2013-12-18 09:06:19

"Dumisheni haki na uhuru wa kuabudu; tafuteni mkakati kwa ajili ya maboresho ya sekta ya elimu nchini Tanzania"


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, Jumapili tarehe 15 Desemba 2013 aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kusherehekea Miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania. Ibada hii ilihudhuriwa na umati mkubwa wa Watanzania wanaosoma na kuishi mjini Roma, wakiongozwa na Dr. James Msekela, Balozi wa Tanzania nchini Italia na Mwakilishi wa kudumu kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko mjini Roma.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Rugambwa amewataka watanzania kumkimbilia Mwenyezi Mungu katika shida na mashaka yao; wawe na ujasiri wa kumshuhudia Kristo kwa njia ya maneno na matendo yao kwa kusimamia ukweli na haki. Ameombea Tanzania inapoendelea kucharuka katika maendeleo na uboreshaji wa miundo mbinu; ugunduzi wa gesiasilia na mchakato wa Katiba Mpya ya Tanzania. Anasema, Tanzania inapaswa kujikita zaidi na zaidi katika kudumisha misingi ya uhuru wa kuabudu, haki na amani.

Askofu mkuu Rugambwa amesikitishwa mno na kushuka kwa kiwango cha elimu nchini Tanzania, jambo ambalo linazua hofu kubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Tanzania kwa siku za usoni. Anasema, hii ni changamoto inayopaswa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka. Zaidi unaweza kuendelea kujitajirisha mwenyewe katika mahubiri yafuatayo:

Wapendwa katika Kristo,
Tumejumuika tena kwa furaha kuadhimisha pamoja Dominika ya tatu ya Majilio, ambayo kwa desturi hujulikana kama Dominika ya Furaha. Hivi ndivyo tunavyosoma katika antifona ya mwaliko: “Furahini siku zote nasema tena furahini. Furahini katika Bwana kwa kuwa yuko karibu” (Fil 4, 4-5). Hii ni Dominika inayokutwa katikati ya Majilio na sasa tunaanza kushuka kuelekea Noeli. Tunaelekea kwenye furaha kuu ya kukutana na Mwokozi Bwana wetu Yesu Kristo. Leo pia tunajumuika pamoja kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 52 ya Uhuru wa Nchi yetu. Tungependa katika tukio hili kumshukuru Mungu na kuzidi kuliombea Taifa letu.

Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu yuko karibu kutwaa mwili na kukaa kwetu. Neno la Mungu linatafsiri vema matumaini ya furaha wanayokuwa nayo waamini wanaoisubiri siku ya Bwana. Ili kuupatia nguvu mwaliko wa kumpokea Masiha, Nabii Isaya, katika somo la kwanza, anatusisitizia kusimama imara na kuwatia matumaini wale wanaoelekea kulegea.

“Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, fanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo msiogope”. Ni neno linaloonesha matumaini mapya ambayo yanapaswa kuwa furaha ya Taifa Teule. Kwa mara nyingine tena, Huruma ya Mungu inakuja kuwakomboa watu, maana hiyo ndiyo nguvu isiyoweza kushindwa na ndiyo nguvu inayoongoza safari ya kiroho ya wanadamu.

Katika Injili tunaongozwa kutafakari swali la Yohane Mbatizaji analolielekeza kwa Yesu na ushuhuda wa Yesu. Yohane hayuko tena Jangwani akipaaza sauti bali yuko mpweke kifungoni. Yohane ni sauti iliyozimwa kwa chuki ya watawala. Humo katika misukosuko ya gerezani imani yake inajaribiwa sana. Hata hivyo Yohane bado hajapoteza mwelekeo. Bado anaendelea kufuatilia habari za Yesu, bila shaka kupitia wanafunzi wake kama anavyodokeza Mwinjili Luka (7: 18). Habari anazosikia kuhusu Yesu zinamtia mashaka. Si Masiha aliyemtangaza. Si Masiha aliyeshika shoka tayari kukata mti usiozaa!

Hata hivyo mahangaiko ya Yohane yanamsukuma kuendelea kutafuta, ili athibitike katika ukweli. Hataki kuamini hisia zake tu, bali anataka kusikia “neno” kutoka kwa Yesu aliye “Neno wa Mungu”. Yohane alikuwa hawaandai tu watu kutengeneza njia ya Bwana ili waweze kukutana na Masiha, bali yeye mwenyewe anatembea katika njia hiyo wa kwanza. Yohane Mbatizaji anawatuma wanafunzi wake waende kumuuliza Yesu kama yeye ndiye Masiha au wamtazamie mwingine.

