Shikamaneni na kusaidiana, kwani hakuna mtu anayeweza kujitosheleza mwenyewe!
Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari
ya Kipapa amewataka watanzania wanapoendelea kuadhimisha Miaka 52 ya Uhuru kukuza
na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, daima wakiwa mstari wa mbele kutafuta
mafao ya wengi. Waendelee kushikamana zaidi katika maisha ya sala na ibada; wawe tayari
kujisadakisha kwa ajili ya huduma kwa watanzania wenzao.
Askofu mkuu
Rugambwa ameyasema hayo Jumapili iliyopita, tarehe 15 Desemba 2013 wakati alipokuwa
anazungumza na watanzania mara baada ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Parokia ya Mama yetu wa La Sallete ambayo ni Parokia ya kitume aliyokabidhiwa Kardinali
Polycarp Pengo kadiri ya Mapokeo ya Kikardinali. Watanzania wanapokuwa nje ya nchi
waoneshe uzalendo kwa nchi na Kanisa lao.
Askofu mkuu Rugambwa amewakumbusha
watanzania kwamba, wanategemeana na hakuna mtu yeyote anayeweza kujidai kwamba, anajitosheleza,
kumbe anahitaji kuonjeshwa upendo kutoka kwa watanzania wenzake kwa njia ya mshikamano
wa dhati.
Amemshukuru Dr. James Msekela, Balozi wa Tanzania nchini Italia
pamoja na uongozi mzima wa ubalozi kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya watanzania
wanaosoma na kuishi Roma na Ubalozi. Amemwomba Balozi kuendelea kutoa ushauri kwa
wanafunzi pale anapoona inafaa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote.