Biashara haramu ya dawa za kulevya inavyoichafua sura ya Tanzania!
Dr. James Msekela Balozi wa Tanzania nchini Italia na Mwakilishi wa Tanzania kwenye
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu mjini Roma anasema, kwa masikitiko
lakini kwa ujasiri mkubwa kwamba Tanzania kwa siku za hivi karibuni imechafuka kwenye
ramani ya kimataifa kutokana na baadhi ya watanzania kujihusisha na biashara haramu
ya dawa za kulevya.
Dr. Msekela
ameyasema hayo hivi karibuni katika Maadhimisho ya Miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania mjini
Roma. Amewakumbusha viongozi wa kidini kwamba, wanayo dhamana ya kimaadili kuwasaidia
watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, kwa kuwaonesha njia mbadala
ya kutafuta maisha, hasa wanapokuwa ugenini. Njia za mkato zinawatumbukiza watu katika
majanga na maafa!
Anasema, inatia aibu na inakera sana, kumbe kuna haja kwa
watanzania wote katika ujumla wao,. kushirikiana kwa pamoja kupambana na biashara
pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Dr. Msekela amewasihi viongozi
wa kidini kuendelea kuiombea Tanzania hasa baada ya kupata uhuru, kwani uhuru ni kazi
na dhamana ambayo inapaswa kufanyiwa kazi. Uingereza ilimkabidhi Mwalimu J. K. Nyerere
nchi kwa vile waliamini kwamba, Nchi itakuwa kwenye mikono salama kutokana uadilifu,
umahiri, umakini, lakini zaidi kutokana Mwalimu kuwa ni Mchamungu.