2013-12-18 11:07:46

Watu wanalilia amani, utulivu na maendeleo Jamhuri ya Afrika ya kati


Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Kwa takribani miaka kumi, wananchi wameendelea kushuhudia mapinduzi ya kijeshi yakifanywa nchini humo, kiasi kwamba, mchakato wa amani umeendelea kuwa ni mgumu nchini humo.

Mashambulizi ya kijeshi, watu kuyakimbia makazi yao na wengine kuuwawa kikatili yamekuwa ni mambo ya kawaida sana nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, jambo ambalo ni kinyume cha matarajio na matumaini ya wengi. Wananchi wanajiandaa kwa Siku kuu ya Noeli, wengi wanajiuliza, Je, Noeli ya Mwaka huu, itakuwa ni fursa ya kuonja tena amani na utulivu? Au watu wataendelea kusikia milio ya bunduki na mizinga ikirindima katika viunga vyao? Wananchi wataendelea kuona Serikali halali zikipinduliwa kijeshi?

Haya ni maswali yasiyokuwa na majibu yanayoulizwa na Askofu Juan Josè Agguire wa Jimbo Katoliki la Bangassou, Jamhuri ya watu wa Afrika ya Kati, wakati wa sala na tafakari ya Novena iliyoanza tarehe 17 Desemba na inayotarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 25 Desemba 2013, kwa kumwomba Bwana wa Amani aweze kuwakirimia zawadi ya haki, amani na utulivu.

Askofu Juan Josè Agguire anabaainisha kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshikirisha mwanadamu pia. Wao wameamua kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia tena amani na utulivu nchini mwao, wamechoka na vita sasa wanataka amani, utulivu na maendeleo ya watu katika mchakato wa kupambana na ujinga, umaskini na maradhi. Wanataka kuona ukombozi wa mtu mzima: kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.