2013-12-18 08:23:27

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutambua: haki, utu na heshima ya wahamiaji


Jumuiya ya Kimataifa inapopanga mikakati ya maendeleo baada ya Mwaka 2015, haina budi kuhakikisha kwamba, haki msingi za wahamiaji zinaheshimiwa, kwani idadi yao kwa sasa imefikia watu millioni 232, sawa na kiasi cha asilimi 3.2% ya idadi ya watu duniani. RealAudioMP3

Jumuiya ya Kimataifa itambue: utu na heshima yao kama binadamu; karama na uwezo wao wa kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi zinazowapatia hifadhi na kule walikotoka.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kudhibiti sababu zinazowafanya watu kuhama au kuzikimbia nchi zao. Baadhi ya watu wanataka kuboresha hali ya maisha; wengine wanakimbia madhulumu na nyanyaso za kisiasa na kidini bila kusahau majanga asilia. Ni watu ambao wana mikakati ya kusaidia kuendeleza Familia zao, jambo ambalo wanalitekeleza kwa sadaka kubwa na kwamba, wanatamani haki zao msingi ziweze kutambuliwa ili kuchangia zaidi.

Ni mchango wa Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva wakati wa mkutano wa 103 wa Baraza la Kimataifa kuhusu wahamiaji, uliohitimsihwa hivi karibuni. Wahamiaji wanachangia kwa kiasi kikubwa ustawi na maendeleo ya nchi zao asilia na kule ambako wamebahatika kupata hifadhi. Ni kundi linachochangia pia katika mapambano dhidi ya umaskini duniani.

Takwimu zinaonesha kwamba, wahamiaji wanaingiza kiasi cha dolla za kimarekani billioni 550 katika nchi zilizoendelea duniani na kwamba, wanaingiza kiasi cha dolla za kimarekani millioni 414 kwa nchi changa duniani, kumbe, wahamiaji wakithaminiwa wanaweza kuchangia mchakato wa maendeleo ya watu wengi duniani. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinapewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati kuhusu wahamiaji.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anasema kwamba, watu wengi wanalazimika kuhama au kuzikimbia nchi zao kutokana na: vita na kinzani za kijamii, kisiasa na kidiini. Katika kipindi cha Mwaka 2012, inakadiriwa kwamba, watu zaidi ya millioni 72 walilazimika kuzihama au kuzikimbia nchi zao, jambo linalosababisha changamoto kubwa katika maisha na haki msingi za binadamu. Ni kundi la watu linalopoteza mawasiliano na familia zao, kumbe ni kundi linalopaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee na Jumuiya ya Kimataifa.

Inasikitisha kuona kwamba, zaidi ya watu 20, 000 kutoka Afrika walikufa maji baharini walipokuwa wanajaribu kuvuka Bahari ya Mediterrani kwenda Ulaya kutafuta hali nzuri zaidi ya maisha. Ni kundi la watu linalokimbia umaskini, njaa, vita na magonjwa. Kwa bahati mbaya wahamiaji na wakimbizi hawa wanaangukia katika mikono ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Hivi karibuni, wahamiaji 300 walikufa maji kwenye Visiwa vya Lampedusa, Kusini mwa Italia, kielelezo cha aibu ya Jumuiya ya Kimataifa inayoendelea kupuuzia kilio na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Ujumbe wa Vatican unakazia umuhimu wa kuheshimu na kulinda haki msingi za binadamu; kwa kuwathamini na kuwajali wakimbizi na wahamiaji kwanza kabisa kama binadamu, kwani wanalazimika kuzikimbia nchi zao kinyume cha utashi wao binafsi. Uhusiano kati ya haki na maendeleo unapaswa kuwa ni kiini cha majadiliano kati ya wahamiaji na maendeleo, kwani hili ni kundi linaloweza kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya nchi zao pamoja na nchi zinazotoa hifadhi.

Ujumbe wa Vatican unaunga mkono vita dhidi ya biashara haramu ya binadamu na kwamba, linaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuangalia kwa makini tatizo la watoto wahamiaji ambao hawaambatani na wazazi wala walezi wao, ili waweze kupata huduma msingi.








All the contents on this site are copyrighted ©.