Mikakati ya kichungaji mara baada ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini Hispania!
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika mkutano wake wa Mwaka uliohitimishwa hivi
karibuni linasema kwamba, athari za myumbo wa uchumi wa kimataifa zinaendelea kusababisha
majanga makubwa katika familia na maisha ya wananchi wengi Hispania. Umoja na mshikamano
wa kitaifa uko katika hali tete kutokana na misimamo tenge mintarafu ndoa na familia.
Bado kuna watu wanaendelea kuteseka kutokana na madonda makubwa yaliyoachwa na
vitendo vya kigaidi nchini humo. Bado cheche za madhulumu ya kidini dhidi ya Wakristo
sehemu mbali mbali za dunia zinaendelea kusikika na kwamba, kuna haja ya kujenga na
kudumisha mshikamano wa upendo na wananchi wa Ufilippini walioathirika kutokana na
tufani iliyoikumba nchini hiyo na kusababisha maafa makubwa ya maisha ya watu sanjari
na uharibu wa miundo mbinu. Kadiri muda unavyozidi kuyoyoma ndivyo watu wanazidi kusahau
taabu na mateso ya wananchi wa Ufilippini. Haya ni kati ya masuala yaliyojadiliwa
na Kardinali Antonio Maria Rouco Varela, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania.
Anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yatakuwa na maana iwapo waamini wataanza kufanyia
kazi changamoto za kiimani, kimaadili na utu wema, zilizopelekea Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto wa kumi na sita kutangaza Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Mmomonyoko wa tunu
hizi msingi unawakumba hata viongozi wa Kanisa wanaojikuta wakimezwa na malimwengu. Kama
anavyoendelea kuhimiza Baba Mtakatifu Francisko, kuna haja ya kufanya toba na wongofu
wa kichungaji, ili kuleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa mahalia
na lile la Kiulimwengu; daima wakijitahidi kusimama kidete kulinda na kutetea haki
msingi za binadamu na mafao ya wengi. Familia na Vijana wanapaswa kusaidiwa ili kukabiliana
na changamoto hasi katika maisha yao, kwa kujenga na kuimarisha mshikamano wa dhati. Kardinali
Varela anasema kwamba, ndoa na familia zinakabiliana na hali ngumu katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kutokana na ubinafsi unaohatarisha
tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hapa anasema kuna haja ya kukazia majiundo
makini kwa wanandoa watarajiwa sanjari na kuendeleza malezi ya ndoa na familia kwa
njia ya vyama vya kitume. Baba Mtakatifu Francisko ameona changamoto za ndoa na familia
ndio maana ameitisha Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia. Maaskofu waendelee
kuwasindikiza vijana wanaotamani kujenga familia kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, kwa
kuwasaidia kutambua kwamba, ndoa si mkataba wa mpito, bali wanandoa wanapaswa kupendana,
kusaidiana na kutakatifuzana hadi siku ile kifo kitakapowatenganisha.