2013-12-17 15:24:21

Papa atuma salam za rambi rambi kutokana na kifo cha Kardinali Gordò


Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambi rambi kwa Kardinali Lluis Martines Sistach, Askofu mkuu wa Barcellona, Hispania kufuatia kifo cha Kardinali Ricard Maria Carles Gordò aliyefariki dunia, Jumanne, tarehe 17 Desemba 2013 akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Baba Mtakatifu anamwombea Marehemu Kardinali Gordò ambaye Mwenyezi Mungu alipenda kumteuwa kushiriki katika utume wa Kiaskofu, kwanza kabisa kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Tortosa na baadaye kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcellona, akajitosa kimasomaso katika mchakato wa Uinjilishaji kwa hekima na ukarimu bila kuchoka.

Alikuwa ni kiongozi mwenye ubinifu mkubwa katika shughuli za kichungaji, akaonesha ukaribu wa pekee kwa Mapadre, Watawa, Waseminaristi. Baba Mtakatifu anamshukuru sana Marehemu Kardinali Gordò kwa huduma iliyotukuka aliyotoa kwa ajili ya Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa salam zake za rambi rambi kwa wote walioguswa na msiba huu. Apumzike kwa Amani. Amina.







All the contents on this site are copyrighted ©.