Hata katika hali hii ya mashaka, Yohane Mbatizaji anabakia na nafasi yake ya kuwa mtangulizi wa Masiha. Yohane anafanya kile ambacho amekuwa akifanya, kile ambacho sisi sote tunaalikwa kufanya: kumtazama Masiha, kumtafuta Masiha na kuwaelekeza watu kwa Masiha. Kutafuta majibu ya mashaka yetu kutoka kwa Kristo mwenyewe. Yohane anasahau kifungo chake cha kimwili na wasiwasi wake sasa ni kuufungua moyo wake ili aweze kupata habari juu ya Masiha. Hakutaka kuendelea kubaki katika kifungo cha mtazamo wake wa awali juu ya Masiha kama inavyoelezwa katika sehemu ya Injili inayotangulia simulizi la leo, (Mt. 3:1-12).

Yohane Mbatizaji anaonesha ujasiri wa kuweka wazi mbele ya Yesu mashaka yake na kuwa tayari kuelekezwa naye. Mt. Ambrose anatukumbusha juu ya ukweli huo pale anaposema, “Tuna kila kitu katika Kristo. Kila kitu ni Kristo kwetu sisi. Kama unataka kutibu madonda yako, Yeye ni mganga. Kama umechemka kwa homa, Yeye ni chemchemi ya maji hai. Kama umekandamizwa na uovu, Yeye ni haki. Kama unahitaji msaada, yeye ni nguvu. Kama unaitamani mbingu, Yeye ni njia. Kama unakimbia giza, Yeye ni mwanga”. Kwa maneno mengine, tumgeukie Kristo daima na katika kila jambo.

“Ni wewe?” Hili ni swali la msingi kwa kila anayemwamini Kristo. Tendo la imani ni tendo endelevu na swali hili, kwa yule anayemtafuta kwa dhati, halikomi. Ni swali linalomsaidia mtu kuongoza matendo yake na namna yake ya kukabiliana na hali na mazingira mbalimbali kwa kutumia hekima ya kimungu. Hata hivyo jambo la muhimu zaidi ni jibu ambalo Yesu anawapatia wanafunzi wa Yohane. Hasemi moja kwa moja kuwa “ni mimi”.

Badala yake anafanya rejea ya unabii juu yake, kama nabii Isaya alivyoagua: “... Mungu, atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, masikio ya viziwi yatazibuliwa ... kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wa aliye bubu utaimba... Nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia”. Hayo yanatimia mbele ya macho ya wanafunzi waliotumwa na Yohane Mbatizaji kuleta kwa Yesu ujumbe wa mashaka aliyokuwa nayo. Yesu anawatuma warudi kwa Yohane na kumsimulia Yohane yale “walioyasikia na kuyaona”.

Kuyaishi yale tunayoyasikia na kuyaona yakitendwa na Mungu ndiyo siri ya Ufalme wa Mungu. Huu ni Ufalme unaojengwa juu ya msingi wa unyenyekevu na udogo. Ni ajabu sana kwamba, katika hali aliyokuwa nayo Yohane, Yesu hatoki na kwenda gerezani kumfungulia Yohane minyororo ya kifungo cha mwili. Yesu anamfungua Yohane kifungo cha imani na anausifu ujasiri wa mtangulizi wake ambaye daima amebaki akiwa amemkazia yeye macho na kumtafuta yeye bila kuchoka hata alipokuwa gerezani. Yesu anaimba masifu juu ya Yohane. Yesu anamsifia Yohane aliye gerezani.

Huko Yohane Mbatizaji anamtukuza Mungu kwa maisha ya ushuhuda wa imani. Yesu mwenyewe alizaliwa na kuishi na kufa katika hali duni anawaambia watu ukuu wa Yohane uko katika unyenyekevu wake na ujasiri wake wa kumshuhudia Kristo kwa matendo yake. Na yeyote atakaye dhubutu kumfuata katika njia hiyo atakuwa mkuu kuliko hata Yohane. Hiyo ni ahadi ya Kristo mwenyewe. Hiyo ni changamoto ya maisha yetu ya kikristo.

Katika adhimisho la leo, tunapata fursa pia ya kuliombea taifa letu ambalo limetimiza miaka 52 ya Uhuru. Hii ni safari ndefu, yenye changamoto nyingi na tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa mema aliyolijalia Taifa letu katika kipindi hiki chote na pia kutafakari mustakabali wa Taifa letu. Toka tulipofanya adhimisho la namna hii mwaka jana tunashuhudia hatua mbalimbali za maendeleo ambazo Taifa letu limepiga. Serikali imeendelea kuimarisha miundo mbinu ya barabara na umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

Ugunduzi wa gesi asilia katika mikoa ya kusini mwa Tanzania inatupatia matumaini ya siku njema zijazo kama wahusika watakuwa makini katika kuunda mazingira yatakayo kuwa na tija na manufaa kwa Taifa letu. Mchakato wa kuandaa Katiba mpya, pamoja na mapungufu ya hapa na pale, unaendelea.

