2013-12-17 11:27:53

Kitabu cha Ukoo wa Yesu ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu katika historia ya binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa pamoja na wafanyakazi wa Nyumba ya Kipapa waliofika kumtakia matashi mema, Jumanne, tarehe 17 Desemba 2013 anaposherehekea Miaka 77 tangu alipozaliwa. Baba Mtakatifu amependa kujumuika na wasaidizi wake wa karibu kwa ajili ya kumwimbia Mungu utenzi wa shukrani kwa zawadi ya uhai.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko ametafakari kuhusu uwepo endelevu wa Yesu katika historia na maisha ya binadamu, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu akafanyika mwili na kuzaliwa na mwanamke na hivyo Mwenyezi Mungu ameingia katika undani wa historia ya binadamu. Huyu ndiye Emmanuel, yaani Mungu pamoja nasi.

Tangu kuanguka kwa binadamu katika dhambi, Mwenyezi Mungu akaanza mchakato wa hija pamoja na binadam, kama inavyojionesha kwa Mababu wa Imani katika Agano la Kale, kwani Mwenyezi Mungu amependa kumkomboa mwanadamu kwa njia ya historia inayojionesha tangu pale mwanadamu alipoumbwa katika hali ya utakatifu na alipojikuta anaogelea katika dimbwi la dhambi na mauti.

Katika historia ya maisha ya mwanadamu, kuna orodha ya watakatifu na wadhambi. Kuna wadhambi wakubwa ambao Mwenyezi Mungu amewatumia kuandika historia ya ukombozi.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mwenyezi Mungu anamwita kila mtu kwa jina ili kuendeleza historia anayotaka kuiandika kwa njia ya kila mwamini. Hiki ni kielelezo cha: Upendo, unyenyekevu na uvumilivu unaooneshwa na Mwenyezi Mungu.

Mara baada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko ameungana na viongozi, wafanyakazi na waamini waliokuwa kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kupata kifungua kinywa cha pamoja, kama kielelezo cha kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Injili ya Uhai.







All the contents on this site are copyrighted ©.