Vita dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo!
Wakristo nchini Ufilippini wameungana pamoja ili kusimama kidete kulinda na kutetea
utu na heshima ya binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu pamoja na kuonesha
mshikamano na wote wanaotendewa na mikasa hii.
Kikundi cha kiekumune kinachodhibiti
biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kinasema, kitaendelea kupambana kufa
na kupona na wote wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu, hadi pale itakapotokemezwa
miongoni mwa Jamii.
Hii ni vita ya muda mrefu inayohitaji ujasiri, ari na
moyo mkuu ili kufikia lengo. Majanga ya maisha, umaskini na ujinga wa watu ni kati
ya mambo yanayotumiwa na baadhi ya watu kuwatumbukiza wanawake, wasichana na watoto
katika biashara haramu ya binadamu, ambayo imeenea sana sehemu mbali mbali za dunia
na ni kati ya biashara ambazo kwa sasa zinashamiri kwenye soko la kimataifa.
Akizungumzia
kuhusu madhara ya biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo, Askofu msaidizi
Broderick Pabillo wa Jimbo kuu la Manila anasema kwamba, biashara hii ina madhara
makubwa, kumbe ni jukumu la watu wote wenye mapenzi mema kushirikiana na kuweka malengo
ya pamoja katika mapambano dhidi ya wafanyabiashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.
Viongozi
wa Makanisa hawana budi kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha
kwamba, lengo hili linafanikiwa, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi
za binadamu pamoja na kubainisha mikakati inayoweza kung'oa tatizo hili kuanzia kwenye
mizizi.
Mwishoni, wadau wawe ni mipango ya muda mfupi na mrefu katika kuwasaidia
waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kwa kuwajengea uwezo
wa kujitegemea na kuzitegemeza familia zao.