Hatuna budi kuipongeza serikali yetu pale inapofanya vizuri katika utendeji. Lakini tunawajibu pia wa kuikumbusha na kuishauri serikali pale ambapo katika maeneo mengi hali haiendi vizuri. Huu ni wajibu wa kizalendo na kila Mtanzania anayelitakia mema Taifa lake anapaswa kuwa sehemu ya ufumbuzi wa matatizo haya.

Hali ya amani ya Taifa letu imekuwa si imara sana. Yameendelea kujitokeza matumizi ya nguvu inayopitiliza ya mkono wa dola. Hapa na pale usalama wa watu na mali zao umeteteleka. Lakini pia mahusiano katika dini moja na nyingine si mazuri sana. Mihadhara ya dini moja kukashfu dini nyingine yameendelea. Bado imo katika kumbukumbu zetu matukio ya kutisha yaliyolikumba Kanisa la Zanzibar. Padri Mkenda aliponea chupuchupu baada ya kupigwa risasi, Padri Evarist Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi na Padri Anselm Mwang’amba alimwagiwa tindikali. Tuzidi kumwomba Mungu atujalie kuthamini amani, ambayo inajengwa kwa kuheshimiana na katika msingi wa haki ya mtu kuabudu atakavyo. Tuzidi kuliombea Kanisa la Zanzibar linalopita katika kipindi cha majaribu makubwa. Tumwombe Mfalme wa Amani aliyezaliwa duniani aziangaze nyoyo za wanadamu wote kwa mwanga wa amani.

Jambo jingine ambalo ningependa tulitafakari ni kuendelea kushuhudia kwa masikitiko hali mbaya ya kuporomoka kwa elimu nchini mwetu. Matokeo ua ufaulu kwa kidato cha nne, kwa mfano, yamekuwa yakishuka mwaka hadi mwaka. Tokea mwaka 2005 ufaulu umeshuka toka 89.12% hadi kufikia 34.5% mwaka 2012.

Zipo sababu mbalimbali zinazochangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu Tanzania. Baadhi ya matatizo hayo ni pamoja na viwango duni vya walimu, uhaba wa waalimu (ingawa wahitimu wa elimu katika vyuo vikuu ni wengi sana ikilinganishwa na fani zingine), waalimu kukosa motisha, upungufu wa zana za kufundishia na kujifunzia pamoja na maslahi hafifu kwa walimu, wanasiasa kuingilia taaluma ya elimu kwa kufanya maamuzi pasipo kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa elimu, n.k.

Athari za kuporomoka kwa kiwango cha elimu Tanzania zinajidhihirisha kwa namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukosa uwezo wa kuliletea Taifa na wao wenyewe maendeleo, kukosa uwezo wa kujenga hoja kimantiki, kukosa uwezo wa kuchanganua mambo kwa ufasaha na mtu kushindwa kubadilika kimtazamo hasi aliokuwa nao. Tunapaswa kukumbuka kuwa adui ujinga anapotawala, maadui wengine kama maradhi na umasikini wanakua pamoja nae. Hali hii siyo changamoto bali tatizo kubwa ambalo Watanzania wote tunapaswa kulitafutia ufumbuzi.

Kwenu ninyi Watanzania mlioko masomoni na mnaofanya shughuli zingine huku ng’ambo, ninawahimiza mfahamu nafasi yenu katika kuijenga jamii na Kanisa la Tanzania. Mambo yasiyofaa yanayotokea nchini ni kwa sababu baadhi ya Watanzania wenzetu wamepuuza umuhimu wa kulitumikia Taifa na watu kwa uadilifu.

Itakuwa ni fedheha kwetu kama tukirudi nyumbani tutashindwa kuonesha tofauti ya uelewa na kutoa mchango uliotegemewa kutoka kwetu. Kumbukeni mmeletwa ili muandaliwe kuwa viongozi katika nafasi mbali mbali; za chini na hata za juu. Kipindi hiki cha maisha yenu huku ni kipindi kinacholenga kuwaandaa kuwa watu wa manufaa kwa Kanisa na Taifa, ili mpate kuwapelekea matumaini ya furaha wanakanisa na taifa kwa ujumla.

Kanisa lazima lishike mahala pake pa kuwa chombo cha kuleta matumaini na kufufua ari ya watu katika kila nyanja: kiroho, kiutu, kiakili na kimaendeleo. Kwa kweli ni kuleta hiyo furaha aliyotabiri Nabii Isaya akisema: “Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kurungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba. Na hao waliokumbolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua vitakimbia.” (Isa. 35: 6-10.)

Basi ninawaalika tuendelee kumkazia macho Kristo aliye Bwana na Mwokozi wetu. Tumualike aje na kukaa kati yetu daima. Tuombe atupe neema ya kuchota kwake faraja ile ambayo watu wanaitazamia kutoka kwa wale wote wanaomwamini Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo








All the contents on this site are copyrighted ©.