Noeli iwe ni siku kuu ya imani na matumaini; mapendo na amani pamoja na mshikamano
na maskini!
Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake, Jumatano, tarehe 18 Desemba 2013, amewakumbusha
waamini kwamba, siku hizi za mwisho mwisho za Kipindi cha Majilio ni mwaliko kwa waamini
kujiandaa kiroho ili kumpokea Yesu anayezaliwa tena katika maisha yao.
Baba
Mtakatifu anasema, Noeli ni Siku kuu ya furaha na matumaini kwa Mwenyezi Mungu ambaye
ameamua kuja na kuishi kati ya watu wake kwa njia ya Mwanaye wa Pekee, Yesu, Mungu
kweli na Mtu kweli. Mwenyezi Mungu ameonesha upendo na huruma yake kwa binadamu kwa
kuwa ni sehemu ya ulimwengu, licha ya kinzani, mateso na umaskini wake. Yesu ni Emmanueli
wa kweli, Yaani Mungu pamoja nasi. Hii ndiyo zawadi kubwa inayoletwa na upendo wa
Kimungu; upendo unaoponya na kuleta mabadiliko katika mioyo ya watu kwa kuondoa woga
na wasi wasi.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kufanya tafakari
ya furaha kuhusu Fumbo la Noeli, ili hatimaye kutambua kwamba, Mungu amejifanya sawa
na binadamu na kwamba, binadamu pia anachangamotishwa kujifanya sawa na Mungu: kwa
njia ya unyenyekevu na mshikamano na jirani zake, hususan maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, kwa kuwa makini ili kusikiliza na kuwatimizia shida zao.
Baba
Mtakatifu Francisko anawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika Kipindi
cha Noeli ya Mwaka huu, kumwomba Bikira Maria Mama wa Yesu na Mama ya Wakristo, kuwasaidia
kuiona ile sura ya Yesu Kristo, Mungu aliyefanyika mtu!
Anawaombea ili waweze
kuwa ni miali ya mwanga unaong'ara kutoka mjini Bethlehemu, ili kuleta furaha na amani;
imani na matumaini kwa watu wote. Mwanga wa Yesu Kristo Mkombozi uenee katika medani
mbali mbali za maisha ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema, ili watu washuhudie
huruma ya Baba wa mbinguni.
Baba Mtakatifu anawaambia waamini wakati wa Maadhimisho
ya Siku kuu ya Noeli, kuhakikisha kwamba, wanawakumbuka pia maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii; Watu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita na kinzani za Kijamii,
lakini kwa namna ya pekee watoto, ili wote hawa waonje uwepo endelevu wa Yesu katika
maisha yao