni mjini Vatican ili kujadili kwa kina na mapana kuhusu tatizo, changamoto na fursa za kupambana na biashara haramu ya binadamu. Vitendo hivi ni uvunjaji wa haki msingi za binadamu na ni vitendo vya uhalifu wa kimataifa ambavyo havina budi kudhibitiwa kikamilifu.

Ushawishi wa Vatican katika maadili na maisha ya kiroho ni chachu itakayoiwezesha tena Jumuiya ya Kimataifa, Serikali na Vyama vya kiraia kusimama tena kidete kwa nguvu na ari mpya kuendeleza mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu. Baadhi ya wajumbe wa mkutano huu wanasema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kukabiliana barabara na soko la bidhaa na huduma zinazozalishwa kutokana na biashara haramu ya binadamu. Haya ni mapambano yanayowahusisha watu wote.

Sheria za kitaifa na kimataifa hazina budi kushika mkondo wake kwani hii ni biashara ambayo inawaingizia wahusika faida kubwa kiasi kwamba, kwa kutumia fedha chafu, watu hawa wamekuwa wakikwepa mkondo wa sheria na hivyo tatizo kuendelea kuwa ni gumu zaidi. Serikali zinapaswa kutambua kwamba, biashara ya ngono ambayo kwa baadhi ya nchi za Magharibi ni kitendo cha halali ina uhusiano mkubwa na biashara haramu ya binadamu.

Mataifa makubwa yakipania yanaweza kusaidia mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, lakini kwa bahati mbaya, nchi kama hizi zimekuwa zikiangalia biashara hii kwa jicho la makengeza. Pale ambapo sheria ni kali na zinatekelezwa, biashara haramu ya binadamu imepungua sana.

Wajumbe wamempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuyaona madhara ya biashara haramu ya binadamu na kuanza kuchukua hatua, jambo ambalo limevuta hisia kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kuna haja sasa kubainisha mikakati iliyochambuliwa na wadau mbali mbali, ili hatua makini ziweze kuchukuliwa dhidi ya biashara haramu ya binadamu duniani, inayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.








All the contents on this site are copyrighted ©.